TAHARIRI: Kulipa watu wazae ni mzaha usiofaa
Na MHARIRI
VIONGOZI wanapopewa mamlaka ya kusimamia masilahi ya umma, hutarajiwa kuonyesha busara katika utendakazi wao.
Wanatarajiwa kuja na mbinu na mipango inayoweza kuwasaidia wakazi, kukabiliana na changamoto za maisha. Mambo hayo, ni kama vile kupatikana kwa huduma muhimu karibu na mwananchi, pamoja na watoto kupata elimu na mafunzo kwa urahisi.
Kwa muda sasa, katika maeneo mengi ya nchi, kuna wanafunzi waliopota vyema na kuitwa wajiunge na shule za upili, lakini hawajaweza kwenda. Ni juzi tu tuliporipoti visa vya wanafunzi kufika shuleni kwa kutembea kwa miguu maili nyingi. Wengine walibeba masanduku pekee bila chochote.
Katika maeneo mengi ya nchi, vijana wanakaa mabarazani wakiwa hawana shughuli. Baadhi yao, wamejiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya na uhalifu, kama sehemu ya kupitisha wakati.
Haya ndiyo mambo ambayo kiongozi anapaswa kuyafikiria na kuyatafutia suluhu, wala si kuwaahidi watu pesa wanapopata uja uzito.
Wikendi, mbunge mmoja eneo la Meru aliwahimiza wakazi wapate ujauzito, na kuahidi kuwa kila mmoja atapata Sh1,000.
Kwamba hatua hiyo inanuiwa kuhimiza watu kuzaa, kwa vile wanaume wameshindwa na majukumu yao ya ndoa kutokana na ulevi wa kupindukia.
Jambo linalofanya watu wa eneo hilo wasizaane, ni kuzama kwa wanaume katika ulevi. Hilo ndilo tatizo ambalo kiongozi huyo anapaswa kulikabili, na wala si wanawake kupata uja uzito. Iwapo mwanaume ameingia katika ulevi wa kupindukia, hata akimpa mkewe uja uzito hatakuwa na uwezo wa kulea mimba wala kumpa malezi bora mwanawe.
Isitoshe, Sh1,000 kwa mtu kushika mimba ni mzaha. Hizo ni pesa ambazo hazitoshi hata kwenda kliniki kwa miezi mitatu. Mja mzito ana mahitaji mengi ya pesa. Hata kama zingekuwa Sh10,000, mwanasiasa huyo na wenzake kote nchini wanafaa kuelewa kuwa, mtoto atakapozaliwa atakuwa na mahitaji ya kimsingi. Mwanasiasa hatakuwa na familia husika kuipa matunzo hadi mtoto akomae.
Tatizo la ulevi ni changamoto kote nchini. Viongozi wanapaswa kuja na mbinu za kulikabili bila ya kuwaongezea watu mzigo zaidi.
Badala ya kuwahimiza wazaane ilhali mwanasiasa hatawajibikia malezi, viongozi wanapaswa kuwahamasisha wanaume watafute njia mbadala za kufurahia bonasi ya mavuno yao. Mojawapo ni kuachana na ulevi wa kupindukia na kusahau majukumu yao nyumbani.