MWANAMUME KAMILI: Athari ya domo kaya kuwepo kizazi kisichojua uwajibikaji
Na DKT CHARLES OBENE
TANGU udogoni, nilijua fika kwamba jamii ya Wakenya kwa jumla ni watu wanaopenda mzahamzaha mno.
Tumekuza sifa kama watu wasiochelea kuliumbua jambo ama kulipa uzito usiostahili na kufanya upepo mwanana kuwa chamchela ama kimbunga. Ndio maana tunaitwa watu wa ajabu na tabia za kustaajabisha! Kweli, hatujaacha kustaajabisha.
Kweli, sisi ni jamii ya watu tunaopenda kusemasema hasa vibarazani. Tunapenda kuzungumza angalau tusikike ila hatutilii maanani mambo tunayosema. Athari ya domo kaya ni kuwepo kizazi kipya kisichojali maana ya uwajibikaji maishani. Tunapenda kufanya kazi ya midomo kuliko kazi ya misuli na akili. Hatuna aibu kufuata kivuli; minofu kigodani hata kama mashamba yanaota kuvu na mimea kufia kuko huko.
Kwanza, tumejaaliwa msimu wa masika; mvua kutwa kucha lakini “tuko hapa hapa” kulalama kama kawaida. Tuko papa hapa na ngebe; “mbona mvua haijapusa angalau kutuachia muda wa mabaraza na vikao vya ulaji miraa?” Isitoshe, nilikuwa vijijini nikapigwa butwaa! Ndio kwanza wanaume wameanza kuchanja kuni mashambani kwa ajili ya kuota moto. Eti wanahofia baridi asubuhi. Kwani huo sio mzaha wa jamii ya Wakenya?
Sivyo nilivyotarajia madume haya kufanya hasa ikizingatiwa kwamba wenda kipindi cha ukame kikafuata masika tunayoona sasa. Iweje wanaume na misuli yote hiyo wanataka ota moto wakati tunahitaji wakulima mashambani? Kama vijitoto vya chekechea vinahimili baridi na matone ya mvua asubuhi kwenda kuongeza kasi ya ukuaji vyuoni, mbona watu wazima – wanaume hasa – kutika nyumbani kuota moto?
Pili, huu mzaha wa nzige umepita mipaka! Kwa zaidi ya wiki moja, tumekuwa tukilalama mno juu ya uvamizi wa nzige! Tazama mwelekeo alioutoa aliyekuwa waziri wa Kilimo – kwamba tuonapo wadudu wanaofanana ama tukiwafananisha na nzige, tuwapige picha – ama tupigwe picha nao – kisha tuzisambaze picha zenyewe mitandaoni angalau kumpa yeye waziri nafasi ya kutathmini ukweli wa kuwepo nzige nchini. Hayo ndiyo mawazo ya mstahiki waziri wa Kilimo.
Mbona wananchi wapewe kazi ya kutafuta nzige na kuwapiga picha? Kwani wanasayansi wa serikali hawajafika kazini kutoka likizo ya Desemba? Najua kwamba ningali mzito wa akili lakini wangapi kati yetu tunajua nzige? Hivi tulivyodhikika kutafuta masurufu na karo kwa watoto wendao kidato cha kwanza, tuupate wapi muda wa kupiga picha ama kupigwa picha na nzige?
Sijapata kuona mwanamume aliyeondokewa na akili namna hiyo. Natumai atapata nafasi nzuri kujihoji binafsi na kutambua kama kweli angali mwanamume kamili, tena kiongozi mwendesha masuala ya serikali. Haistahimiliki kuona viongozi wakifanya mzaha ama wakitania maisha ya watu wanaosubiri na wanaotegemea hekima na bidii ya viongozi wao.
Hilo liwe funzo kwetu, hasa akina sisi tunaotembeza viwiliwili bila kujua tuendako ama tufanyacho kimaisha. Tulisema mwanzoni kwamba huu ni mwaka wa wanaume kujituma ipasavyo na hatuna budi kufafanua vivyo hivyo.
Baadhi yetu tuliotii agizo la waziri sio watu wenye akili timamu. Nasema hivi kwa ukakamavu na ujasiri maana tulifanya mzaha usio kifani. Picha zilizopakiwa mitandaoni zilidhamiria kumdhihaki waziri badala ya kumpa kazi ya kufanya. Si kuku, si sokwe, si mende, si nzi, si majibwa, si nungunungu, si kumbikumbi, si mchwa na wadudu wengine wa ajabu! Nilivyodhani jamii ya Wakenya ni watu wenye shughuli za tija, tena watu waliosoma ama waliosomeshwa wakajua maana na thamani ya muda!
Vituko hivi tuvionavyo mitandaoni ni ishara tena ithibati ya jinsi wanaume kwa wanawake wa leo walivyopungukiwa hekima na akili. Jukumu la watu wazima ni kutambua thamani ya kufanya kazi za tija na kuheshimu hadhi ya watu wazima kujituma kwa manufaa ya jamii na familia.
Hizi picha za ajabu zilizotumiwa waziri hazikufaa kamwe. Afadhali muda huo tungeutumia mashambani ama viwandani kuchumia pato. Mwanamke na mwanamume kamili ni watu wanaotumainiwa kimaisha. Ndio maana nawasihi kusitisha mzahamzaha huu wanaofanya kina yakhe wa leo.