• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
DIMBA PWANI: Karate inavyozua msisimko licha ya vizingiti vya udhamini

DIMBA PWANI: Karate inavyozua msisimko licha ya vizingiti vya udhamini

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KARATE ni mojawapo ya michezo ambayo inaendelea kupata umaarufu katika jimbo la Pwani na hasa katika Kaunti ya Mombasa ambapo kuna klabu kadhaa za mchezo huo.

Wanakarate kadhaa wamewahi kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa na kufanya vizuri.

Kwenye mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ya Taifa Open Individual JKS Championship katika uwanja wa shule ya Greenwood Groove Academy, Nyali mjini Mombasa, wanakarate kadhaa wa Pwani walishiriki na kupata medali nyingi za dhahabu, fedha na shaba.

Mkurugenzi wa Shotokan Academy, Walid Timimy aliambia Dimba kuwa kutokana na jinsi washiriki wadogo na wakubwa walioshiriki kwenye mashindano hayo ya siku mbili, imedhihirisha wazi kuwa mchezo wa karate eneo la Pwani unazidi kuimarika.

“Tuna uhakika kama mashindano kama hayo yaliyotayarishwa na Japan Karata Shotorenmei (JKS) yatakuwa yakifanyika mara kwa mara, vijana wetu watapiga hatua kubwa ya maendeleo na wengi wataweza kuwika kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa,” akasema Timimy.

Mkurugenzi huyo alisifu Munawwarah Karate Club kwa jinsi inavyouchukulia mchezo huo kwa umuhimu na akatoa ombi kwa klabu nyingine zifanye bidii ili jimbo la Pwani litoe wanakarate wengi hata kwa timu ya taifa itakayoshiriki kwenye mashindano na michezo ya kimataifa.

Alisema ni jambo la kujivunia kuwa kuna klabu nyingi za mchezo huo katika kaunti zote sita za jimbo la Pwani za Lamu, Mombasa, Kwale, Kilifi, Taita Taveta na Tana River lakini ukosefu wa udhamini ndio pingamizi kubwa ya kuwafanya vijana wakose kushiriki mashindano ya kimataifa.

“Kama serikali za kaunti pamoja na serikali kuu zingeliwadhamini wanakarate waliofuzu kwenda kushiriki mashindano na michezo mbalimbali ya kimataifa, basi Pwani ingelikuwa sehemu itakayotoa wachezaji wazuri zaidi humu nchini,” akasema Timimy.

Alisema ameongea na maafisa wa Shirikisho la Karate la Kenya (KKF) kuwasihi wakubali ombi lake la Shotokan Academy ikishirikiana na serikali ya Kaunti ya Mombasa wakubaliwe kuandaa mashindano ya kitaifa ya Kenya Open Karate Championship ya mwaka wa 2020.

“Tutawasilisha ombi letu hilo kirasmi kwa kuiandikia KKF na tunatarajia maafisa wake watalikubali ili tuanze matayarisho ya mapema,” akasema Timimy anayeamini kuwa Kenya inaweza kufanya vizuri kwenye mashindano yoyote ya kimataifa mipango mizuri ikifanyika.

Nahodha wa timu ya Munawwarah KC, Labib Said anasema kuwa wamefurahikia kwa kupata tuzo kadhaa na hiyo imetokana na juhudi za maafisa na ushirikiano wao pamoja na wachezaji na wazazi wa vijana walioko katika klabu hiyo.

Said aliwashukuru wadhamini wa timu yake na akatoa ombi kwa klabu za karate za jimbo la Pwani pamoja na nyinginezo kote nchini wadumishe umoja na ushirikiano ili hali ya mchezo huo nchini Kenya uimarike na kutambulika kote duniani.

“Ninaamini kama maafisa wa klabu pamoja na wale wa KKF watashirikiana na kuwa wamoja, hakuna litakalozuia timu za Kenya kutamba na kuibuka washindi kwenye mashindano yote ya kimataifa,” akasema nahodha huyo wa Munawwarah KC.

Naye Mwenyekiti wa Swahili Pot Hub, Mahmood Noor almaarufu Mentor 001 alisema wakati wa kumalizika kwa mashindano hayo ya Taifa Open kuwa kuna umuhimnu mkubwa wa kuinua hali ya michezo kwa vijana na hasa wale wa jimbo la Pwani.

Noor aliomba kuweko na mawasiliano ya karibu baina ya klabu za jimbo la Pwani ili ziweze kusaidiana ili vijana wafanikiwe kuwa wanakarate wa majina makubwa.

“Kama klabu za Pwani zitakuwa zikisaidiana, basi nina hakika sio karate pekee bali hata michezo mingine itaimarika,” akasema.

Seneta wa Kaunti ya Mombasa, Mohamed Faki aliyekuwa mgeni wa heshima katika mashindano hayo ya Taifa Open alisema amefurahia kuona jinsi washiriki walivyopambana na kuonyesha viwango vya juu vya mchezo huo wa karate.

“Ninaamini kama kutakuwa na mashindano kama haya mara kwa mara, nina uhakika vijana wengi wataweza kuwa wenye kutambulika kimataifa na kuwa maarufu sawa na walivyo maarufu wanariadha wa hapa nchini,” akasema.

Alisema ameshuhudia na kutambua kuwa mchezo wa karate unajenga nidhamu na afya ya mwili huku pia ukileta uhusiano bora kati ya wanakarate wa sehemu mbalimbali za nchi ya Kenya.

“Kwetu Mombasa, nimefurahi kuona vijana wengi wakishiriki mashindanoni,” akasema Faki.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Mbona mpenzi alinikana baada ya kuhamia...

BBI: Viongozi zaidi ya 150 wa Jubilee wakutana Naivasha

adminleo