Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nahisi uchungu mwingi baada ya kung'oa jino

January 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

MIMI ni mwanamke mwenye umri wa miaka 33. Wiki kadhaa zilizopita niliong’olewa jino langu la nyuma kwenye utaya wa juu. Nilidhani kwamba hatua hii ingesuluhisha tatizo ambalo limekuwa likinisumbua, lakini uchungu umezidi. Hii ni kawaida?

Jessica, Nairobi

Mpendwa Jessica,

Kuna uwezekano mkubwa kwamba maumivu ya jino hilo yanatokana na mwasho wa neva kwenye mzizi wa jino hilo lililoondolewa. Hii yaweza kuwa ni kutokana na uvimbe au maambukizi. Kutokana na sababu kuwa maumivu yangalipo, kuna uwezekano kwamba maambukizi yalienea hadi kwenye ufizi au kipande kidogo cha jino kilivunjika na kusalia mle. Aidha, unaweza kupata maumivu ya jino yanayotoka katika sehemu zingine mwilini kama vile uwazi katika mfupa ndani ya fuvu unaowasiliana na mianzi ya pua, na tatizo hili haliwezi tatuliwa kwa kuondoa jino.

Unashauriwa kufanyiwa uchunguzi na daktari wa meno. Ikiwa kuna maambukizi, basi litakuwa jambo la busara kutumia viua vijasumu. Aidha, suuza mdomo wako kwa kutumia mchanganyiko wa maji yaliyopashwa moto na chumvi. Pia, waweza kutumia dawa za kukabiliana na maumivu.

 

Mpendwa Daktari,

Kwa kawaida hedhi inapaswa kudumu kwa siku ngapi?

Purity, Mombasa

Mpendwa Purity,

Hedhi ya kawaida huja baada ya kati ya siku 21 na 42 ambapo hudumu kwa kati ya siku 2 na 8. Ikiwa hedhi zitakuja kabla ya siku 20 au baada ya 42, kwa kawaida ni kutokana na tofauti ya usawa wa viwango vya homoni zinazodhibiti mzunguko wa hedhi: estrogen na progesterone. Hii inaweza kutokana na hali inayofahamika kama polycystic ovarian syndrome, matumizi ya mbinu za upangaji uzazi za kihomoni, maradhi ya tezi (thyroid disease), msongo wa akili, mabadiliko ya uzani (yaweza kuwa kuongeza au kupunguza kiwango kikubwa cha uzani) na mazoezi kupita kiasi. Wakati mwingine, hedhi zisizo za kawaida zaweza kutokana na matatizo ya uterasi kama vile uterine polyps, fibroids, au jeraha la tishu kwenye uterasi (Asherman’s syndrome).

 

Mpendwa Daktari,

Mimi ni baba wa mabinti wawili ambapo nawalea peke yangu. Mabinti zangu hawa wanakaribia umri wa kubalehe. Nitaanzaje kuwazungumzia kuhusu masuala ya ngono?

Faustine, Nairobi

Mpendwa Faustine,

Unapaswa kuanza mjadala huu kuambatana na jinsi mtoto wako anavyoelewa suala hili tokea utotoni ili iwe shughuli ya utaratibu. Ni vyema ikiwa watoto tayari wana uhuru wa kujadili miili yao kabla ya kuanza kushuhudia mabadiliko makubwa. Ikiwa wanajua majina na kazi za sehemu hizi za miili, basi waweza wafahamisha zaidi kuhusu sehemu hizi au uhusiano na watu wengine. Aidha waeleze kuhusu sehemu nyeti za mwili zisizostahili kuguswa na watu wengine. Unaweza anzisha mjadala pengine kutokana na maoni ya mmoja wao, au kutoka kwa tukio kwenye kipindi cha televisheni na kadhalika. Ikiwa baadhi ya mada zinafedhehesha kutokana na suala la jinsia, unaweza kumtumia jamaa au rafiki unayemuamini. Hata hivyo, jambo muhimu ni kwa watoto wako kuhakikishiwa upendo wako na kwamba utawakubali kwa vyovyote ili wawe na uhakika kwamba hautakasirishwa na swali lolote wanalokuelekezea.