• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya miujiza ya Mtume SAW ambayo kila Muumin afaa kuijua

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya miujiza ya Mtume SAW ambayo kila Muumin afaa kuijua

Na HAWA ALI

KILA sifa njema zinamstahikia Allah (subuhanahu wata’ala) Mola wa viumbe vyote.

Swala na salamu zimuendee kipenzi cha ummah Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam). Ndungu wa Kiislamu, wapo watu wanaoshuku Utume na miujiza ya Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam. Ningependa kukudondolea nukta hizi muhimu kuhusu mada hii.

Kuwa alidhihirisha miujiza na alama mbali mbali ambazo hazidhihirishwi ila na Mitume wa Allah; kwani Sunnah ya Allah Ta’ala imepita katika mikono ya Manabii waliopita imevunja ada (mazoea) ili iwe ni miujiza kwao, na dalili ya ukweli wao, na nia ya kusimamisha hoja kwa kaumu yao, na miujiza ya kila Mitume ilikuja kwa jinsi ambayo kaumu ya mtume yule ilivyopiga maendeleo katika jambo fulani.

Hivyo basi muujiza wa Musa (‘Alayhi salaam) ukanasibiana na jinsi kaumu yake ilivyopiga hatua katika fani maalumu; nayo ni fani ya uchawi, Allah kwa miujiza aliompa Musa akabatilisha uchawi wao, na wakashindwa kushindana na Musa katika hilo pamoja na werevu mkubwa na uhodari wa hali ya juu waliokuwa nao katika aina mbalimbali za uchawi.

Kaumu ya Issa (‘Alahyi Salaam) waliiga maendeleo makubwa katika fani ya utabibu na madawa, Allah akawaponya katika mikono ya Issa (‘Alahyi Salaam) katika maradhi yaliyoshindikana kutibiwa kiasi cha kuwa Allah akawafufua wafu katika mikono ya Issa (‘Alahyi Salaam).

Miujiza yote hii ilikuwa ni ya kihisia (yaani yenye kuonekana), imefungamana na mahali na zama maalum, haina sifa ya kilimwengu na kudumu, miongoni mwa miujiza ya Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ni kama miujiza ile ya kihisia; miongoni mwa miujiza hiyo ni:

  • Kububujika maji kutoka katika vidole vya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam).
  • Chakula kidogo kukifanya kingi kiasi cha kula yeye pamoja na Waislamu wengine walio nae, na kubakia.
  • Kufanya maji kuwa mengi kiasi cha kunywa jeshi zima na kutawadha.
  • Gogo kumlilia alipoacha kulitumia katika mimbari.
  • Jiwe kumsalimu alipokuwa Makkah.
  • Mti kumnyenyekea yeye.
  • Changarawe kusabahi katika kiganja chake.
  • Kuponya magonjwa kwa uwezo wa Allah, na mengineyo,

Qur’an imerekodi moja katika miujuza ile muujiza wa Israa na Miiraji; Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) alipopelekwa Israa kutoka msikiti wa Masjid Al-Haram Makkah kuelekea Al-Masjidil Aqswaa, kisha akapaishwa Mii’raj kutoka katika msikiti wa Aqswa hadi mbingu ya saba, Allah Ta’ala amesema: “SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.” (17:1).

Vivyo hivyo muujiza wa kupasuka kwa mwezi; ambapo Allah Ta’ala amesema: “Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!” (54:1),

Na hii ilitokea wakati makafiri walipomtaka Mtume Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) athibitishe ukweli wake kwa muujiza uliokuwa wazi kabisa, na wakaainisha wazi awapasulie mwezi, na kuahidi kuwa baada ya hapo wataamini, siku hiyo ya tukio ilikuwa ni siku ya mwezi kamili (Badri), yaani: usiku wa siku ya kumi na nne ya mwezi; ambao mwezi unakuwa kwa ukamilifu wake na kwa uwazi zaidi..

Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) akamuomba Mola wake ampe walichokiomba; mwezi ukapasuka mara mbili: nusu ikawa juu ya mlima wa Saffa na nusu nyingine juu ya Jabali Qayqu’aan inayoelekeana nayo, baada ya kupatikana kwa muujiza huu mkubwa washirikina wa Kikureishi hawakuamini, bali waliuzingatia kuwa ni uchawi, na huu ndio mwendo wa wapingaji wa dini ya Allah.

Ni kawaida ya wapingaji pindi haki inapobomoa utawala wao na nuru ya Allah inapofunika upotofu wao, hapo hufanya vitimbi na kusimama mbele yake, ima kwa kupotosha misingi yake au kugeuza hakika zenyewe, kwa dhana ya kuwa hayo yatatosha kumaliza na kuangamiza ukweli wenyewe, Allah amesema:

“Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea. Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.” (68:2-3)

You can share this post!

Olunga atafaulu kupiku Kipchoge tuzo za SOYA leo Ijumaa?

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Methali na misemo ya Abagusii...

adminleo