• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
SHINA LA UHAI: Makovu ya ubakaji tishio kwa afya

SHINA LA UHAI: Makovu ya ubakaji tishio kwa afya

Na PAULINE ONGAJI

NI mwendo wa saa mbili usiku ambapo Nadia, yuko nyumbani kwake mtaani Kariobangi, viungani mwa jiji la Nairobi.

Nadia, msichana mwenye umri wa miaka 24, anaishi pamoja na mwanawe anayekaribia miaka mitatu, pamoja na mjakazi wake. Anajiandaa kwenda kwa shughuli zake za kawaida mjini ambapo kwa takriban miaka mitatu sasa amekuwa akifanya kazi ya ukahaba.

Hii ni licha ya kuwa yeye ni mhitimu wa masuala ya kibiashara kutoka chuoni na ana ajira. Anasema kwamba uchu wake wa kujihusisha na kazi hii hautokani tu na kiu ya pesa, bali ni hisia zilizomteka baada ya kubakwa miaka mitatu iliyopita.

“Nilikuwa natoka chuoni usiku ambapo baada ya kushuka kwenye matatu, nilivamiwa na mwanamume mmoja kichochoroni na kubakwa. Ni tukio lililoniacha na hofu na woga mwingi kiasi kwamba sikuenda hospitalini kutibiwa wala kupewa dawa. Bahati nzuri ni kwamba sikuambukizwa maradhi ya zinaa, lakini nilipata ujauzito,” aeleza.

Kulingana naye, kabla ya hapo alikuwa bikira na msichana aliyezingatia maadili. “Kwa sasa suala la maadili kamwe halinijii akilini mwangu. Niliamua kufanya hivyo kwani hakuna haja ya kuendelea kujilinda na kudumisha maadili ilhali nilipokonywa kwa nguvu nilichokuwa nikikilinda kwa muda huu wote,” aeleza.

Utafiti uliofanywa Mei mwaka wa 2018 na idara ya polisi nchini, ulionyesha kwamba visa vya ubakaji na dhuluma za kimapenzi vilikuwa vimeongezeka nchini.

Sabia Mwinyi, mhudumu anayesimamia kitengo cha kuhudumia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi na kijinsia katika Hospitali ya Coast General, anasema kwamba miaka 12 tangu kuzinduliwa kwa kitengo hiki, takriban waathiriwa 8,000 wa ubakaji na dhuluma za kimapenzi wametibiwa hapo.

“Tokea Mei 2007 hadi Septemba mwaka jana, tuliwahudumia waathiriwa 7761 wa ubakaji na dhuluma za kijinsia. Aidha, kutoka Januari hadi Oktoba 31 mwaka jana, tulishughulikia waathiriwa 484,” asema Bi Mwinyi.

Ripoti iliyochapishwa na International Center for Reproductive Health ICRH mwaka wa 2012 ilionyesha kwamba 80% ya waathiriwa wa unyama huu kwa kawaida huwa wanawake, huku wengi wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Umri wa wahalifu

Kulingana na Bi Mwinyi, kwa upande mwingine watekelezaji unyama huu huwa kati ya umri wa miaka ya 20 na 40.

“Hata hivyo, katika baadhi ya visa, wahusika huwa kati ya miaka 70 na 80, au wavulana ambao hawajatimu miaka 18.

Lakini huenda kwa baadhi ya watu hizi ni takwimu tu, lakini kwa wahudumu wanaohusika moja kwa moja na waathiriwa wa ubakaji na dhuluma za kijinsia, uhalisia wa uhalifu huu haumithiliki huku wanaokumbana ana kwa ana na unyama huu wakiendelea kuuguza majeraha ya kimwili na hata kiakili.

Bi Sabia ambaye pia ni mtaalamu anayehusika na matibabu ya waathiriwa wa dhuluma za kimpenzi, anasema kwamba majeraha hasa kwa watoto huwa ya kutisha.

Mbali na maradhi ya zinaa, anasema kwamba waathiriwa hukumbwa na majeraha mabaya ya kimwili kama vile sehemu za uzazi kuharibiwa kabisa na hata vifo.

“Nimeshuhudia visa ambapo watoto wanaletwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya zaidi katika sehemu ya uzazi,” aeleza.

Mara nyingi waathriwa huwa na majeraha yanayohitaki kufanyiwa upasuaji mara kadhaa kurekebisha hali. “Hasa miongoni mwa watoto, kinachohuzunisha ni kwamba hata baada ya kufanyiwa upasuaji, wengi bado hupoteza uwezo wa kuzaa baadaye maishani,” aeleza.

Kando na majeraha ya sehemu za uzazi, kuna wale ambao hukumbwa na majeraha ya sehemu zingine za mwili hasa ikizingatiwa kwamba watekelezaji wa ubakaji na dhuluma za kimapenzi hutumia nguvu kupata wanachotaka.

“Kuna wale ambao majeraha yao huwa katika sehemu mbali na za uzazi. Kwa mfano, unaweza kupata muathiriwa na majeraha shingoni, kifuani, kwenye mapaja, huku baadhi wakipoteza maisha yao,” aeleza.

Sio hayo tu, Bi Mwinyi asema waathiriwa wengi wa ubakaji hujawa na hofu hata ya kuguswa na yeyote. “Kwa wengi, hata mguso kidogo usio na hatia waweza kumsababisha kuruka na kumshambulia mhusika,” asema.

Pia, aongeza kwamba kuna hatari ya kushika mimba ambapo hii huwakumba sana wanaokosa kufika hospitalini kupata matibabu au wanaofika wakiwa wamechelewa.

