Matayarisho ya Olimpiki yanoga Japan
Na MASHIRIKA
TOKYO, Japan
WAANDALIZI wa Tokyo 2020 wanakamilisha hatua za mwisho huku ikisalia chini ya miezi sita kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki.
Hata hivyo, suala linalopatiwa kipaumbele na waandalizi hao bado limesalia kujiandaa kwa janga lolote la kimaumbile linaloweza kuzuka wakati wa michezo hiyo.
Huku maelfu ya raia wa kigeni wakitarajiwa kufurika jijini Tokyo kwa hafla hiyo itakayoanza Julai 24 hadi Agosti 9, waandalizi wamemakinika pakubwa kuhusu haja ya kutoa maagizo dhahiri kwa Kiingereza na kutoa uhamasishaji kuhusu kinachohitajika kufanywa endapo mitetemeko ya ardhi au tsunami itatokea.
Hapo jana, wakazi zaidi ya 200 jijini Tokyo ambao ni miongoni mwa karibu raia wa kigeni 570,000, walikusanyika katika Kituo cha Spoti cha Musashino Forest ambacho kitaandaa michuano hiyo wakati wa Olimpiki, ili kudurusu hatua zinazolenga kuwafanya stadi zaidi katika kukabiliana na majanga.
Pamoja na kufanyia majaribio vifaa vya kugundua mitetemeko ya ardhi, washiriki pia walifunzwa jinsi ya kutumia vifaa vya kuzima moto, kutembea katika vyumba vilivyojaa moshi, kupigia polisi simu wakati wa dharura na hata mazoezi yanayofaa unapokwama katika kituo cha uokoaji.
Japan ni mojawapo wa mataifa yanayoathiriwa zaidi na majanga ulimwenguni kama vile dhoruba na mitetemeko ya ardhi huku ikishuhudia jumla ya mitetemeko ya ardhi 1,500 kwa mwaka, ingawa ni visa vichache vinavyosababisha uharibifu wowote, au hata vifo.
Hata hivyo, wataalam wanaamini kwamba kuna uwezekano wa asilimia 70 ya mtetemeko mkuu wa ardhi kukumba jiji kuu la Japan katika kipindi cha miaka 30 ijayo.
Kwa sababu hii, raia hao wa kigeni walikaribisha ushauri wote ambao wangeweza kupata.
“Kwa serikali ya Japan kuandaa hafla kama hii, hakika inasadia raia wa kigeni kama mimi kwa sababu watoto nchini Japan tayari wamefunzwa shuleni lakini sisi hatuna habari yoyote,” alisema mwanafunzi kutoka Vietnam, Hoa Nguyen, ambaye ameishi Japan kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Zaidi ya wakalimani 30 wanaozungumza lugha sita tofauti walikuwa tayari kuwasaidia washiriki kutoka mataifa 44.
“Nafikiri inashangaza juhudi wanazotumia kukueleza ujiandae, ujiandae, ujiandae kwa sababu ni rahisi kuishi maisha ya kila siku na usijali kuhusu hilo,”
“Hivyo basi serikali ya Tokyo imefanya kazi murwa kwa hafla kama hizi,” alisema Rodrigo Coronel, balozi wa Nicaragua, Japan.