Makala

Vyama vya Ushirika vinavyosaidia kuweka akiba na kutoa mikopo kufadhili biashara ndogondogo na zile za kadri

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

BW Roger Wekhomba ambaye ni mwekezaji katika biashara ya uongezaji thamani mazao ya kilimo na mimea alikuwa na kizingiti kimoja tu wakati akianza; ukosefu wa fedha kuafikia malengo yake.

Maarifa na ujuzi, alikuwa nayo ila mtaji – fedha ama mali inayotumika kuanzishia au kupanulia biashara au shughuli yoyote ile kujiimarisha kimapato na kimaendeleo ilikuwa balaa bin belua.

Aliweza kufanikisha azma yake baada ya kuweka akiba kwa miaka kadhaa na pia kupigwa jeki na mfadhili.

Mjasirimali huyo anakiri ukosefu wa fedha hususan miongoni mwa vijana ndiyo changamoto kuu inayowakumba kuafikia shabaha yao katika kilimobiashara, na pia kujiunga na sekta ya biashara ndogondogo na zile za kadri, ndiyo SMEs.

“Ile kuu ni ukosefu wa mtaji, ikifuatwa na ufahamu wa biashara bora kuwekeza, jambo linalohitaji utafiti wa kina na kuangaziwa,” asisitiza.

Ni kizingiti ambacho vijana wenye talanta mbalimbali na maono kinazidi kuwakera na kuzima ndoto zao.

Hata hivyo, uwekaji akiba kidogo kidogo ambacho hatimaye hujaza kibaba, kulingana na wataalamu wa masuala ya fedha na biashara ni mojawapo ya suluhu kufanikisha azma yoyote ya uwekezaji.

Benki, vyama vya ushirika na makundi, ni baadhi ya mashirika ya kifedha yanayotoa huduma za uwekaji fedha, ambazo huzaa faida na pia kutoa mikopo kwa wafanyabiashara.

Anderson Kimathi, mtaalamu na meneja wa Chama cha Ushirika cha Southern Star, tawi la Githurai, Nairobi anaungama wafanyabiashara wengi hasa wateja wa Sacco hiyo wameimarika kupitia uwekaji akiba na ununuzi wa hisa, kisha wanapata mikopo. “Zaidi ya asilimia 90 ya wateja wetu ni SMEs, ambao huweka akiba ya hadi Sh20 kwa siku,” anasema.

Kuanzisha biashara au kuingilia kilimo, kulingana na mtaalamu huyo si lazima mwanzilishi awe na maelfu au mamilioni ya pesa.

“Ukiwa na hata chini ya Sh5, 000, unaweza kuingilia biashara ya uuzaji wa nguo, uipalilie polepole,” Kimathi aelezea.

Anaongeza kusema: “Tuna wateja wanachama waliotangulia kwa mkopo wa chini kidogo na sasa biashara zao zina thamani ya maelfu na mamilioni ya pesa.”

Akitoa mfano wa Sacco ya Southern Star ambayo imekuwa ikitoa huduma za fedha kwa takriban miaka 25 nchini, Kimathi anasema ili kujisajili unahitaji Sh300 pekee na nakala ya kitambulisho cha kitaifa. Sh200, anasema ni pesa za usajili kufungua akaunti na Sh100 zinasimamia hisa moja, (bei ya hisa moja). Ni muhimu kutaja kuwa akiba unayoweka inaendelea kuzaa faida, kwa mujibu wa kanuni za chama cha ushirika au benki.

“Ili kupata mkopo unahitaji kuwa umeweka akiba na kununua hisa kwa muda wa miezi mitatu mfululizo. Kiwango cha mikopo hutathminiwa kwa hisa, ambapo unapaswa kuwa na hisa zenye thamani zaidi ya Sh5,000,” afafanua.

Kuwa mwanachama, unaweza kujiunga binafsi au kwa kundi la watu kadhaa.

Ili kupata mkopo au ufadhili wa biashara, mteja binafsi kwenye kundi anazidishiwa mara nne ya akiba yake, wanachama wenza wakiwa ndio dhamana yake.

Kimathi anasema kundi likitaka ufadhili, linazidishiwa mara tano ya akiba yao.

Mwenye akaunti binafsi, anasema anapewa mkopo wa hadi asilimia 70 ya akiba yake, kwa mujibu wa idadi ya hisa. Southern Star hutoza riba ya asilimia 12 kwa mwaka, katika mkopo.

Kutokana na kuimarika kwa teknolojia, benki na vyama vya ushirika vimeibuka na apu zinazotoa mikopo, kwa njia ya simu.

Southern Star, ina apu ya huduma hizo kwa wateja wake, maarufu kama ‘Jikwamue’.

Sekta ya SMEs inakadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini, na kulingana na Kimathi haja ipo kuipiga jeki kiufadhili, ambapo anashauri wafanyabiashara kujiunga na vyama vya ushirika ili kuweza kujiimarisha kibiashara na kimaendeleo.