Kimataifa

Nchi kadha zapinga mpango wa Trump kuhusu Palestina

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MPANGO wa kurejesha amani katika eneo la Mashariki ya Kati uliotangazwa na Rais wa Amerika Donald Trump umeibua hisia mseto katika mataifa mbalimbali huku Wapelestina wakiupinga vikali.

Huku Uingereza na Umoja wa Mataifa (UN) zikisifia mpango huo uliotangazwa Jumanne, mataifa ya Kiarabu yameupinga yakisema unapendelea Israel.

Mpango huo unaipa Israeli mengi ambayo imekuwa ikipigania kwa miongo kadha kama vile udhibiti wa Jerusalem kama mji wake mkuu, wala sio mji ambao itatumia pamoja na Palestina.

Vilevile, mpango huo unairuhusu Israeli kutwaa eneo la makazi ya West Bank huku ukiitaka taifa la Palestina kusitisha vita.

Akitangaza mpango huo mnamo Jumanne katika Ikulu ya White House akiwa ameandamana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Trump alisema mpango huo utaleta mwamko mpya katika Mashariki ya Kati.

“Kwa pamoja, tunaweza kuleta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa manufaa ya mataifa hasimu ya Israeli na Palestina,” Trump akasema mbele ya wageni waliojumuisha Waisraeli na Waamerika Wayahudi. Hakuna Mpalestina hata mmoja alikuwa miongoni mwa umati uliomsikiza Rais huyo wa Amerika.

Lakini Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas alipuuzilia mbali mpango huo akisema nchi yake bado inapania kutwaa Jerusalem kutoka udhibiti wa Israeli.

“Baada ya upuzi ambao tuliusikia leo (Jumanne) tunasema ‘la, mara elfu moja’ kwa mpango huo,” Abbas akasema kwenye kikao na wanahabari katika mji wa Ramallah ulioko West Bank, ambao ndio makao makuu ya Mamlaka ya Palestina.

Alisema Wapalestina watafanya kila wawezalo kuwafurusha Israeli na kuunda taifa huru lenye makao yake makuu mashariki mwa Jerusalem.

“Hatutapiga magoti na hatutakufa moyo au kujiuzulu,” Abbas akasema. Hata hivyo alisisitiza kuwa Wapalestina watapinga mpango huo kwa njia “ya amani na itakayoungwa mkono na wote.”

Sami Abu Zhuri, afisa wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza, alisema taarifa ya Trump ni “dhalimu na itachochea ghadhabu.”