Mgogoro wa kiitifaki wanukia Mombasa mkutano wa uhamisisho BBI
Na CHARLES WASONGA
HUENDA mgogoro wa kiitifaki ukashuhudiwa Jumamosi katika mkutano wa uhamisisho kuhusu ripoti ya muafaka wa maridhiano (BBI) mjini Mombasa.
Hii ni endapo Naibu Rais William Ruto atahudhuria mkutano huo baada ya wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kuahidi kushiriki mkutano huo katika uwanja wa Tononoka.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kuongoza mkutano huo kama ambavyo amekuwa akifanya katika mikutano ya awali yaliyofanyika katika miji ya Kisii na Kakamega.
Seneta wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala amesema kuwa Bw Odinga ndiye atahutubu wa mwisho katika mkutano huo hata kama Dkt Ruto atakuwepo.
“Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ndio vinara wawili, na wa kipekee, wa mchakato wa BBI. Kwa hivyo, endapo Rais hatahudhuria mkutano wa Mombasa, Raila ndiye ataongea wa mwisho hata kama Ruto atakuwepo,” akasema Jumanne usiku katika kipindi ‘Sidebar’ kwenye runinga ya NTV.
Akaongeza: “Tunawaalika wanachama wa ‘Tangatanga’ katika mikutano yetu ya BBI lakini wajue kuwa kinara wao sharti atii itifaki yetu sio ile ya serikali. Ile yao inatumika tu katika sherehe za kitaifa.”
Bw Malala, ambaye ni naibu kiongozi wa wachache katika seneti, alisisitiza kuwa itifaki ya serikali ambapo Bw Odinga huongea kabla ya Dkt Ruto haitatumika katika mikutano ya BBI “kwa sababu handisheki ilikuwa kati ya watu wawili pekee.”
Na wabunge wanne wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamedokeza huenda viongozi wa ‘Tangatanga’ wasipewe nafasi ya kuhutubu katika mkutano huo wa Mombasa.
Mbw Junet Mohammed (Suna Mashariki), Kanini Kega (Kieni), Fatuma Gedi (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Wajir) na Seneta wa Nairobi walisema viongozi wa Mombasa ndio wataamua ni kina nani watahutubu katika mkutano wa Tononoka.
“Tunawakaribisha wenzetu ambao wameingiwa na roho mtakatifu na kuamua kuunga mkono BBI. Lakini wasilete fujo na kutaka kuuteka mkutano wetu wa Mombasa kwa kulazimisha wapewe nafasi ya kuongea,” akasema Bw Mohammed ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa.
Naye Bw Kega akaeleza: “Sisi sote tutakuwa wageni kule Mombasa. Na ni viongozi wenyeji ndio watapata fursa ya kuangazia masuala kuhusu huko wanayotaka yajumuishwe katika BBI. Huenda baadhi yetu wageni, na hata wao, tusipate nafasi ya kuongea,”
Aidha, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, Jumatano amelionya kundi la ‘Tangatanga’ dhidi ya kuzua rabsha katika mikutano inayopaniwa kuhamasisha ripoti ya jopo la maridhiano nchini (BBI).
Mbunge huyo wa Chama cha ODM na anayeegemea kundi linalounga mkono Rias Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga, amesema kwa vyovyote vile hawatakubali azma ya kuunganisha taifa kusambaratishwa.
“Tunakaribisha wenzetu, wameonesha mkondo tuliochukua ni wa kuunganisha taifa na kuleta amani. Lakini tunawaambia mkuje kwa njia ya adabu,” akasema Junet kwenye kikao na waandishui wa habari jijini Nairobi.
Kauli ya mbunge huyo inajiri siku moja baada ya kundi la ‘Tangatanga’ na ambalo linaegemea upande wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto kutangaza kuunga mkono hamasisho la ripoti ya BBI.
Seneta wa Elgeyo Marakwet na ambaye pia ni kiongozi wa wengi seneti Jumanne alitoa taarifa kwa niaba ya wabunge wa kundi hilo kwamba watakuwa wakishiriki mikutano ya kuhamasisha BBI mashinani.
Wikendi iliyopita hali ya mshikemshike ilishuhudiwa Mumias pale baadhi ya wabunge hao walipania kufanya mkutano wa hadhara na ulioonekana kupinga BBI.
Wakati huo huo kiongozi wa ODM Raila Odinga aliongoza kundi la ‘Kieleweke’ katika uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega kupigia upatu BBI.
Azma ya ‘Tangatanga’ ilizimwa, maafisa wa usalama wakitumia gesi ya vitoa machozi kuwafurusha.
Kwenye kikao na waandishi wa habari Jumatano Junet ambaye pia ni kiranja wa wachache bungeni alieleza kushangazwa kwake na ‘Tangatanga’ kudai itakuwa ikishiriki mikutano ya kuhamasisha ripoti ya BBI ilhali inasema itakuwa na mikutano yake binafsi.
Kampeni ya BBI wikendi ijayo inatarajiwa kuelekezwa eneo la Pwani.
“Yaliyoshuhudiwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya wakati wa kuzindua rasmi ripoti ya BBI yasionekane. Tunashangaa wakisema wana mkutano mwingine, ilhali wanadai wameungana nasi,” akasema.
Akionekana kucharura kundi hilo, Junet alionya kuwa Kieleweke iko tayari kukabiliana nao endapo watazua mtafaruku.
“Wakija, waje na nia njema,” Junet akasema.
Wengine waliozungumza katika kikao hicho ni pamoja na seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na mbunge wa Kieni Kanini Kega.
Jopokazi la BBI lilibuniwa 2018 na kiongozi wa taifa Uhuru Kenyatta na mwenzake wa upinzani, ODM, Raila Odinga, kupitia salamu za maridhiano maarufu kama handisheki kufuatia mgawanyiko kushuhudiwa nchini katika uchaguzi mkuu wa 2017.