MWANASIASA NGANGARI: Amukowa Anangwe, waziri msomi ambaye aliboresha sekta ya afya
Na KEYB
FREDERICK Dickson Amukowa Anangwe alijiunga na siasa wakati kampeni za kushinikiza siasa za vyama vingi zilikuwa zimeshika kasi miaka ya themanini na mapema miaka ya tisini.
Ingawa hakufaulu katika azma yake alipogombea kiti cha ubunge mwaka wa 1992, maisha yake ya kisiasa yalibadilika 1997 aliposhinda kiti cha eneobunge la Butere na akateuliwa Waziri wa Ustawi wa vyama vya Ushirika.
Anangwe alifanya kazi kama mkuu wa tarafa ya Ngong, (DO) karibu na Nairobi, miaka ya mwanzo ya utawala wa Moi. Akiwa DO, alipata ufadhili wa masomo kwenda kusomea digrii ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa umma nchini Uholanzi. Alitumia fursa hiyo kujifunza Kifaransa.
Aliporejea Kenya alifunza katika Taasisi ya Masuala ya Usimamizi ya Kenya inayofahamika kwa wakati huu Kenya School of Government.
UZAMIFU
Alipata ufadhili mwingine wa masomo katika chuo kikuu cha Manchester nchini Uingereza na akapata digrii ya uzamifu.
Anangwe alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi kufunza sayansi ya kisiasa katika Idara ya Serikali. Hapo ndipo alianza kuvutiwa na siasa. Nafasi ya kushiriki siasa kikamilifu ilimjia Moi alipokabiliwa na hatari ya kupoteza mamlaka 1992 wakati upepo wa mabadiliko ulipovuma kote nchini kushinikiza akubali demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.
Hii ilikuwa ni kampeni ya kubadilisha katiba kuondoa kifungu cha 2A katika katiba ya zamani kilichoanzishwa 1982, kufanya Kanu kuwa chama cha pekee cha kisiasa nchini Kenya.
Akiwa mwanafunzi wa Sayansi ya siasa, na akiwa amehudumu kama DO na kufurahia nguvu zinazoambatana na cheo hicho, Anangwe alifahamu maana ya kuwa na mamlaka.
Wakati huo, vuguvugu la Youth for KANU ’92 (YK ’92), lililoongozwa na Cyrus Jirongo, lilikuwa limechipuka na nguvu zaidi kumfanyia kampeni Moi ili ashinde uchaguzi mkuu uliokuwa umekaribia.
Anangwe alijiunga na kundi hilo akiwa na wahadhiri wengine wakiwemo Eric Aseka, Chris Wanjala na Henry Mwanzi na wakaanza kusajili vijana kumpigia debe Moi.
Wakati huo, jarida la kila wiki la Weekly Review lililochapishwa na Hilary Ng’weno, ambaye alikuwa mhariri mkuu wa kwanza Mwafrika wa gazeti la Daily Nation, liliandika habari kuu zilizosema: “100 Lecturers Say no to Multi-partism( Wahadhiri 100 wakataa vyama vingi vya kisiasa).”
Hata hivyo, jarida hilo halikutaja majina ya wahadhiri hao. Habari hizo zilikosolewa kwa madai hayo kwa sababu idadi ya wahadhiri wakati huo ilikuwa ni zaidi ya 100; na baadhi yao walikuwa wakiunga upinzani.
Kuchapishwa kwa habari hizo kulisadifiana na hatua ya Moi ya kuteua kamati chini ya Makamu Rais George Saitoti kukusanya maoni kutoka kwa umma kubaini iwapo Kenya ilipaswa kukumbatia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.
Moja kati ya mapendekezo ya ripoti ya kamati hiyo ambayo ilichangiwa sana na wahadhiri hao na YK ’92, ilikuwa ni kwamba Wakenya hawakutaka mfumo wa vyama vingi vya kisiasa lakini walitaka demokrasia kupanuliwa ndani ya KANU.
Hata hivyo, ukweli ulikuwa ni kwamba kokote ambako kamati ilienda, Wakenya walikuwa wakiungana katika wito wa kutaka vyama vingi vya kisiasa.
Anangwe alikuwa mwanachama wa jopo lililobuniwa na Aseka, kupitia waziri William Ntimama, kukutana na Moi kumfahamisha habari walizokuwa wamepata mashinani.
