• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Wanaojidai wamiliki ardhi Manda-Maweni watatiza shughuli za wakazi 2,000 wanaotegemea uchimbaji mawe

Wanaojidai wamiliki ardhi Manda-Maweni watatiza shughuli za wakazi 2,000 wanaotegemea uchimbaji mawe

Na KALUME KAZUNGU

WACHIMBAJI mawe na wapiga kokoto eneo la Manda-Maweni, Kaunti ya Lamu wanahofia kupokonywa fursa za kufanya kazi zao kufuatia hatua ya baadhi ya mabwanyenye ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitwaa udhibiti wa vipande vya ardhi.

Kijiji cha Manda-Maweni kiko na zaidi ya wakazi 2,000 ambao wengi hutegemea uchimbaji wa mawe na kokoto kujikimu maishani.

Katika kikao na wanahabari kijijini Manda-Maweni Jumapili, wakazi hao walisema baadhi ya machimbo yao ya mawe na kokoto tayari yamezingirwa ua na baadhi ya mabwenyenye na wawekezaji binafsi wanaodai kumiliki ardhi hizo.

Msemaji wa wachimba migodi, Bw James Chege alisema mara nyingi imekuwa vigumu kwao kufikia machimbo yao ya mawe na kokoto kwani hulazimika kuwaomba ruhusa wanaojidai kuwa wamiliki wa ardhi husika kwanza kabla ya kukubaliwa kuendeleza shughuli zao.

Bw Chege aliitaka serikali ya kaunti ya Lamu kupitia Gavana, Fahim Twaha kuingilia kati na kusuluhisha tatizo la ardhi eneo la Manda-Maweni ili wakazi waishi bila hofu.

“Ikiwa serikali ya kaunti haitaingiulia kati na kutatua migogoro ya ardhi inayoendelea hapa Manda-Maweni, basi hata sisi wachimba mawe na kokoto tutakosa kazi zetu. Kuna mabwanyenye ambao wanaendelea kuvamia ardhi za shughuli za mawe na kuzitwaa kama zao binafsi. Baadhi ya migodi yetu ya tangu jadi tayari imezingirwa ua na wanyakuzi. Haturuhusiwi kuingia vivi hivi kwenye machimbo hayo ya mpaka tupewe ruhusa na wanaojidai kuwa wamiliki. Tunateseka hapa,” akasema Bw Chege.

Bw Fredrick Otieno aliiomba serikali ya kaunti kuzitambua ardhi za migodi ambazo ziko Manda-Maweni na kuzitangaza kuwa za umma.

Alisema kuna haja ya serikali ya Kaunti kufikiria kutoa hatimiliki maalum kwa ardhi za migodi ili kuepuka kunyakuliwa na mabwenyenyenye na wawekezaji wengine wa kibinafsi.

“Hapa Manda-Maweni sisi hutegemea uchimbaji mawe na kokoto pekee kukimu familia zetu na kusomesha watoto wetu. Ni vyema serikal;I ya kaunti kupitia Gavana wetu, Fahim Twaha kutoa hatimiliki maalum kwa ardhio zote za machimbo. Ardhi hizo zifanywe kuwa za umma ili zilindwe kutoka kwa hawa wanyakuzi. Ikiwa zitaachwa hivyo na kunyakuliwa zote sisi tutabaki bila kazi hapa,” akasema Bw Otieno.

Bi Nancy Irungu ambaye ameishi kijijini Manda-Maweni tangu 1986 alishikilia haja ya usoroveya kufanywa kwa ardhi za eneo hilo na kila mkazi kugawanyiwa kipande chake cha ardhi na hatimiliki ili kuzilinda ardhi hizo kutokana na wanyakuzi ambao wanadaiwa kuzikodolea macho.

Bi Irungu alisema wakazi wengi eneo hilo wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kufurushwa wakati wowote kutokana na kwamba hakuna hata mmoja ambaye serikali imemkabidhi hatimiliki kwa ardhi anayokalia.

  • Tags

You can share this post!

MAVIZIONI: Arsenal kucheza dhidi ya Bournemouth

Shujaa yapiga Afrika Kusini, yasonga hatua 1

adminleo