Makala

TAHARIRI: Tukiwekeza katika michezo tutavuna

February 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

UWEKEZAJI wa kutosha ndiyo suluhisho pekee la kudidimia kwa viwango vya michezo mbalimbali nchini.

Mataifa mengi ya Afrika Mashariki yamekuwa yakilemewa katika michezo ya kimataifa hasa kutokana na ukweli kwamba hayajawekeza katika sekta hiyo vya kutosha.

Hii ndiyo maana utapata michezo mingi hasa soka inatawaliwa na mataifa ya Magharibi au Kaskazini mwa Afrika. Kenya, kwa mfano, haijawahi kupita hatua ya makundi katika fainali za Kombe la Afrika ambazo kwa sasa zinaitwa AFCON.

Wala si kukosa kupiga hatua katika fainali hizo tu, mataifa ya ukanda wa Afrika yanafuzu kwa fainali hizo kibahati nasibu tu.

Sharti hali hii ibadilike upesi maadamu mashabiki wa spoti katika ukanda huu nao wangependa kuona fahari pale vijana wao wanatamba katika mashindano mbalimbali duniani au barani.

Naam Kenya inafanya vyema katika riadha licha ya kwamba fani hiyo pia ina changamoto zake za kifedha. Yakini taifa hili linang’aa katika mchezo huo kutokana na bidii za wakimbiaji wenyewe tu. Yamkini pia ni kutokana na sababu za kimaumbile na motisha kutoka kwa watangulizi wao waliovuma enzi hizo.

Ithibati tosha kuwa iwapo tungependa michezo yetu iimarike sharti tuwekeze, ni mchezo wa raga wa wachezaji saba kila upande.

Unapotazama mwaka 2019 Kenya iliponea padogo kushushwa ngazi katika raga ya dunia (IRB Series).

Lakini mwaka huu tangu shirikisho la raga la Kenya (KRU) liajiri mjuzi wa raga kutoka New Zealand, Paul Feeney kama kocha na mkurugenzi wa kiufundi wa kikosi cha taifa (Shujaa), Kenya imeanza kutesa hata timu kubwa katika mashindano hayo msimu huu.

Wikendi iliyopita kwa mfano, Kenya ilifanikiwa kuangusha majabali wa mchezo huo barani na duniani, Afrika Kusini. Ili kudhihirisha maarifa yake, kuna dalili nyingi kuwa hivi karibuni Kenya itaanza kushtua hata timu mahiri zaidi kama vile New Zealand na Fiji.

Hali ilikuwa vivyo hivyo, shirikisho la mchezo huo lilipomwajiri mkufunzi stadi duniani, Mike Friday, ambaye baadaye alichukuliwa na Amerika.

Uwekezaji mzuri katika mabenchi ya kiufundi ya vikosi vya taifa pamoja na katika michezo ya vijana, bila shaka utazaa matunda, yaani unavuna ulikopanda.

Serikali, kwa ushirikiano na mashirikisho ya michezo mbalimbali, inafaa iongeze bajeti yake ya michezo maadamu mbali na kuchangia kuinua viwango vya spoti nchini, fani mbalimbali za michezo zitatoa nafasi murwa za ajira kwa vijana wenye talanta.

Miundomsingi ya kisasa itatekeleza dhima kubwa katika kuwapa vijana jukwaa la kutamba kispoti.