• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Mkutano wa tatu wa BBI kufanyika katika uwanja wa Tononoka

Mkutano wa tatu wa BBI kufanyika katika uwanja wa Tononoka

Na CHARLES WASONGA

KAUNTI ya Mombasa itakuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa uhamasisho kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Mkutano huo umeratibiwa kufanyika katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa hii ikiwa ni kulingana na makubaliano yaliyofikiwa Jumatatu katika mkutano wa magavana wa Pwani uliongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga afisini mwake jijini Nairobi.

Mkutano wa kwanza ulifanyika mnamo Januari 10, 2020, mjini Kisii ambapo viongozi wa uliokuwa mkoa wa Nyanza walitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ambayo wangetaka yafanyiwe ripoti hiyo.

Walipendekeza katiba ifanyiwe marekebisho ili kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili.

Ripoti ya sasa inapendekeza Waziri Mkuu asiye na mamlaka makuu na ambaye atateuliwa na Rais kutoka chama au muungano wenye idadi kubwa ya wabunge.

Mkutano wa pili ulifanyika katika uwanja wa michezo wa Bukhungu mnamo Jumamosi 18, 2020.

Mikutano hiyo yote ilihudhuriwa na Bw Odinga ambako siasa zilishamiri huku wafuasi wa Naibu Rais William Ruto wakidai mikutano hiyo ilikuwa na lengo la kupigia debe azma ya Bw Odinga ya kuwania urais mwaka 2022.

‘Si lazima Raila awe Rais’

Lakini akihutubu uwanjani Bukhungu, Bw Odinga alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa mchakato huo haulengi kumsadia kuingia Ikulu.

“Sio lazima niwe Rais wa Kenya lakini tunashiriki shughuli hii kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata Rais bora,” akauambia umati katika uwanja huo.

Licha ya kutisha kuusia mkutano huo wakidai kutohusishwa katika maandalizi yake, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula walibadili msimamo dakika za mwisho na kufika uwanjani humo.

Baadhi ya magavana waliokutana na Bw Odinga Jumatano kujadili maandalizi ya mkutano wa BBI awamu ya Pwani ni; Ali Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Godhana Dhadho (Tana River) na Granton Samboja (Taita Taveta).

You can share this post!

Klopp aambia Liverpool, tulieni taji lingali mbali

Knut yatetea walimu kukiwa na madai wanaamuru watoto wasio...

adminleo