• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
Sonko akesha akiomba kesi ya kuvamia askari itupwe

Sonko akesha akiomba kesi ya kuvamia askari itupwe

Na WAANDISHI WETU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko alikesha Jumanne akiomba kesi dhidi yake ya kumshambulia afisa wa polisi itupiliwe mbali.

Maombi hayo yalianza nje ya mahakama ya Voi, ambapo Bw Sonko alionekana akibubujikwa na machozi, afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ilipowasilisha ombi la kumuondolea mashtaka hayo.

Bw Sonko alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Facebook na kuchapisha video aliyonukuu “Mambo ya Mungu ni Mengi.”

Akifafanua sababu iliyomfanya kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Bw Sonko, afisa aliyeripotiwa kushambuliwa na gavana Bw Rashid Yakubu, alisema alichukua hatua hiyo baada ya moyo wake kumwelekeza kusamehe na kusahau.

“Sikushinikizwa na Sonko. Simjui na sijawahi kukutana naye. Mimi ni Mwislamu na huwa siweki kisasi. Alinishambulia lakini nikaamua kumsamehe,” alisema Bw Yakub.

Kufuatia hatua hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Voi, Bw Fredrick Nyakundi, jana alifutilia mbali kesi ya kumshambulia afisa wa polisi akiwa kazini.

Afisa huyo alikuwa amemshtaki gavana Sonko dhidi ya kumpiga teke kwenye paja alipokuwa akimkamata katika Uwanja wa Ndege mjini Voi mnamo Disemba 6, mwaka jana.

Kuondolewa kwa kesi hiyo bila shaka ni afueni kuu kwa Bw Sonko anayekabiliwa na mashtaka mengine, ikiwemo kesi ya ufisadi kuhusu zabuni ya uzoaji taka ya Sh357 milioni kinyume cha sheria.

Hakimu alisema kulikuwa na sababu kamili kwa kesi hiyo kufutiliwa mbali, na kwamba, mshukiwa hakupinga maamuzi hayo na hakukuwa na chuki kati ya mshukiwa na mlalamishi.

“Baada ya kuliangalia ombi lililotolewa na mwendeshaji wa mashtaka ya umma (DPP) kuwa mshukiwa asamehewe mashtaka, ninakubaliana na ombi hilo na kwa hivyo, kesi hii imeondolewa rasmi,” akasema.

Na jana, Bw Sonko alifika kortini kisirisiri akiandamana na mawakili wake wakiongozwa na Bw Cecil Miller.

Baadhi ya wafuasi wake, akiwemo mbunge wa zamani wa Kibwezi Magharibi, Bw Kalembe Ndile na wawakilishi wa wadi wa kaunti ya Nairobi pia walikuwepo.

Awali, Bw Sonko alikuwa amekosa kufika kortini, baada ya wakili wake Bw George Kithi kueleza mahakama kwamba alikuwa mgonjwa.

Ripoti za LUCY MKANYIKA, BRIAN OCHARO na MARY WAMBUI

You can share this post!

RIZIKI: Ndoto zake za biashara ‘hazikufa’ licha ya...

Washukiwa 43 wa ugaidi kukaa kizuizini siku 2

adminleo