KINAYA: Hapa kwetu, BBI na kukabili upinzani ni muhimu zaidi kuliko janga la nzige
Na DOUGLAS MUTUA
MWAMBIE ‘Ouru’ atafute dawa ya nzige haraka, na asisahau pia kutafuta dawa ya Mwangi Kiunjuri.
Bila shaka unajua tunahitaji kuwaua wadudu hao waharibifu ambao wanatafuna mimea yetu kishenzi na kutishia kutuletea njaa ya mwaka.
Ukiangalia nzige wanavyofanya uharibifu Mashariki na Kaskazini Mashariki mwa nchi, unajiuliza kati ya hatari hiyo na uhamasisho wa Ripoti ya Maridhiano (BBI) ni gani muhimu.
Mambo yakienda yanavyoonekana, nadhani tutazunguka kote nchini kuhubiri injili ya BBI, tukirejea tupate nzige wametafuna kila mmea, tulalie mate.
Kumbuka Katiba si chakula, ni karatasi kama nyingine tu, hivyo basi huwezi kuitafuna unaitia tumboni.
Na tayari tuna Katiba iliyopitishwa 2010, tena iliyotumia mabilioni ya pesa. Sikatai tuibadilisha, lakini sijui italeta sufuria ngapi za ugali mezani fukara ale na kushiba.
Rafiki yangu Jackson Mandago, ambaye ni Gavana wa Uasin-Gishu, amesema peupe kwamba BBI ni njama ya wanasiasa wasiotaka kustaafu mapema.
Ameuliza yeye mwenyewe atastaafu akiwa na miaka 46 aende wapi! Ni kwa sababu hiyo, alisema, ambapo BBI inaungwa mkono na magavana wengi wanaostaafu.
Kumbuka kuna pendekezo kwamba, mbali na serikali za kaunti, ziundwe nyingine 12 za kimaeneo, yaani kama mikoa ya zamani.
Huko, kwa mujibu wa ‘Ouru’, ‘Baba’ na washirika wao, ndiko kupunguza mzigo. Sijui vipi, hasa kwa maana nina uwezo wa kuunga moja na moja nikapata mbili, lakini nitasubiri tu.
Nitasema na kurudia mara kadhaa kwamba nzige ni janga la kitaifa ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa dharura.
Lakini ninajua hakuna atakayenisikiza kwa sababu kawaida ya serikali za Kenya tangu tuwe huru, tatizo si tatizo ikiwa halijafika viungani Nairobi, Kati na Rift Valley.
Labda shughuli za kukabiliana na nzige zitaanza pale kahawa, majani-chai na viazi vya mtu vitakapotafunwa sawasawa.
Sawa na ‘Ouru’ asivyoonekana kufahamu nzige wanavyotutafunia mimea, nadhani hajui anavyotafunwa na Kiunjuri; waziri aliyeshindwa kukabiliana na nzige akapigwa kalamu.
Na ndiyo maana nikapendekeza ‘Ouru’ amtafutie dawa Kiunjuri upesi. Si kwamba bwana huyo aliyetimuliwa kutoka baraza la mawaziri hivi majuzi ana minyoo tumboni, la hasha!
Wala haumwi, anauma. Hata nzige hatusemi watafutiwe dawa ya kuwaponya, ni ya kuwaangamiza. Sikiza: sijapendekeza Kiunjuri aangamizwe kisiasa, nawaza tu.
Anayohitaji ‘Ouru’ ni dawa ya kumzima kisiasa kabla hajawa zimwi la kumla mzimamzima akistaafu akose pa kwenda.
Hata wewe hungetaka kurejea kwenu mashambani, kisha wenyeji ulioacha huko wakila vumbi wakuulize umerejea kufyata nini!
Kiunjuri si kama wanasiasa wengine wa mlimani, anakoita kwake ‘Ouru’, ambao wakimtusi anakwenda mashinani kuwachochea wakazi dhidi ya ‘huyu mtu mliyechagua’.
Kiunjuri si mbunge wala waziri, hakuna eneo moja analowakilisha, tena anampiku ‘Ouru’ kwa ufasaha wa kukitema Kikikuyu kilichojaa mafumbo kama cha wazee wa kale!
Nimemwona Kiunjuri juzi akiwashawishi wakazi wa mlimani kwa weledi mkubwa walipe deni la Sugoi, wasiwe wezi wa fadhila kama walivyozoeleka tangu zamani. Alishangiliwa sana!
Mimi na wewe tusononeka kuhusu nzige, ‘Baba’ kuhusu BBI, naye ‘Ouru’ asononeshwe na nzige-mtu. Inaonekana kila mtu ana kazi, tusilaze damu.