UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchangamano wa dhana ya itikadi katika miktadha ainati
Na ALEX NGURE
KAMUSI ya Kiswahili Sanifu inatoa kijelezi cha neno itikadi kama:
1) imani katika jambo la dini na jinsi ya mapokezi yake; wanavyofuata; mwafaka wa kufuata jambo fulani hasa dini; fikra za kuaminika; imani.
2) mawazo fulani ambayo ni misingi ya nadharia za mfumo wa kisiasa au za kiuchumi.
Kutokana na kijelezi hiki, tunaona maelezo yanayofungamanisha itikadi na uchambuzi wa mifumo iliyopo katika jamii kama vile siasa na uchumi. Kwa mfano, itikadi ya kijamaa; itikadi ya kibepari.
Itikadi ni dhana changamani na imezua mijadala mingi miongoni mwa wahakiki na wasomi mbalimbali. Licha ya kuzungumziwa kwa mapana, dhana hii inabaki telezi kuelezea.
Uchangamani wa dhana hii unatokana na ukweli kuwa ina sifa ya kufasiliwa kwa namna mbalimbali kama inavyoaridhiwa katika makala haya.Hebu tuchunguze maoni ya baadhi ya wasomi na wanafalsafa kuhusu dhana hii.
Wanafalsafa Engels na Marx wanasema kwamba ‘Itikadi ni mawazo yanayoakisi matakwa ya tabaka fulani katika kipindi fulani cha kihistoria,yanayowasilishwa kama ya jumla na ya milele’
Naye Prof I. Shivji anafafanua: ‘Kimsingi, ili kuelewa itikadi ni lazima tufahamu nadharia. Hivi vyote ni dira ya utambuzi wa binadamu.Lakini nadharia ni yale yaliyotokana na uchambuzi. Inajenga hoja ya kijumla. Katika Umaksisti kuna hatua.
Hatua ya utambuzi(perception)na ile ya kutafakari (conception). Hatua ya kutafakari ndiyo ya juu kabisa ya maarifa. Hatua ya utambuzi husawiri malezi aliyopata mtu katika jamii yake kwa kuwa kuna itikadi. Kutokana na mawazo ya Karl Marx, kazi ya itikadi ni kueleza na kuhalalisha mfumo uliopo. Marx aliita itikadi kama jambo lenye ukweli kidogo na uongo kidogo lakini si uongo mtupu. Kwa mfano, katika mfumo wa kibepari itikadi yake ni ya Kisheria, ilhali ukabaila una itikadi ya Kidini.
Ukabaila unajaribu kuwasadikisha watu kuwa mfalme ni mwakilishi wa Mungu na kwamba kila kitu kimepangwa na Mungu.
Hivyo, kuwa tajiri au maskini ni mpango wa Mungu. Kwa wazo hili, utabaini kuwa hakuna ukweli bali itikadi hufanya kazi ya kuhalalisha mfumo uliopo.
Ubepari ambao huongozwa na itikadi ya Kisheria nao huamini kuwa watu wote ni sawa.Katika hili kuna ukweli ndani yake.Maskini ana fursa ya kuwa tajiri na kwamba kama hawi tajiri ameamua mwenyewe, hakuna anayemzuia.
Hoja hii nafikiri inahalalisha tu mfumo wa Kibepari kwa kuwa si kweli kwamba watu wote wana fursa ya kuwa matajiri. Hapo ndipo unapouona uongo wa itikadi hiyo’ (mazungumzo 14-6-2010).
Katika Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake, uk 185, Prof K W Wamitila anasema:
‘Kimsingi, itikadi ni uwasilishaji wa pamoja wa mawazo, fikira na tajriba hasa ikiwa vitalinganuliwa na uhalisi wa kiyakinifu vinakotegemezwa. Terry Eagleton anapendekeza fasili mbalimbali za dhana hii:
Kwanza, kuelezea njia za kiyakinifu za kijumla za uzalishaji wa mawazo, imani, na tathmini katika maisha ya kijamii.Pili,mawazo na imani (za kweli au za uongo), ambazo huashiria mazingira na uzoefu wa maisha ya tabaka maalum la kijamii.
Tatu,ukuzaji na uhalalishaji wa matakwa na matamanio ya tabaka hilo la kijamii dhidi ya matamanio na matakwa kinzani.
Nne,kurejelea pale ambapo ukuzaji na uhalalishaj huo unaendelezwa na kundi la kijamii lenye nguvu.
Tano, mawazo na imani ambazo husaidia kuhalalisha matamanio na matakwa ya tabaka tawala na hasa kwa upotoshaji.
Sita, imani danganyifu na potoshi zinazozuka sio kutokana na matakwa ya tabaka tawala bali kutokana na muundo wa kiuzalishaji wa kijamii.
Loius Althusser anasema kuwa jamii za kitabaka zinadumishwa na muafaka unaozuliwa ki-itikadi kwa njia mbili kuu. Njia ya kwanza ni kwa matumizi ya Vyombo vya ki-Itikadi vya Dola (VID). Njia ya pili ni Vyombo Kandamizi vya Dola (VKD).
Kwa mujibu wa Althusser,jamii za kitabaka hudumishwa kwa makubaliano yanayopatikana ki-itikadi kupitia kwa Vyombo vya ki-Itikadi vya Dola.
Vyombo hivi ni kama asasi za kielimu, sheria, siasa, mashirika ya wafanya kazi na jamaa au familia. Vyombo hivi huchangizana na VKD.
Vyombo Kandamizi vya Dola ni asasi ambazo hutumia njia za kukandamiza ili kuwafanya watu; hususan wafanyakazi,kulitii tabaka tawala.Mifano mikuu hapa ni polisi, magereza na majeshi.
Wahakiki ambao wameathiriwa na Michel Foucault hawatilii maanani sana neno ‘itikadi’ bali ‘usemi au diskosi’.