Makala

TEKNOHAMA: Uraibu unaduwaza wauguzi kazini

January 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

URAIBU wa mitandao ya kijamii miongoni mwa wahudumu wa afya unachangia katika kuchelewesha wagonjwa kupata matibabu hospitalini, utafiti umebaini.

Ikiwa umewahi kwenda hospitalini na ukalazimika kungojea kwa muda mrefu kwenye foleni, kuna uwezekano wahudumu wa afya waliofaa kukushughulikia walikuwa wamezama kwenye mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Twitter, Instagram, Facebook kati ya mingineyo.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Hazara nchini Pakistan na matokeo yake kuchapishwa katika jarida la Advanced Nursing, ulionyesha kuwa uraibu wa mitandao ya kijamii unaathiri pakubwa utendakazi wa wahudumu wa afya kama vile wauguzi.

“Wauguzi wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii badala ya kuhudumia wagonjwa,” unasema utafiti huo.

Utafiti huo unashauri wasimamizi wa hospitali kuwapa mafunzo wahudumu wa afya kuhusu namna ya kutumia mitandao ya kijamii bila kuathiri utendakazi wao.

Watafiti hao walihusisha wauguzi 460 kutoka mataifa 53 kote duniani.

“Watu siku hizi wanatumia mitandao wanapokuwa safarini, nyumbani au kazini. Hata hivyo, uraibu wa mitandao unaweza kusababisha madhara makubwa haswa miongoni mwa wahudumu wa afya ambao wanajihusisha na uokoaji wa maisha ya watu,” wakasema watafiti hao.

“Wahudumu wa afya, haswa wauguzi ni nguzo muhimu katika taasisi ya afya. Wauguzi ndio huhitajika kuwasaidia wagonjwa kila wakati hivyo wanapotumia muda mwingi kuzama kwenye mitandao, basi wagonjwa huumia,” wanaongezea.

Watafiti hao, hata hivyo, walisema kuwa mbali na mitandao ya kijamii, mambo mengine yanayoathiri utendakazi wa wahudumu wa afya ni mishahara duni na kufanya kazi kwa muda mrefu.

Watafiti hao waliwatumia maswali wauguzi 461 na kuwauliza namna wanavyotumia mitandao ya kijamii.

Walibaini kuwa uraibu wa mitandao ya kijamii hutatiza utendakazi wao.

“Wauguzi sawa na watu wengine katika jamii, pia wanakabiliwa na changamoto ya uraibu wa mitandao ya kijamii ambao huathiri utendakazi wao,” wakasema watafiti.

Walisema uraibu huo umeongeza mivutano miongoni mwa wauguzi au kati ya wagonjwa na wahudumu wa afya.

“Kilichotusukuma kufanya utafiti huo ni kuwa wahudumu wa afya wanafanya kazi inayohitaji umakini. Uokoaji wa maisha ya binadamu ni suala linalofaa kuchukuliwa kwa uzito,” wakasema watafiti.

Mbali na kuzubaisha wahudumu wa afya, mitandao ya kijamii pia imeshutumiwa kwa kutumiwa kueneza taarifa za kupotosha kuhusiana na matibabu.

Kulingana na mtandao wa NBCNews.com, habari za kupotosha kuhusu zaidi ya maradhi 50 zilisambazwa katika mitandao ya kijamii na kusomwa na mamilioni ya watu mwaka jana.

Maradhi ya kansa ndiyo yaliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya taarifa feki.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Stanford ulibaini kwamba idadi kubwa ya watu walidai kuwa bangi inaweza kutibu kansa.

Miongoni mwa taarifa hizo za kupotosha ni madai kwamba tangawizi inaweza kuua viini vya kansa mara 1,000 kuliko matibabu ya sasa.

Watumiaji wengine walidai kuwa majani ya papai, tende na kitunguu saumu vinatibu kansa.

Mwaka jana, Wakenya walitakiwa kupuuzilia mbali matangazo ya kupotosha yaliyokuwa yakisambazwa kupitia mitandao ya Facebook na Instagram yaliyodai kuwa tembe za PrEP zinazopunguza uwezekano wa watu kupatwa na virusi vya HIV, kwa asilimia 99 ni hatari kwa afya.

Mtandao wa Facebook ulilazimika kupiga marufuku baadhi ya akaunti za watu waliokuwa wakieneza madai hayo.

“Tembe za Truvada zina madhara tele kwa afya. Kampuni iliyozitengeneza ilificha dawa nzuri ikawauzia dawa hizo hatari,” linasema moja ya matangazo hayo.

Kulingana na mtandao wa habari wa The Guardian, matangazo hayo yalilipiwa na kampuni ya kutoa huduma za kisheria ya KBA Attorneys iliyoko Virginia, Amerika.

Matangazo hayo pia yalidai kuwa kuwa watu wanaotumia tembe za PrEP wako katika hatari ya kupatwa na maradhi ya figo; madai ambayo si ya kweli.