• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Ngilu azindua ambulansi 10 kusaidia wagonjwa mahututi

Ngilu azindua ambulansi 10 kusaidia wagonjwa mahututi

 Na KITAVI MUTUA

Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu Jumanne alizindua ambulansi 10 ambazo zitatumika kuwahudumia wakazi hasa wakati wa majanga ya kidharura.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta ya afya na utoaji wa huduma bora.

Ambulensi hizo sasa imefikisha idadi ya magari hayo kaunti kuwa 35. Hata hivyo, 10 yaliyotolewa sasa yana vifaa vya kisasa kusaidia kuwaokoa wagonjwa waliopo katika hali mahututi.

Kwa mujibu wa Bi Ngilu, ambulensi hizo zitagawanywa kwa maeneobunge manane katika kaunti hiyo ili pia kuwahudumia wakazi wanaotoka mashambani.

Afisa Mkuu wa Afya kaunti, Dkt Richard Muthoka, alifichua kwamba ambulensi hizo zilinunuliwa kwa Sh9.5 milioni na zilifuata sheria mpya za utoaji zabuni zilizoasisiwa na wizara ya Afya kuanzia mwaka uliopita.

“Magari hayo yote 10 yana mashine za kisasa za teknolojia zinazotumika kuwasaidia wagonjwa mahututi wapate fahamu. Pia yana mashine ambazo zinasaidia akina mama kujifungua kabla ya kufika hospitalini,” akasema Dkt Muthoka.

Vile vile, madereva ambao wanatarajiwa kuendesha ambulensi hizo wamepokea mafunzo maalum ya jinsi ya kuwashughulikia wagonjwa, aliongeza.

You can share this post!

Jaji Mumbi ajiondoa kwa kesi ya Sonko

Nzige sasa waharibu mimea Baringo na Turkana

adminleo