Lakini mbali na majeraha ya kimwili, kuna athari za kudumu kwa waathiriwa ambazo huanza kujitokeza baadaye maishani na zinazoweza kuharibu kabisa maisha ya muathiriwa.

Lynette Odidi, mwanasaikolojia na mwanaharakati wa afya ya kiakili mjini Kisumu, anasema kwamba kwa kawaida waathiriwa wa ubakaji hushuhudia mshtuko.

Kulingana naye, mara nyingi ameshuhudia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi na ubakaji wakikumbwa na hisia za wasiwasi, msongo wa akili na hofu.

“Ikiwa hisia hizi zitaongezeka na kuendelea kwa muda mrefu kiasi cha kuathiri maisha ya kawaida, basi huenda muathiriwa akakumbwa na hali inayofahamika kama Post-Traumatic Stress Disorder (PTSD),” aongeza.

Bi Odidi, aidha anaongeza kwamba wengi wa waathiriwa pia wanakosa motisha maishani na hata kuacha kujishughulikia. “Kuna wale ambao baada ya muda utashuhudia kwamba wanapoteza uwezo wa kuelewa hisia za wengine. Pia, kunao wanaojitenga huku baadhi wakikumbwa na hasira na ushari.

Sio hayo tu kwani anasema kwamba kuna baadhi ya waathiriwa wanaokumbwa na matatizo ya kulala. “Pengine muathiriwa atashindwa kulala, au atalala wakati usio wa kawaida. Aidha, kuna wale ambao watalala kwa muda mrefu na wengine kwa muda mfupi,” aongeza.

June P. Tangney, Profesa wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha George Mason, nchini Amerika anasema kwamba kwa kawaida waathiriwa wa ubakaji huenda wakakumbwa na hisia za kujilaumu, suala ambalo mara nyingi huwasukuma kujihusisha na maovu, kama mbinu ya kujiadhibu.

“Hisia za kujilaumu zinahusisha muathiriwa kujilaumu kutokana na unyama uliomtendekea, na anahisi kwamba endapo angefanya mambo tofauti, basi huenda hangebakwa, suala linalopelekea aibu.”

Kulingana na mwanasaikolojia huyu, kuna wale ambao hukumbwa na hisia za kana kwamba wanapitia tukio hilo la ubakaji mara kwa mara, suala ambalo huenda likaathiri uhusiano wao wa baadaye na hasa wakati wa tendo la ndoa.

Aidha, asema kwamba hisia hizi zinatokana na muathiriwa kutawaliwa na hisia za kutojithamini baada ya kubakwa.

“Kubakwa au dhuluma za kimapenzi huhusisha haki za muathiriwa kukiukwa na huenda muathiriwa akaingiwa na hisia za kutojithamini, suala ambalo laweza kumsukuma kujihusisha na uraibu wa mihadarati, pombe au hata kujihusisha na mambo kama vile ukahaba,” aeleza.

Aidha, anasema kwamba kwa upande wa watoto wanaokumbana na unyama huu wakiwa na umri mdogo, ni kawaida kwao kukumbwa na aibu. “Hii huwaweka katika hatari ya kujihusisha na mihadarati, kuanza kujihusisha na masuala ya ngono mapema au kukataa kujihusisha na masuala ya mahusiano baadaye maishani,” aeleza.

Kwa upande wa wanaume ambao wamewahi kukumbana na dhuluma za kimapenzi, utafiti kwa jina Effects of Rape on Men uliofanywa mwaka wa 2005, ulionyesha kwamba, kando na madhara kama vile msongo wa akili, wasiwasi na hamaki, wengi huchanganyikiwa kuhusu ujinsia wao.

“Waathiriwa wa kiume walihisi kana kwamba hawana nguvu kwa sababu waliamini kwamba wamepoteza fahari na hadhi yao ya kiume,” ripoti hiyo ilisema.

Bi Mwinyi anasema kwamba waathiriwa wengi husita kutafuta matibabu kwa hofu ya kuhukumiwa, suala ambalo pia huchangia hisia za aina hii baadaye maishani.

“Kumbuka kwamba matibabu haya huhusisha pia ushauri nasaha, na endapo mhusika hatohudumiwa, basi kuna pengo ambalo huachwa na huenda likasababisha matatizo hayo katika siku za usoni,” aeleza.

Ni kutokana na sababu hii ndipo Bi Odidi anasisitiza umuhimu wa kutafuta usaidizi mara moja baada ya kukumbana na unyama huu. “Ni muhimu kumuita mtu umjuaye na hasa rafiki wa karibu, baada ya kukumbana na ukatili wa aina hii. Mtu ambaye waweza kumweleza siri zako pasipo kuwa na hofu ya kuhukumiwa,” asema huku akiongeza kwamba umuhimu wa kuzungumzia tukio hili ni kwamba hukusaidia kupona.

Kulingana na Tangney, ushauri nasaha unapaswa kuhusisha suala la muathiriwa kujilaumu.

“Tiba inapaswa kushirikisha utaratibu uitwao Cognitive Restructuring au Cognitive-Behavioral Therapy. Utaratibu huu unamaanisha kumsaidia muathiriwa kujifunza kutambua mawazo potovu. Ni tiba inayohusisha kutumia ukweli wa mambo na kuunda mawazo ambayo hayajaathiriwa na majuto.”

Aidha, anasema kutokana na sababu kuwa ni vigumu kushawishi waathiriwa wengi wa ubakaji kwamba hayakuwa makosa yao, tiba hii inawasaidia kukabiliana na tatizo la aibu na hivyo kuwapa uwezo wa kuhisi salama tena.

You can share this post!

Gavana apiga muuguzi kalamu kwa kuchelewa kufika kazini

Familia kadhaa zafurushwa kutoka kipande cha ardhi...

adminleo