• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
JAMVI: Jinsi tajiri Muthoka alivyounganisha vigogo wa siasa Ukambani kuhusu BBI

JAMVI: Jinsi tajiri Muthoka alivyounganisha vigogo wa siasa Ukambani kuhusu BBI

BENSON MATHEKA Na KITAVI MUTUA

Huenda siasa za eneo la Ukambani zikachukua mwelekeo mpya iwapo juhudi za kuunganisha viongozi zinazoendelezwa na mfanyabiashara Peter Muthoka zitafua dafu.

Mfanyabiashara huyo alifaulu kuwaleta pamoja vigogo wa kisiasa wa eneo hilo ambao walikuwa wamepanga mikutano tofauti ya kuvumisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na wafuasi wake walikuwa wamepanga mkutano wa BBI mjini Wote, Kaunti ya Makueni nao magavana wa kaunti tatu za eneo hilo Charity Ngilu ( Kitui) Alfred Mutua ( Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni) walikuwa wamepanga mkutano mjini Kitui, jambo ambalo lilionyesha mgawanyiko mkubwa wa viongozi kuhusu suala hilo.

Bi Ngilu aliteuliwa na Rais Kenyatta kuongoza shughuli za kuvumisha BBI eneo la Ukambani, na akiwa na magavana wenzake walihudhuria mikutano ya awali katika Kaunti ya Kisii, Kakamega na Mombasa.

Bw Musyoka alihudhuria mkutano wa Mombasa ambako alitofautiana na magavana hao kuhusu maandalizi ya mkutano wa BBI eneo la Ukambani.

Hii ilimfanya Bw Muthoka ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta kuingilia kati kwa kubuni mikakati ya kuwapatanisha viongozi hao.

Dkt Mutua alikuwa wa kwanza kubadilisha nia na kujitenga na magavana wenzake akiwalaumu kwa kuzua mgawanyiko kuhusu BBI ilhali ni mchakato wa kuunganisha Wakenya.

Kulingana na gavana huyo, BBI inapaswa kuleta viongozi pamoja na si kuitumia kuonyesha ubabe wa kisiasa.

Ilibainika kuwa hatua ya gavana huyo kubadilisha nia ilitokana na ushawishi wa Bw Muthoka ambaye pia aliwasiliana na viongozi wengine wa kisiasa eneo la Ukambani kwa lengo la kuwataka wazike tofauti zao na kuungana.

Bw Muthoka aliwaleta pamoja viongozi hao na washirika wao kwenye mkutano uliofanyika Jumatano katika eneo la Stoni Athi Resort, Kaunti ya Machakos na wakakubaliana kuandaa mikutano ya BBI pamoja.

Mikakati ya bwanyenye huyo ambaye anasema hana nia ya kugombea kiti chochote ilihusisha maspika wa mabunge ya kaunti tatu za Ukambani na viongozi wa wengi na wachache ambapo walijadili jinsi jamii hiyo inavyoweza kuungana.

Inasemekana kuwa aliwapigia simu mahasimu wa kisiasa -Musyoka na magavana hao watatu- na akawashawishi waache misimamo yao mikali kwa manufaa ya jamii.

Ni baada ya kuzungumza nao ambapo Dkt Mutua, alitumia tajiriba yake kama mtaalamu wa mawasiliano kutoa taarifa akijitenga na magavana wenzake waliokuwa wameapa kuendelea na mikutano yao ya BBI bila kumhusisha Bw Musyoka na washirika wake.

Kwa maagizo ya Bw Muthoka, viongozi hao walipigiana simu kujadili jinsi ya kuunganisha jamii ya Wakamba.

Katika mkutano uliofanyika Stoni Athi, Bw Musyoka na Bi Ngilu walikiri kuwa waliwasiliana kufuatia agizo la bwanyenye huyo na wakaamua kulegeza misimamo yao kuhusu mikutano ya BBI.

Kulingana na Bw Musyoka, alipokea simu kutoka kwa Gavana Mutua aliye nje ya nchi na wakakubaliana kuwa wanafaa kuunganisha jamii. Mikakati yake ya kuhusisha maspika na viongozi wa mabunge ya kaunti ilizaa matunda madiwani na wabunge walipohudhuria mkutano wa Stoni Athi katika hatua ambayo wadadisi wanasema ikidumishwa, inaweza kubadilisha siasa za Ukambani.

“Juhudi za Bw Muthoka ni nzuri. Ni mwelekeo unaofaa na ukidumishwa, eneo na jamii nzima inaweza kuzungumza kwa sauti moja. Shida ni ukosefu wa nia njema miongoni mwa wanasiasa na tabia yao ya kigeugeu kila mmoja akitaka kutimiza malengo ya kibinafsi,” asema mdadisi wa siasa eneo la Ukambani John Kisilu.

Katika mkutano wa Stoni Athi ambao inasemekana Bw Muthoka aliufadhili, viongozi hao walikubaliana kuzika tofauti zao na kuandaa mikutano ya BBI pamoja kuanzia na uliofanyika Kitui jana.

Wadadisi wanasema ni mkutano uliopangwa mjini Wote Februari 7 ambao utaamua iwapo umoja wa viongozi hao utadumu.

“Kwa maoni yangu, viongozi hao hawana nia ya dhati ya kuungana. Ni hali ilivyo nchini kwa wakati huu hasa kuhusu BBI inayowafanya kumsikiliza Muthoka na kukubali kuandaa mikutano ya pamoja. Wanajua kwamba anawakilisha maslahi ya Rais na hawataki kumvunja moyo,” asema Kisilu.

Katika mkutano huo, Bw Muthoka aliwakemea viongozi wa kisiasa kwa kupigania ubabe wa kisiasa badala ya kuungana kupigania miradi ya maendeleo ya kunufaisha wakazi.

Bila kulaumu mtu binafsi, mfanyabiashara huyo aliwahimiza viongozi hao kufikiria jinsi ya kuimarisha maisha ya wakazi badala ya kupigania ubabe wa kisiasa.

Alitaja miradi mitatu mikubwa ambayo imekwama eneo la Ukambani huku viongozi hao wakipigania maslahi yao ya kibinafsi.

Miradi hiyo ni Bwawa la Grand Falls Dam, Kaunti ya Kitui linalonuiwa kujengwa kwa gharama ya Sh200 bilioni, mradi wa makaa ya mawe pia Kaunti ya Kitui na jiji la kiteknolojia la Konza.

Kulingana na wadadisi, hatua ya Bw Muthoka inafaa kuwa mwamko mpya kwa viongozi wa Ukambani.

Magavana Ngilu, Mutua na Kibwana wamekuwa wakimpiga vita Bw Musyoka wakimlaumu kwa kupuuza jamii ya Wakamba licha ya kuhudumu serikalini kwa miaka mingi.

Bw Musyoka na Dkt Mutua wametangaza nia ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kila mmoja amekuwa akitaka kutambuliwa kama msemaji wa jamii.

You can share this post!

JAMVI: Kauli za Rais zaonyesha huenda asing’atuke...

JAMVI: Ukaidi wa Ruto kwa Rais wafika kilele, nani...

adminleo