Sitazuiwa na yeyote kukagua miradi, tuheshimiane – Ruto
RUTH MBULA, ONYANGO K’ONYANGO na GERALD BWISA
NAIBU Rais William Ruto amesisitiza ataendelea kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo.
Alisema hayo siku mbili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuelezea masikitiko kwamba viongozi aliowapa jukumu la kuzindua miradi ya maendeleo wanaitumia kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Rais Kenyatta Ijumaa alisema kuwa sasa ataanza kuzuru na kukagua miradi ya maendeleo mwenyewe.
Lakini Jumatatu, Dkt Ruto aliyekuwa akizungumza katika Kaunti ya Kisii alisema: “Nitaendelea kuzindua miradi ya maji, barabara, elimu na umeme. Nitaendelea kuzuru eneo hili kwa sababu mimi ni naibu wa rais na ninalipwa mshahara na Wakenya.”
“Hakuna mtu yeyote hapa Kisii ambaye amelalamika kwamba natekeleza majukumu yake. Kila mtu aachwe atekeleze majukumu yake na tuheshimiane,” akasema Dkt Ruto.
Naibu wa Rais alikuwa akizungumza katika eneo la Itierio, Kaunti ya Kisii wakati wa hafla ya kumtawaza Askofu Joseph Omwoyo wa Kanisa la Kiinjili la Lutheran.
Dkt Ruto amekuwa akisisitiza hali ni shwari katika ushirikiano wake na Rais Kenyatta licha ya kuwa ishara ni tofauti.
Wakati huo huo, wanasiasa wa kundi la Tangatanga wamesema kuwa wako tayari kukabiliana na wenzao wa Kieleweke wanaopanga kutimua Naibu Rais kupitia bungeni.
Waliwataka wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenya na kiongozi wa ODM Raila Odinga wajiandae kwa makabiliano makali wabunge watakaporejea kutoka mapumzikoni.
Wabunge wanaounga handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga juzi walifichua mipango ya kutaka kumtimua Dkt Ruto kutokana na madai kwamba anahujumu rais.
Inaaminika kuwa mpango wa kumtimua Naibu Rais ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano utakaofanyika mjini Nanyuki.
Wanasiasa hao wanaounga handisheki watakutana siku ambayo wanasiasa wa Tangatanga nao watakuwa na mkutano wao wa kwanza wa kupigia debe ripoti ya BBI.
Viongozi wa Bonde la Ufa wakiongozwa na mbunge wa Soy, Caleb Kositany, walisema kuwa hoja ya kutaka kumtimua Dkt Ruto itatupiliwa mbali Bungeni.
“Walete hoja hiyo mara moja na tutaitupilia mbali,” Bw Kositany akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.
“Ili hoja ya kumtimua naibu wa rais ifaulu ni sharti iungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge. Dkt Ruto ana idadi kubwa ya wabunge hivyo itakuwa vigumu kwa mswada huo kupitishwa,” akaongezea.
Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono alisema kuwa wanaojiandaa kuwasilisha hoja hiyo ‘wanapoteza wakati kwani haitafaulu’.
“Wamegundua kuwa ripoti ya BBI imeanza kufa sasa wanataka kutumia njia za mkato kuingia mamlakani. Wajue kwamba Naibu wa Rais anaungwa mkono na wabunge zaidi ya 200.
“Wabunge wa upande wakiamua kutimua afisa yeyote wa serikali ataenda nyumbani kwani sisi ni wengi,” akasema Bw Rono, ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto.
Viongozi hao walisema kuwa kubanduliwa afisini kwa aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ni njia mojawapo ya kutishia wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto kuwa rais 2022.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema kuwa wandani wa Dkt Ruto wanaandamwa kwa lengo la kuzima safari ya Ikulu ya naibu wa rais.
“Gavana Waititu alibebeshwa msalaba kutokana na uhusiano wake wa karibu na Naibu wa Rais,” akasema Bw Cherargei, aliyekuwa miongoni mwa maseneta waliopinga kutimuliwa kwa Bw Waititu, Jumatano.
Mbunge wa Chesumei, Wilson Kogo, alisema kuwa wataendelea kumpigia debe Naibu wa Rais na ‘hatutaogopa vitisho’.
Alisema kuwa hawataruhusu Bw Odinga kutumia handisheki baina yake na Rais Kenyatta kutatiza azma ya Naibu wa Rais kuingia Ikulu 2022.
Bw Kogo alisema, “Masaibu ya Gavana Waititu yalitokana na siasa. Wale waliojiunga na serikali hivi karibuni wanalenga kutishia watu wanaounga mkono Dkt Ruto, lakini hatutawaruhusu.”
Lakini mbunge wa Cherang’any Joshua Kutuny aliambia Taifa Leo kuwa wameanza harakati za kukabiliana na wanasiasa wa Jubilee wanaohujumu Rais Kenyatta.
“Tumeanza mikakati ya kumfurusha Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen kwa kuhujumu BBI ambao ni mradi wa kiongozi wa chama Rais Kenyatta,” akasema Bw Kutuny.