Habari

Mahakama yamuagiza Prof Kiama ajitenge na shughuli za usimamizi wa UoN

January 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Nairobi leo Ijumaa imemuagiza Prof Stephen Gitahi Kiama, ambaye uteuzi wake kuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) ulitenguliwa, asiingilie shughuli za usimamizi wa asasi hiyo.

Jaji Maureen Onyango, wa Mahakama ya Masuala ya Ajira na Mahusiano ya Leba, ametoa maagizo hayo akitilia zingatio kwamba masuala yaliyoibuliwa na pande zinazohasimiana ni sharti yajadiliwe na muafaka kupatikana kuhusu uhalali wa Prof Kiama kuwepo katika wadhifa huo.

Uteuzi wa Prof Kiama ulianza kutekelezwa mara moja Januari 6, 2020, lakini Waziri wa Elimu George Magoha akaufuta katika kile alidai kuwa baraza la UoN lilikosa kuipa serikali ruhusa ya mashauriano ikiwemo kumjulisha Rais wa Jamhuri.

Prof Magoha alimteua Prof Isaac Meroka Mbeche kaimu Naibu Chansela, hatua iliyosababisha mvutano na hatimaye VC but that marked the kufanya Prof Kiama na waziri kuwasilisha kesi mahakamani.

Prof Kiama aliwasilisha kesi akipinga hatua ya waziri kutengua uteuzi wake na Tume ya Huduma za Umma (PSC).

Kupitia kwa wakili Fred Ngatia, msomi na mtaalamu huyo alitaka uteuzi wake utambuliwe na pande zote katika chuo kikuu hicho.

Mahakama ilimruhusu kuendelea kuhudumu, lakini Magoha akawasilisha kesi kutaka Kiama aenguliwe ili kuruhusu Prof Mbeche aendelee kuhudumu katika wadhifa wa Naibu Chansela.

Ijumaa mahakamani, Jaji Onyango ameagiza Prof Kiama akae kando hadi kesi ya waziri Magoha isikizwe Alhamisi wiki ijayo.

Jaji Onyango ametoa agizo hilo baada ya wakili Evans Monari, anayewakilisha waziri na Mwanasheria Mkuu, kuiomba mahakama itoe ufafanuzi wa agizo la Januari 20, 2020, lililotupa kwa muda hatua ya waziri Mahoga kumteua Prof Mbeche kama kaimu Naibu Chansela.

Wiki jana, jaji alisitisha utekelezaji wa barua iliyoidhinisha Prof Mbeche kama kaimu Naibu Chansela, akisema PSC ilimteua Prof Kiama kuiongoza UoN kwa kufuata hatua muhimu kisheria.

Mawakili Ngatia na Ahmednasir Abdullahi anayewakilisha chuo hicho wamepinga Bw Monari kuwakilisha waziri na Mwanasheria Mkuu, wakisema hajateuliwa kisheria kuwasilisha serikali katika masuala yanayohusu migogoro ya kiusimamizi.

Wakati huo huo, Muungano wa Wafanyakazi wa Kiakademia wa Vyuo Vikuu (Uasu), kupitia wakili Titus Koseyo, umeitaka mahakama iweke kando agizo kwamba Prof Kiama atambuliwe kama Naibu Chansela.