Polisi akamatwa kwa kutia chang'aa maji
NA MWANDISHI WETU
AFISA wa Polisi amekamatwa akidaiwa kuiba chang’aa iliyonaswa kwenye msako, kisha kujaza maji kwenye vibuyu vilivyokuwa na pombe hiyo haramu.
Vitalis Otieno alikamatwa baada ya pombe iliyonaswa katika msako Jumamosi kutoweka katika hali ya kutatanisha katika kituo cha polisi cha Sindo, Kaunti ya Homabay, .
Msako huo ulinasa lita 140 za pombe aina ya chang’aa, lakini maafisa wa serikali walioendesha msako huo walipigwa na butwaa walipopata ‘imegeuka’ kuwa maji.
Kamishna wa eneo la Nyanza, James Kianda jana alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu jinsi lita 140 za pombe haramu zilivyotoweka na vibuyu kujazwa maji.
Katika Kaunti ya Bomet, washukiwa watatu wamekamatwa kwa madai ya kushambulia machifu.
Kamishna wa Bomet, Geoffrey Omoding alisema washukiwa hao walikamatwa baada ya wanakijiji kupasha habari polisi.
Walikuwa miongoni mwa watu walioshambulia machifu sita katika eneo la Konoin wakisaka pombe haramu miezi minne iliyopita.