Waititu ni kionjo tu, Rais aonya magavana
GEORGE MUNENE na WANDERI KAMAU
RAIS Uhuru Kenyatta amewaonya magavana wote wanaoshiriki katika ufisadi kwamba, watang’olewa mamlakani.
Onyo hilo lilijiri Jumamosi; siku chache baada ya Bunge la Seneti kuidhinisha hoja ya kumng’oa mamlakani aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinard Waititu.
Akihutubu katika uwanja wa michezo wa Wang’uru, Kaunti ya Kirinyaga, Rais aliwaambia magavana wengine wanaojihusisha na ufisadi kuwa madiwani watawatimua mamlakani.
“Madiwani wanatazama na hawatasita kuwaondoa magavana wasiozingatia kanuni za utendakazi. Yeyote ambaye amepora fedha zilizopangiwa kusaidia umma hatanusurika,” alisema.
Aliongeza kuwa magavana waliotuhumiwa kushiriki kwenye ufisadi wamekuwa wakiwaelekezea watu wengine lawama, badala ya kuubeba msalaba wao na kukariri kuwa serikali haitawalinda.
“Magavana ambao wamepora fedha za umma wataubeba msalaba wao wenyewe. Madiwani wanapaswa kuendelea kuwachukulia hatua bila kuogopa,” alisema.
Alishangaa jinsi Wakenya watakavyofaidika kwa maendeleo, ikiwa ufisadi utaendelea nchini.
“Lazima tushinde vita hivi dhidi ya ufisadi,” alisema.
Bw Waititu aling’olewa mamlakani na Bunge la Kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 19, 2019, kwa tuhuma za ufisadi, ukiukaji wa Katiba na matumizi mabaya ya mamlaka.
Bw Waititu anakisiwa kuipora kaunti hiyo Sh588 milioni anazodaiwa kulipa kampuni ghushi kwenye utoaji wa kandarasi katika kaunti hiyo.
Baadhi ya kampuni zilizopokea fedha hizo zinadaiwa kumilikiwa na jamaa zake, akiwemo mke na mwanawe. Licha ya tuhuma hizo, amekuwa akijitetea akisema kuwa, njama hizo zimekuwa zikiendeshwa na mahasimu wake kisiasa.
Kufuatia hatua ya Seneti, aliyekuwa naibu wake, Dkt James Nyoro aliapishwa rasmi mnamo Ijumaa kama gavana mpya wa Kiambu.
Kando naye, magavana Mike Sonko (Nairobi) na Moses Lenolkulal (Samburu) wanakabiliwa na mashtaka na mahakama imewazuia kufika katika afisi zao.
Bw Sonko anakabiliwa na tuhuma za kupora zaidi ya Sh357 milioni kupitia utoaji kandarasi kwa kampuni hewa.
Naye Bw Lenolkulal anadaiwa kupora zaidi ya Sh270 milioni.
Wakati huo huo, Rais aliushambulia vikali mrengo wa siasa wa ‘Tanga Tanga’, unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, akisema kuwa unawachochea Wakenya kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI).
Aliwaomba Wakenya kupuuzilia mbali kauli za wanasiasa hao na kuunga mkono mpango huo.
“BBI italeta amani, hivyo, kila Mkenya anapaswa kuiunga mkono,” alisema.
Wabunge wa eneo hilo Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati), Kabinga wa Thayu (Mwea) na Gichimu Githinji (Gichugu) ambao wanaegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ hawakuruhusiwa kuhutubu.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Gavana Anne Waiguru, Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirici na Seneta Charles Kibiru.
Rais Kenyatta amekuwa akifanya msururu za ziara katika kaunti mbalimbali eneo la Mlima Kenya, katika hatua inayoonekana kama mkakati wa kuupigia debe mpango wa BBI.