• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
HUWAWEZI: Liverpool yapiga wenyeji Wolves

HUWAWEZI: Liverpool yapiga wenyeji Wolves

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

VIONGOZI Liverpool walipiga hatua kubwa katika juhudi zao za kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kung’ata Wolves 2-1 uwanjani Molinuex usiku wa kuamkia Ijumaa.

Vijana wa Jurgen Klopp, ambao watamaliza ukame wao wa miaka 30 bila taji hili wakishinda mechi tisa zijazo, walivuna ushindi wao wa 22 kutokana na mechi 23 walizosakata kupitia kwa mabao ya Jordan Henderson na Roberto Firmino.

Liverpool iliingia mchuano huo na rekodi nzuri dhidi ya Wolves baada ya kuwapiga wapinzani hao mara saba mfululizo ligini.

Henderson alifungua ukurasa wa magoli dakika ya nane baada ya kukamilisha kona safi kutoka kwa Trent Alexander-Arnold kupitia kwa kichwa chake.

Liverpool, ambayo ilikuwa imeshinda Bournemouth, Watford, Leicester, Wolves, Sheffield United, Tottenham na Manchester United kwa jumla ya mabao 15-0 katika mechi saba za ligi zilizopita, ilipata pigo dakika ya 33 pale mshambuliaji wake na mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2019, Sadio Mane alipoumia.

Raia huyo wa Senegal alipata jeraha la mguu, ambalo ripoti zinadai huenda likamkosesha mechi tatu zijazo dhidi ya Shrewbury (raundi ya nne ya Kombe la FA) na West Ham na Southampton kwenye ligi.

Nafasi yake ilijazwa na Takumi Minamino. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Mjapani huyo kupata nafasi ya kushiriki mechi ya ligi tangu ajiunge na Liverpool mnamo Januari 1, 2020 akitokea Red Bull Salzburg nchini Austria.

Dakika sita baada ya kipindi cha pili kuanza, Wolves, ambayo ilikuwa imelemea Liverpool 2-1 mara mbili katika mechi tisa zilizopita, lakini kwenye Kombe la FA, ilisawazisha 1-1 kupitia kwa Raul Jimenez.

Mshambuliaji huyo wa Mexico alipokea krosi murwa kutoka pembeni kulia kutoka kwa mvamizi matata wa Uhispania Adama Traore na kummwaga kipa Alisson Becker kupitia kwa kichwa chake.

Mbrazil Becker alipangua mashambulizi mengine mawili hatari kutoka kwa Jimenez na Traore, lakini mabao ya kuchelewa yameonekana kuipendelea Liverpool katika kampeni yake, na haikuwa tofauti katika mechi hiyo.

Timu hiyo ilipohitaji nafasi moja tu ya kubadilisha mkondo wa mechi hiyo kabisa, raia wa Brazil Firmino ndiye aliyejitokeza na kukamilisha pasi ya Henderson kwa ustadi katika dakika ya 84.

Baada ya mechi, Klopp alisifu vijana wake kwa ushindi huo akisema ulikuwa “jibu tosha” kwa presha kali kutoka kwa ‘Mbwa Mwitu’ wa kocha Nuno Espirito Santo.

Mjerumani huyo pia aliridhishwa na soka ya Minamino, na Traore, ambaye vilevile aliimiminia Liverpool sifa akisema ndiyo “timu bora barani Ulaya.”

You can share this post!

Bei ghali ya Wanyama yafukuza wanunuzi

RAGA ZA DUNIA: Shujaa yaanza vibaya kampeni yake ya duru ya...

adminleo