• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Ingwe wakaribia kujaza pengo la Kitambi

Ingwe wakaribia kujaza pengo la Kitambi

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya KPL, AFC Leopards, wamefichua kwamba wako pua na mdomo kupata huduma za mkufunzi mpya atayelijaza kwa mafanikio pengo la kocha Dennis Kitambi ambaye atakatiza rasmi uhusiano wake na wapambe hao wa soka ya humu nchini mnamo Mei 2018.

Kitambi ambaye ni mzawa wa Tanzania anapigiwa upatu wa kutua nchini Bangladesh kuungana na mkufunzi wa zamani wa Leopards, Stewart Hall ambaye aliwahi kushirikiana naye kukitia makali kikosi cha Simba SC, Tanzania.

Leopards ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 17, walimpokeza Kitambi mikoba ya kikosi hicho mnamo Machi 2018 baada ya usimamizi wa miamba hao kuagana rasmi na mkufunzi wa zamani wa Bidco United na Ulinzi Stars, Robert Matano ‘The Lion’.

Chini ya Kitambi, Leopards wamejivunia ushindi katika jumla ya michuano minne, kusajili sare moja na kupoteza mechi moja kati ya sita iliyopita.

Ni matokeo ambayo yanawaweka Leopards katika nafasi nzuri ya kuendeleza ushindani mkali dhidi ya wapinzani wao wakuu msimu huu, wakiwemo Gor Mahia na Mathare United ambao hadi kufikia sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali.

“Leopards watakuwa wamempata kocha mpya kufikia mwisho wa wiki ijayo. Kwa sasa usimamizi umepiga hatua kubwa katika mazungumzo yanayolenga kurasimisha ujio wa mkufunzi atakayemrithi Kitambi ambaye amefichua mipango ya kuondoka mwishoni mwa mwezi huu,” akasema Mwenyekiti wa Leopards, Dan Mule.

Ingawa Mule hakufichua jina la kocha huyo atakayepokezwa chombo cha Leopards, kinara huyo alidokeza kuwa kikosi chake kimekamilisha mazungumzo na makocha watatu – kutoka Tanzania, Ufaransa na Argentina ambao wote kwa sasa wananoa klabu za soka barani Afrika.

You can share this post!

Korti yaagiza Boinnet afurushe Mnigeria kipenzi cha...

KCB yatuza kikosi cha voliboli

adminleo