• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
MWANAMUME KAMILI: Mume wa leo mwingi wa kero, hajui kufurahia alichojaliwa

MWANAMUME KAMILI: Mume wa leo mwingi wa kero, hajui kufurahia alichojaliwa

Na DKT CHARLES OBENE

WAJA wenzangu makinikeni maishani maana ujaliwapo punda, huna budi kumkama!

Kweli maisha sanaa! Waliojaaliwa mili wanazidi tiririsha jasho jingi katika jitihada za kupunguza kilo na minofu vilevile. Akina sisi tunaotafuta kuunga, ndio kwanza tunakesha jikoni, kila kitu kinywani! Nini hasa anachotaka mwanadamu wa leo?

Nawaona kila siku wanaume wanavyogugumiza mate wanapomwona mke aliyekula akashiba vyake. Nawaona vilevile wanawake wanatekenyeka wakiona misuli ting’inya. Je, kina sisi wembamba kama mwiko wa pilau, nani atakayetuchumbia?

Na ifahamike kwamba uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti. Ole nyinyi mnaotafuta vitu. Zaidi na utu, vinginevyo si vya tija maana mwishowe huwa vya kutu. Mwajisumbua bure kutafuta mili ya kuzinga! Umbo si kitu maadamu mwana wa mtu ana utu? Umbo umejaa hadaa na mja hana haja kuundondoshea mate! Kaka zangu mtachoka kutafuta vya duniani!

Ama kweli wanaume kwa wanawake wa leo wanaishi kuigiza na sanaa hii iitwayo maisha inazidi kutuzolea dhiki. Maisha na mahusiano baina ya waja wa leo ni sanaa inayochekesha hali kadhalika kuchusha. Bila shaka vitimbi hivi vinazidi kudunisha mno hadhi ya watu wazima – watu wanaotumainiwa kama viongozi wa leo na kesho vilevile.

Wiki jana nilikuwa mahakamani kusikiliza kesi ya wangwana wawili walioomba mahakama kuwaridhia talaka. Kwa mujibu wa mke, hakutaka tena kuishi na mume asiyemwezesha kuishi kwa amani. Yaani amekwisha kuwa kero zaidi ya kero. Hana hanani. Mke yule alidokeza kwamba mumewe amekwisha hamia kijiji jirani wala hana haja tena na mkewe wala watoto.

Kwa mujibu wa mume, alikwisha choka kudaiwa kila kitu na mkewe. Mwenyewe alisema kwamba hana tena mwili wa kutandikwa na mkewe ndio maana akamua kujinusuru kwa hiari. Dume lilichekesha mahakama kwamba mkewe alikwisha “kumpiku kwa uzani licha ya kwamba ndiye mtafutaji nyumbani”. Alipoulizwa mbona alishindwa kutononoka mwili, alijibu kwamba “analishwa mate tu!” Kisa hiki cha watu wazima kuchoka kuishi pamoja ndio mtindo wa mapenzi ya kina yakhe wa leo.

Pamoja na hawa wanaochoka kwenye ndoa, wapo vilevile wanaume wanaojikakamua kutafuta wenzao kama dhahabu na punde ndege anapoingia kiotani, wanakuwa si watu tena. Wapo wanawake wanaonyenyekea na kutii wanaume kama njia tu ya kumshawishi mtu kukubali usuhuba. Punde wanapotia nyayo nyumbani, wanageuka kuwa chatu kuwang’ata na kuwatemea mate ya kinyaa wanaume na majirani

Tatizo kubwa ni kwamba wanadamu wa leo wako mbioni kutafuta wasichokijua. Hata wanapopata hawajui wafanye nini nacho. Kisa cha wawili wanaotafuta talaka kwa kushindwa kutatua tofauti zao ni dhiki kubwa.

Baadhi ya hizi ndoa za watu kuchoka njiani ndizo hizo zilizochipuka kwa mtindo wa kuzinguana pasipo msingi wala heshima. Jamani kuzinga na kuzinguana tuwaachie vijana wanaoota ndoto asubuhi! Sifa za mke chache sana. Ajue kupika na kuandika mezani. La muhimu ajue kumpikia na kumpakulia mumewe. Ole nyinyi mnaosaza kwa misingi ya miguu au hata kwa kukadiria ukubwa wa nyonga!

Nakubaliana na msemo kwamba “mwanamume wa leo mwingi wa kero, hajui kufurahia alichojaaliwa!” Kweli. Ndio maana haishi mbwembwe kutafuta asivyojua. Akimpata mke mdogo mwembamba kimbaumbau mwiko wa pilau; tetesi ni zilezile. Mara hana minofu! Mwana hashikiki hana ashiki! Akijaaliwa tipwa la jike, vijembe vilevile. Hizi tabia za kitoto sizo za mwanamume kamili.

Tatizo zaidi ni kwamba kila uchao tunakumbana na wanaume wanaofanya maamuzi bila tathmini. Wanaume wanayumba kushoto – kulia! Kucha kutwa wanang’ang’ania mapenzi; vidosho kuwasaka ilhali wenyewe bado kujiweka tayari kiakili na kirasilmali! Kila apandaye sharti kujenga ghala!

Maisha ni jaala na mtu hupata ajaaliwacho sio atakacho. Hivyo ina maana kwamba mwanamume anaweza kumpata na kumwoa mke ambaye katu hakudhani ndiye. Mwanamke vilevile anaweza kuolewa na kiatu cha mtu! Talaka sio suluhu kwa matatizo ya ndoa. Ujaaliwapo punda huna budi kumkama.

[email protected]

You can share this post!

Moto waharibu vibanda kadhaa sokoni Gikomba

BBI: Jinsi mambo yalivyokuwa Kitui

adminleo