• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kumakinikia kisa kikuu ndiyo njia pekee ya kuibuka na riwaya ya kufana

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kumakinikia kisa kikuu ndiyo njia pekee ya kuibuka na riwaya ya kufana

Na ENOCK NYARIKI

SIFA mojawapo ya riwaya ni kuwa na visa vingi ambavyo huungana ili kuunda hadithi kuu.

Ijapokuwa visa huwa vingi, kimoja kati ya hivyo huwa ndicho kisa kikuu ambacho kwacho visa vingine huhimiliwa. Kisa kikuu kinaweza kupewa fasili nyingi ambazo zinafungamana mno.

Nitazitaja fasili hizo kisha nizielezee kwa kina baadaye. Kwanza, ndilo wazo la msingi la mwandishi wa riwaya. Pili, ni kiunzi cha riwaya nzima. Tatu, ni kitovu ambacho kwacho mawazo huchotwa. Mwisho, ni dira inayomwelekeza mwandishi wa riwaya. Sasa tusidadavue hoja hizi moja baada ya nyingine.

Kisa kikuu huchukuliwa kama wazo la msingi la mwandishi wa riwaya kwa sababu huwa msukumo au kichocheo cha utunzi wa riwaya. Mtunzi wa kazi ya fasihi haanzi tu kutunga bila ya kuwa na jambo fulani ambalo angependa kutunga kwalo. Jambo hilo huwa na uhalisia fulani na yale yanayotendeka katika jamii ya mwandishi. Hata ndani ya uhalisiamazingaombwe au uhalisia ajabu hujificha uhalisia ambapo mwandishi hukusudia kuuwasilisha kwa hadhira yake. Alimradi wazo kuu hukumbatia ukweli kwamba utunzi wa kazi yoyote ya fasihi haukujikita katika ombwe tupu.

Kisa kikuu huwa kiunzi(skeleton or framework) cha hadithi kwa sababu ni kwacho ambapo visa vingine vimehimiliwa. Kiunzi kina umuhimu mkubwa katika kuupa mwili umbo lake. Kupitia kwacho hujitokeza fuvu, sehemu za kifua na fumbatio. Ifahamike kuwa kiunzi peke yake hakiwezi kukipa kitu utambulisho kamili. Kwa kuitumia analojia ya mwili wa binadamu , visa vingine kwenye riwaya huwa ni mfano wa nyama ambazo ‘huambikwa’ kwenye kiunzi ili kukipa utambulisho wake. Nimeitumia kauli utambulisho kwa maana ya sura kamili ya kitu.

Jambo jingine kuhusu kisa kikuu ambalo linajitokeza kwenye utangulizi ni kuwa ni kitovu ambacho kwacho mwandishi huchota mawazo yake.

Jambo muhimu kulifahamu hapa ni kuwa huenda kisa kikuu kikuu au wazo la msingi peke yake lisitoshe kuzaa maneno ambayo yanahitajiwa kuikamilisha riwaya. Kinachohitajika ili kulifikia lengo hili ni ubunifu.

Ubunifu huu unaweza kujitokeza kwa njia ya matumizi ya taharuki, taswira miongoni mwa mbinu nyingine za sanaa. Mbinu mojawapo ambayo imewazalia matunda mema waandishi wa riwaya ni taharuki. Waandishi hao huyakawisha matukio kwenye kisa kikuu kwa kuvihusisha visa vingine kwenye usimulizi.

Hata hivyo, visa hivi sharti vikizunguke kisa kikuu. Hii ndiyo sababu inayotufanya kusema kuwa kisa kikuu ni kitovu ambacho kwacho mwandishi huchota mawazo.

Hatimaye, kisa kikuu ni dira inayomwelekeza mwandishi wa riwaya. Dhima ya dira ni kumwelekeza mtu kufika hatima yake. Kwa hivyo, kisa kikuu katika riwaya hufanya kazi kama dira kwa njia zifauatazo.

Kwanza, huongoza mtiririko wa vitushi katika riwaya huku wakati huo ikimwacha msomaji na taharuki ya kutaka kujua jinsi hadithi itakavyokamilika. Pili, ni kupitia kwacho ambapo mgogoro unaoanzishwa na mwandishi hutatuliwa hatua kwa hatua.

Tatu, huyarejesha mawazo ya mwandishi katika kazi anayoitunga. Dira humkumbusha mwandishi kuwa wakati anapovihusisha visa vingine kuijenga kazi yake, akumbuke kwamba lipo wazo la msingi ambalo anapaswa kulirejelea muda baada ya mwingine.

Kutokioanisha kisa kikuu na visa vingine wakati wa kutunga riwaya husababisha mambo yafuatayo. Kwanza, riwaya huishia kuwa mfano wa diwani ya hadithi fupi ambamo hadithi hazina uhusiano wowote. Jambo hili hutokea hivyo ikiwa matukio kwenye kisa kikuu hayaingiliani na matukio kwenye visa vingine.

Neno matukio katika muktadha huu lina maana ya matendo wala si visa( ijapokuwa katika miktadha fulani matukio pia hurejelewa kama visa).

Pili, mgogoro hutatuliwa mapema mno na kuyafanya matukio mengine kugagamizwa na kusukumwa mbele. Jambo hili huifanya kazi kukosa mvuto. Kazi ambayo haina mvuto humchosha na kumchusha msomaji.

Wahusika hukosa mtagusano. Jambo muhimu katika utanzi wa riwaya ni kuwa, wahusika sharti wawe na uhusiano wa aina fulani. Neno uhusiano katika muktadha huu halina maana ya ukuruba wa kinasaba ingawa huo pia unaweza kuwa uhusiano mmojawapo.

Mwandishi sharti aoneshe uhusiano wa kimazingira miongoni mwa wahusika , jinsi wahusika wenyewe wanavyolandana au kuhitilafiana kimtazamo na jinsi wanavyoitatua migogoro inayowakumba miongoni mwa mambo mengine.

Kwa muhtasari, kabla ya kuanza kuandika riwaya, ni muhimu mwandishi kuwa na picha ya jumla ya matokeo ya kazi yake.

Aghalabu, hisia za msisimko huwateka waandishi wengi wanapoanza kutunga wakasahau kuwazia jinsi ya kukikamilisha kisa chenyewe. Kazi ambazo hazikuwaziwa vyema kabla ya kuanza kuandika mara nyingi huishia kuwa na miisho ya kupwaya.

You can share this post!

Bingwa Kipchoge kuongoza uwindaji dhahabu Olimpiki

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchangamano wa dhana ya itikadi...

adminleo