• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Pesa zinazomwagwa wakati wa kampeni zaiponza Kenya

Pesa zinazomwagwa wakati wa kampeni zaiponza Kenya

Na MARY WANGARI

KENYA imerudi nyuma kwa alama moja kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi ambapo imeorodheshwa nambari 137 miongoni mwa mataifa 180 ulimwenguni, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa Alhamisi na shirika la kimataifa la Transparency International.

Katika Orodha ya Kimataifa kuhusu Ufisadi (CPI) iliyotolewa na shirika hilo, Kenya ilifanikiwa kujizolea alama 28 miongoni mwa jumla ya alama 100.

Hii inamaanisha kuwa Kenya ilikosa kufikisha kiwango cha jumla kinachohitajika kimataifa cha alama 43 na kiwango kinachohitajika Barani Afrika cha alama 32.

Aidha, Kenya imeoredheshwa nambari 137 miongoni mwa mataifa 180 yaliyohusishwa katika utafiti huo huku matokeo hayo yakithibitisha ulegevu katika juhudi za kuangamiza ufisadi kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa TI.

“Tangu 2012 Kenya imepata alama baina ya 25 na 28 zikiwa ni za chini mno ikilinganishwa na alama 100. Aidha, iliandikisha alama 27 mnamo 2018. Hii inaonyesha juhudi za kupiga vita ufisadi zinaendelezwa kwa kasi ya chini mno. Katika orodha hiyo, Kenya iko katika nafasi ya 137 miongoni nchi na maeneo 180 yaliyohusishwa katika utafiti,” ilisema taarifa kutoka kwa TI.

Rwanda iliongoza bara la Afrika ikijitwalia alama 53 na kufuatiwa na Tanzania iliyopata alama 37.

Kenya na Uganda zilifuatia kwa alama 28 huku Burundi na Sudan Kusini zikiandikisha alama 19 na 12 mtawalia.

Mataifa mengine yaliyohusishwa katika utafiti huo ni pamoja na Ethiopia iliyonyakua alama 37, Nigeria alama 26, Zimbabwe alama 24 na Zambia alama 34.

Licha ya kupitisha Sheria kuhusu Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi Nchini 2013 Kenya imekosa kudhibiti hela zinazotumika katika kampeni, hali inayolemaza juhudi za kukomesha ufisadi kulingana na taarifa hiyo.

Bunge limeahirisha utekelezaji wa sheria hiyo hadi katika uchaguzi wa 2022 na kulemaza zaidi uwezo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuangazia na kudhibiti hela zinazotumiwa katika kampeni.

“Hii imefanya chaguzi nchini Kenya kuwa miongoni mwa shughuli ghali zaidi Afrika, hali ambayo inapaswa kurekebishwa.

“Serikali ni sharti ziangazie kwa dharura nafasi ya ufisadi kuhusu kiwango kikubwa cha hela katika ufadhili wa chama cha kisiasa na ushawishi usiofaa unaoshinikiziwa mifumo yetu ya kisiasa,” alisema Delia Ferreira Rubio, Mwenyekiti wa Transparency International.

Alisema ili kuwezesha umma kuwa na imani na serikali, ni sharti vitengo husika vya serikali vilivyotwikwa jukumu la kukomesha ufisadi, vionyeshe matokeo halisi.

Visa vya hivi majuzi ambapo wanasiasa maarufu ikiwemo kurejeshwa kwa mali ya umma iliyoibiwa ni miongoni mwa juhudi zitakazofanikisha kukomesha ufisadi nchini kulingana na ripoti hiyo.

You can share this post!

‘Inahitajika dharura kuokoa elimu ya mtoto wa kiume...

Wafanyakazi watano wa kaunti ya Kiambu wakanusha shtaka la...

adminleo