• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
TAHARIRI: Harambee wapeni Wakenya furaha

TAHARIRI: Harambee wapeni Wakenya furaha

Na MHARIRI

MNAMO Alhamisi, Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), lilitangaza droo ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2022 kati ya timu za Afrika.

Kwenye droo hiyo, Kenya ilitiwa katika kundi moja na Mali, Uganda na Rwanda.

Kwa tathmini ya mbali, japo wengi wanaliona kama rahisi, ukweli ni kwamba, ni kundi gumu sana.

Uganda na Mali ndizo timu nzito zaidi ambazo sharti Harambee Stars ijiandae vyema na kucheza kwa umakinifu, iwapo ina ndoto ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika nchini Qatar.

Unapotumia fainali za Afrika (AFCON) za mwaka jana kama kigezo, hali inayojitokeza ni kuwa Uganda inaipiku Kenya kwa mbali. Maadamu taifa hilo lilipiga hatua tamanifu sana huku Kenya ikishindwa kusonga mbele.

Kwenye fainali hizo zilizofanyika Misri, Uganda ilimaliza katika nafasi ya pili kundini, nyuma ya wenyeji hao walioongoza kundi. Jamhuri ya Congo na Zimbabwe zilifuatia mtawalia.

Unapotazama mchezo wa timu ya Uganda, almaarufu Cranes, utakubali kuwa kwa sasa inaipiku kwa mbali Kenya. Ndiyo sababu hata FIFA inaiorodhesha katika nafasi bora duniani kuliko Kenya.

Kwenye fainali hizo za Misri, Mali iliongoza Kundi E lililojumuisha miamba kama Tunisia na Angola ambazo zilifuatia, huku Mauritania ikishika mkia.

Kwa hivyo, litakuwa kosa kubwa iwapo Kenya itachukulia mechi hizo za kufuzu kwa mzaha eti kwa sababu haikupangwa na majabali wa bara kama vile Nigeria, Ghana, Cameroon, Misri na Algeria.

Sharti Kenya, ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya 106 duniani, ijizatiti zaidi iwapo ina hamu ya kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa angalau mara ya kwanza tangu ulimwengu kuumbwa. Mali inaorodheshwa katika nafasi ya 56 duniani huku Uganda ikishikilia nafasi ya 77.

Hiyo ni ishara tosha kuwa mambo si rahisi jinsi baadhi ya mashabiki wanavyofikiria. Hata Rwanda ambayo inashikilia nafasi ya 131 duniani isifanyiwe masihara.

Kenya ifanye nini ndipo iimarishe nafasi yake ya kufuzu? Sharti ifanye mazoezi makali huku benchi la kiufundi likibuni mbinu za kipekee za kushinda miamba wa kundi hilo; Mali na Uganda.

Serikali kwa ushirikiano na FKF pia zinafaa zihakikishe kuwa timu inapata ufadhili wa kutosha, wakati inapojiandaa na pia kucheza mechi hizo za kufuzu.

You can share this post!

Kivumbi chanukia ‘Tangatanga’ wakishiriki...

MWITHIGA WA NGUGI: Viongozi waunganishe Wakenya si...

adminleo