Walimshawishi Rais Moi kwamba wito wa siasa za vyama vingi ulikuwa ya kiusomi tu na ulipaswa kuzimwa kupitia wasomi.
Licha ya kumpigia kampeni Moi achaguliwe tena, Anangwe aliendela kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi hadi uchaguzi mkuu uliofuata.
Mnamo 1997 aligombea kiti cha eneobunge la Butere kilichokuwa kimeshikiliwa na Martin Shikuku. Alishirikiana na vigogo wa KANU Saitoti na Joseph Kamotho.
Anangwe aliteuliwa waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika. Alikuwa ameonja uongozi akiwa nahodha wa shule ya Shimo la Tewa High School iliyoko Mombasa.
Hata hivyo, anakumbukwa kwa jukumu alilotekeleza akiwa waziri wa huduma za matibabu. Anangwe anasifiwa kwa kubuni jopokazi kuchunguza mbinu za kupunguza bei za dawa nchini, hatua ambayo ilinuiwa kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu nchini.
Wanachama wa Jopokazi hilo walikuwa wawakilishi wa wizara ya afya, Shirika la Afya Ulimwenguni, UNAIDS, Chama cha Matabibu nchini, Chama cha wanafamasia cha Kenya, chama cha watengenezaji wa dawa cha Kenya, Medecins Sans Frontieres, Wizara ya Fedha na kitivo vya dawa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Mwenyekiti wa Jopokazi hilo alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Richard Muga na mwanafamasia mkuu Kipkerich Koskei, alikuwa katibu wake.
Jukumu la jopo lilikuwa ni kuchunguza kanuni za kuthibiti wadau katika sekta hiyo. Waziri alishikilia kuwa asilimia 50 ya Wakenya hawakuwa wakipata dawa za kimsingi za kuokoa maisha jambo ambalo alisema halikubaliki kimaadili na kisiasa.
Alisema Wakenya walikuwa wakifariki kila siku kutokana na maradhi yanayoweza kutibiwa. Gharama ya juu ya kutengeneza dawa au uagizaji kutoka nje na kodi ni miongoni mwa mambo yaliyohusishwa na bei ya juu ya dawa.
Anangwe alihisi kwamba bei ya dawa nchini ilikuwa ya juu kuliko nchi nyingine. Alilinganisha bei ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (wakati huo hazikuwa zikitolewa bila malipo) ambazo Wakenya hawangemudu na bei nchini Malaysia.
Alieleza wanahabari kwamba bei ya dawa kama vile fluconazole, ya kutibu meningitis kwa wanaougua Ukimwi ilikuwa nafuu Thailand kuliko Kenya.
Alisema kwamba Kenya ilihitaji kuchukua hatua za dharura kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa raia wake.
Kufuatia juhudi zake, kampuni za kutengeneza na kuuza dawa zilipunguza bei ya dawa za kukabiliana na makali ya Ukimwi.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Kenya ilitaka bei ya dawa hizi ipunguzwe kwa asilimia 85.
Hata hivyo, Anangwe alisema: “Hata kama tunapendekeza bei ipunguzwe, bei ya dawa itakuwa ya juu.”
Kwa mfano, alieleza, gharama ya kukabiliana na Ukimwi kwa mtu mmoja baada ya bei kupunguzwa ingekuwa zaidi ya Sh6,000 kwa mwezi wakati huo ikiwa ni dola 720 za Amerika.
GHARAMA YA JUU
Alisema gharama hii ilikuwa ya juu mno kwa Wakenya wengi. Bei ya dawa hizo ilibaki kuwa ya juu hadi miaka ya 2000s wakati serikali ilianza kuwapa wagonjwa dawa za kukabiliana na makali ya Ukimwi bila malipo.
Anangwe alifahamisha wanahabari kwamba bei iliyopunguzwa ya kampuni kubwa za dawa ilikuwa ikikinzana pakubwa na ya kampuni za dawa nchini India na akatoa mfano wa kampuni ya Cipla Corporation.
Baadaye, wizara ilikabiliwa na mzozo kuhusu zabuni ya kununulia hospitali ambulensi chini ya Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya.
Hii inaweza kuwa ndiyo ilisababisha Anangwe na maafisa wengine kuondoka wizara ya Huduma za Matibabu. Muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002, aliteuliwa waziri msaidizi katika Ofisi ya Rais.