Habari

Ruto asisitiza maswala ya BBI yawe ya kila Mkenya

February 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KILA Mkenya ana haki ya kutoa maoni yake kuhusu maswala ya ripoti ya mchakato wa maridhiano (BBI) bila kubaguliwa.

Naibu Rais Dkt William Ruto, alisema mchakato wa kujadiliana maswala ya BBI lisiwe ya watu wa ngazi ya juu, pekee lakini kila mmoja apatiwe nafasi yake ili aweze kusikizwa.

“Tusijadili maswala ya BBI ya kugawana vyeo lakini liwe ni maswala ya kuhudumia mwananchi wa chini ili kila mmoja ajisikie kuwa anatambulika,” alisema Dkt Ruto.

Alisema iwapo Wakenya watajadiliana kwa njia ya uwazi na haki bila kuingiza chuki, bila shaka “tutafika mbali.”

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa mjini Thika alipozuru shule mbili za wasichana wakati wa kutoa zawadi kwa waliofanya vyema kwenye mtihani wa KCSE mwaka 2019.

Naibu Rais alizuru shule ya wasichana ya Chania na ile ya Thika Girls Karibaribi.

Alisema serikali imetenga takribani Sh8 bilioni za kujenga vyuo vya kiufundi 30 nchini ili vijana waweze kupata ajira.

Alisema vijana wanastahili kupata nafasi ya ajira iwapo watakamilisha mafunzo yao katika vyuo hivyo.

“Kila mtoto hapa nchini anastahili kupewa heshima yake kwa sababu wana talanta tofauti na kwa hivyo serikali itafanya juhudi kuona kila mmoja anasoma hadi kiwango atakachofikia,” alisema Naibu Rais.

Wakati wa ziara hiyo ya Ruto aliahidi kununua mabasi mawili ya shule hizo mbili na kukamilisha baadhi ya miradi iliyokwama, huku pia akiamuru maji ya kisima yachimbwe katika shule ya Thika Girls’ Kribaribi.

Kuhusu elimu, alisema tayari asilimia 93 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la nane wamejiunga na kidato cha kwanza.

“Serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba hakuna mwanafunzi yeyote anayebaki nyumbani bila kufanya chochote,” alisema naibu wa Rais.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema ni vyema kila Mkenya kuunga mkono serikali ili iweze kuafikia ajenda zake nne za ujenzi wa viwanda, Afya, Uhifadhi wa chakula na ujenzi wa majumba.

“Iwapo tutazingatia hayo kwa sasa bila shaka nchi yetu itakuwa imepiga hatua kubwa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema viongozi wanastahili kujiepusha na siasa na kuzingatia maendeleo ili mwananchi wa chini aweze kunufaika.

Mbunge wa Gatundu Kusini alisema wananchi wanastahili kuhudumiwa badala ya kuwaimbia maswala ya siasa kwani hakuna atakayenufaika na malumbano ya kila mara.

“Mwananchi wa kawaida anataka kuona kazi zikibuniwa, bei ya kahawa na chai ikirekebishwa, maziwa na miwa ikikadiriwa bei ya kuwafaidi,” alisema Bw Kuria.

Leo Jumamosi Ruto anaongoza viongozi wa North Rift katika hafla kubwa ya Askofu wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki Eldoret Dominic Kimengich anayechukua mikoba rasmi.

Hafla yenyewe inaandaliwa katika uwanja wa Seminari ya Mother of Apostles, Eldoret.