Gavana Nyoro huru kuteua naibu wake
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA mpya wa kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro sasa yuko huru kumteua naibu wake.
Hii ni baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la gavana wa zamani Ferdinand Waititu , Dkt Nyoro azuiliwe kumtaja naibu wake kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi aliyowasilisha.
Agizo hili la mahakama sasa limeyumbisha kabisa azma ya Bw Waititu kurudi tena katika uongozi wa kaunti ya Kiambu hivi karibuni ikitiliwa maanani bado anakondolewa macho na kesi ya ufisadi ya Sh588m inayotokana na utoaji tenda za ujenzi wa barabara.
Matumaini yake yatasalia tu mahakamani lakini itachukua muda mrefu kujinanusua na mitego ya kesi dhidi yake.
Akitupilia mbali ombi la Bw Waititu , Jaji James Makau alisema Mahakama haina mamlaka kumzuia Dkt Nyoro kumteua naibu wake kwa vile “ni jukumu lake kikatiba kuwa na naibu.”
Jaji huyo alikubalia ombi la wakili Kibe Mungai anayemwakilisha Gavana Nyoro aliyeapishwa Ijumaa iliyopita baada ya Bunge la Seneti kumtimua mamlakani Bw Waititu kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.
Jaji Makau alisema baada ya Gavana Nyoro kuapishwa kutwaa hatamu za Ugavana “ Kilichobaki ni kuunda Serikali ya kaunti hiyo kwa kufanya teuzi mbali mbali.”
Akimsihi Jaji Makau atupilie mbali ombi la Bw Waititu anayewakilishwa na Bw Wilfred Nyamu, Bw Mungai alimweleza Jaji Makau kwamba wakati uliopo sasa ni gavana huyu mpya kuwateua mawaziri pamoja na naibu wake.
“Kesi hii ya Bw Waititu inalenga tu kuvuruga utenda kazi katika kaunti hii ya Kiambu ambayo kwa muda utoaji huduma umeathiriwa kufuatia Bw Waititu kukamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa ufisadi wa Sh588m,” alisema Bw Mungai.
Mahakama ilielezwa Bw Waititu ameunganisha kesi mbili za kujaribu kumtimua Dkt Nyoro uongozini na kumzuia asimteue naibu wake.
“Kesi hizi za Bw Waititu ni mbili na mwelekeo wapasa kutolewa jinsi ya kuzisikiza na kuziamua,” alisema Bw Mungai.
Jaji Makau aliamuru pande zote ziandae tetezi zake na ushahidi zitakazotegemea kuwasilisha kesi zao kabla ya kuteuliwa kwa siku ya kusikiza kesi hiyo.
Kitumbua cha Bw Waititu kiliingia mchanga Bunge la Seneti lilipopitisha hoja ya “kumtimua uongozini baada ya kumpata na hatia ya ufisadi.”
Ijumaa Bw Waititu alifika mahakama asubuhi na mapema kujaribu kusitisha hafla ya kusimamisha shughuli ya kuapishwa kwa Dkt Nyoro na Jaji John Onyiengo katika ukumbi wa kaunti ya Kiambu.
Jaji Weldon Korir alikataa kusitisha zoezi hilo na kumweleza Bw Waititu , “ hii ni hafla ya idara ya mahakama na kamwe haiwezi kusimamishwa.
Bw Waititu , mkewe Susan na washukiwa wengine 11 wamekanusha mashtaka ya kula njama iliyopelekea kaunti ya Kiambu kupoteza zaidi ya Sh588milioni.
Bw Waititu anakabiliwa na shtaka la kupokea Sh24milioni kwa njia ya ufisadi.
Bw Waititu amekanusha mashtaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana ya Sh10milioni.
Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Lawrence Mugambi alimwamuru Bw Waititu akome kuenda katika afisi za kaunti ya Kiambu na pia kutekeleza majukumu yake ya Ugavana.