• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
KAULI YA MATUNDURA: Mgogoro wa ushairi wa Kiswahili ulivyomtia matatani mtaalamu Mugyabuso Mulokozi

KAULI YA MATUNDURA: Mgogoro wa ushairi wa Kiswahili ulivyomtia matatani mtaalamu Mugyabuso Mulokozi

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO 2017, nilifanya utafiti kuhusu ‘mgogoro wa ushairi wa Kiswahili’ uliozuka mnamo miaka ya 1960.

Mgogoro huo miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili ulichochewa na masuala mawili. Kwanza, utata kuhusu maana ya ushairi kwa jumla. Iliki, maana ya ushairi wa Kiswahili. Mgogoro huo ulizua mapote mawili yaliyokinzana. Pote la kwanza lilikuwa na wanamapokeo au wahafidhina.

Pote la pili lilikuwa la wanamapinduzi au wanamabadiliko. Baadhi ya wanamadiliko walikuwa ni pamoja na kina Jared Angira, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein, Crispin Haule, Mugyabuso Mulokozi, Fikeni Senkoro, Alamin Mazrui na Kulikoyela Kahigi – miongoni mwa wengine walioanza kuandika ‘mashairi ya kisasa’.

Wanamapokeo walikuwa ni pamoja na Kaluta Amri Abedi, Abdilatif Abdalla, Shihabbuddin Chiraghdin, Hassan Mwalimu Mbega, Saadan Kandoro, Jumanne Mayoka, Mathias Mnyampala miongoni mwa wengine. Utafiti wangu ulilenga kuutathmini mgogoro huo miaka hamsini baadaye. Je, ulififia? Ungalipo? Hatima yake ilikuwa ni ipi? Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika Jarida la Mwanga wa Lugha Juzuu 1 Na. 2 ; la Idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Moi. Nilidhani kwamba mgogoro huo ulikuwa wa kiakademia tu. Hata hivyo, nilishangazwa wiki iliyopita kwamba mgogoro huo ulivuka mipaka ya kiakademia na kuwaathiri vibaya baadhi ya wanamapinduzi.

Mmoja wa wanamapinduzi aliyeumia kwa sababu ya msimamo aliouchukua kuhusiana na mgogoro huo ni Prof Mugyabuso Mulinzi Mulokozi. Kwenye makala yake: ‘Pambazuko la Taaluma ya Fasihi ya Kiswahili Afrika Mashariki: 1968 -1980’ yaliyochapishwa katika Lugha Na Fasihi : Essays In Honour And Memory of Elena Bertoncini Zubkova (2019). Prof Mulokozi anadai kwamba, kwa sababu ya msimamo wao (yeye na wanausasa wenzake), njama zilifanywa kumzuia asiajiriwe katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) au Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 1975, licha kwamba alikuwa na sifa zote za kitaaluma zilizohitajika.

Wengine waliojipata matatani kutokana na mgogoro huo ni Kulikoyela Kahigi na Zubeida Tumbo Masabo. Mulokozi anasema kwamba njama hizo zilifanikiwa kwa muda tu. Alikuja kuajiriwa na TUKI mnamo 1979. Mhakiki Elena Bertoncini – Zubkova, ambaye kwa muda mrefu alifundisha katika Chuo Kikuu cha Napoli, nchini Italia alifariki 2018. Kazi ya mtaalamu huyu iliyoacha taathira kubwa mno katika taaluma ni Outline of Swahili Literature: Prose, Fiction and Drama (1989). Kazi hii ambayo aliiandika kwa ushirikiano na Prof S.A. Mohamed, Prof K.W. Wamitila na Dkt Mikhail Gromov ndiyo kazi ya pekee inayojaribu kutoa taswira kamili ya fasihi ya Kiswahili na waandishi wa fasihi hiyo tangu miaka ya 1960.

Mwangwi wa ‘mgogoro wa ushairi wa Kiswahili’ bado ungalipo. Utafiti wangu ulibainisha kwamba licha kwamba mgogoro huo haujabainisha au kujitokeza wazi miaka hamsini baadaye, utaendelea kuathiri kwa kipindi kirefu jinsi au namna utanzu wa ushairi wa Kiswahili unavyotazamwa na wahakiki. Diwani za mashairi zinazotungwa hivi sasa zinajumuisha mashairi yanayofuata arudhi ya yale yasiyofuata kanuni za utunzi wa mashairi alizopendekeza Kaluta Amri Abedi katika Sheria ya Kutunga Mashairi Na Diwani ya Amri (1954).

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. Yeye pia ni mfasiri wa Moses Series (Oxford University Press).

 

[email protected]

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Tufurahikie hatua ya wenzetu kupigia upatu...

SEKTA YA ELIMU: Serikali iipige jeki elimu ya watoto wenye...

adminleo