• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:40 AM
‘SUPASTAA’ MARTINELLI: Tineja aifungia Arsenal mabao 10 katika msimu mmoja

‘SUPASTAA’ MARTINELLI: Tineja aifungia Arsenal mabao 10 katika msimu mmoja

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KINDA Gabriel Martinelli mwenye umri wa miaka 18, alifunga bao la kusawazisha dhidi ya Chelsea, na kuwa tineja wa kwanza kufungia Arsenal mabao 10 katika msimu mmoja, tangu Nicholas Anelka msimu wa 1998-99.

Lakini beki Shkodran Mustafi amelaumiwa vikali na mashabiki kwa kufanya makosa yaliyoiweka kifua mbele Chelsea, katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Uingereza (EPL) iliyochezwa Jumanne usiku uwanjani Stamford Bridge.

Baada ya kupewa kichapo cha 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza nyumbani Emirates, Arsenal ilijituma sana na kuhakikisha imetoka na alama moja, baada ya mechi kukamilika 2-2.

Katika kisanga cha Mustafi, beki huyo alijaribu kumrudishia mpira kipa wake Berno Leno, lakini ukachukuliwa na mshambuliaji Tammy Abraham ambaye kiasha aliangushwa na David Luiz katika kisanduku akielekea kufunga bao.

Luiz alionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa hilo huku Chelsea wakipewa penalti, ambayo ilimiminwa wavuni na Jorginho.

Kosa hilo na mengine mengi ya awali yaliwafanya mashabiki wa Arsenal kupendekeza Mustafi apigwe mnada kwa bei ya kutupa sokoni, hata ingawa alinunuliwa kwa kitita cha Sh4.8 bilioni akitokea Valencia mnamo 2016.

Arsenal hawakucheza vizuri lakini walistahili heko kwa kupambana kijasho baada ya kubali wachezaji 10 uwanjani.

Isitoshe, walitoka nyuma na kusawazisha mabao yote mawili kila walipofungwa, na kulazimisha sare hiyo.

Makosa mengi katika safu ya ulinzi ya Arsenal yalisababisha nahodha Cesar Azipilicueta kufungia Chelsea bao la pili dakika ya 84.

Lakini Arsenal walipambana na kupata lao la pili kupitia kwa beki Hector Bellerin, aliyepiga kombora kali kwa mguu wa kushoto baada ya kumchanganya beki mwenzake, Emerson.

Chelsea watajilaumu kwa kutoshinda mechi hiyo ambayo walitawala kwa kipindi kikubwa huku wakikosa kumalizia nafasi walizopata. Lakini sare hiyo imewawezesha kubakia katika nafasi nzuri ya kukita katika mduara wa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA), msimu ujao.

Kwa Arsenal, kupoteza kungewaweka katika hali mbaya zaidi, ikikumbukwa kwamba wanashikilia nafasi ya 10, kwa tofauti ya pointi 10 nyuma ya Chelsea wanaoshikilia nafasi ya nne.

Kinda Martinelli alionekana kuishiwa nguvu, lakini kocha Mikel Arteta alimuamini kabla ya kufunga bao hilo la kwanza la kusawazisha, akimpita mbio kiungo N’Golo Kante aliyeteleza na kuanguka katikati ya uwanja.

Arsenal yatoka sare

Kabla ya kukutana Jumanne usiku, Chelsea walifungwa 1-0 na Newcastle ugenini St James Park wakati Arsenal ikitoka sare 1-1 na Sheffield United nyumbani Emirates.

Kufikia sasa, Chelsea wameshindwa mara nne kati ya michezo 23 ya ligi msimu huu, wakiwazidi Manchester United kwa pointi sita katika nafasi ya tano.

Mechi ya Jumanne ilikuwa ngumu kwa kocha Frank Lampard ambaye anatarajiwa kufanya usajili baada ya Chelsea kupunguziwa marufuku ya miaka miwili kutosaini wachezaji.

Arsenal waliingia ugani Stamford Bridge wakiwa hawajapata ushindi katika mechi nne za ugenini zilizopita. Wametoka sare dhidi ya Everton, Bournemouth, Crystal Palace, Sheffied United na juzi Chelsea.

Aidha, Gunners hawajashinda mechi yoyote nyumbani kwao Emirates tangu walaze Manchester United 2-0, siku ya Mwaka Mpya. Lakini hawajafungwa ugenini tangu Novemba 9, 2019, walipochapwa 2-0 na Leicester City.

You can share this post!

Bao la Aguero lasaidia City kuondoka na ushindi finyu

UJUZI NA MAARIFA: Fundi aliye na ujuzi wa kuunda ua wa...

adminleo