• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Ruto: Tusipewe masharti kuhusu BBI

Ruto: Tusipewe masharti kuhusu BBI

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema kuwa hakuna kundi lolote linalopaswa kutoa kanuni kwa Wakenya kuhusu vile wanapaswa kushiriki kwenye mchakato wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Kauli yake inajiri baada ya wabunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), Kanini Kega (Kieni) na Seneta Johnstone Sakaja wa Nairobi kuwaonya wabunge wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ dhidi ya ‘kuvamia’ mchakato huo.

Watatu hao walisema kuwa ingawa wanawakaribisha wenzao kutoka ‘Tangatanga’, “wanapaswa kuwa na heshima.”

Lakini akihutubu Alhamisi katika eneo la Kariobangi Kusini, jijini Nairobi, Dkt Ruto alisema kuwa mchakato huo unahusu maisha ya Wakenya wote, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa na usemi.

“BBI inahusu mustakabali wa Wakenya. Kenya ni yetu sote, hivyo, hakuna mtu ama kundi linalopaswa kudai kuimiliki. Tuko tayari kutoa maoni yetu,” akasema Dkt Ruto alipozindua miradi kadhaa katika eneo hilo.

Mnamo Jumanne, wabunge wanaomuunga mkono Dkt Ruto walisema kuwa wanaunga mkono kikamilifu mchakato huo.

Na ili kuonyesha uungwaji mkono wake, walisema kuwa watahudhuria mkutano wa kuipigia debe ripoti hiyo utakaofanyika kesho katika Uwanja wa Tononoka, jijini Mombasa.

Wabunge hao waliongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Bw Kipchumba Murkomen, Kiranja wa Wengi katika Seneti Bi Susan Kihika, mbunge Moses Kuria kati ya wengine

Dkt Ruto alisema kuwa kamati inayoongoza mchakato huo inapaswa kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanapewa nafasi kutoa maoni yao na hautekwi na wanasiasa kama jukwaa la kuendeleza chuki na ukabila.

“Kamati ya BBI inapaswa kuweka utaratibu ambapo kila Mkenya atapata nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo bila kuingiliwa na wanasiasa. Inapaswa kuhakikisha mchakato huu umelindwa dhidi ya mwingilio wa aina yoyote ile,” akasema Dkt Ruto.

Mnamo Jumanne, Bw Murkomen, ambaye pia ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, alisema kuwa watahudhuria mikutano hiyo, ili kuondoa dhana kwamba wanapinga mchakato huo.

Dkt Ruto amekuwa akionekana kutengwa kwenye mipangilio ya  maandalizi ya mikutano hiyo, huku washiriki wakuu wakiitumia kumshambulia kisiasa.

Naibu Rais hakuonekana katika mikutano ya Kisii na Kakamega, licha ya kusema anaunga mkono uratatibu huo.

Tayari, imebainika kuwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamebuni kundi maalum la wanasiasa ambao wataongoza kampeni hizo, ambapo Dkt Ruto na waandani wake wameachwa nje.

Wadadisi wanasema kuwa lengo kuu la kundi hilo kubadili msimamo wake kighafla linalenga kuondoa dhana kuwa Dkt Ruto anapinga ripoti hiyo, licha ya kuwa ajenda ya serikali.

You can share this post!

Watu 3 wafariki wakizima moto nchini Australia

Lionesses waalikwa kushiriki Raga za Dunia Canada

adminleo