Hatimaye serikali kumfidia Amrouche Sh108m
Na GEOFFREY ANENE
SERIKALI itagharamia fidia ya Adel Amrouche ya Sh108 milioni baada ya Shirikisho la Soka nchini Kenya kukatiza kandarasi yake Agosti 2014 kutokana na msururu wa matokeo duni alipokuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Harambee Stars.
Hayo yamefichuliwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF) Barry Otieno mnamo Jumatatu wakati wa kuzinduliwa rasmi kwa bodi ya Uchaguzi wa shirikisho hilo ulioratibiwa kufanyika kabla ya Machi 30, 2020.
Akizungumza baada ya kutambulisha maafisa wa bodi hiyo itakayokuwa chini ya afisa wa mawasiliano Kentice Tikolo, Otieno alisema kuwa FKF imefanya mazungumzo na serikali ikitafuta kulipa deni hilo.
“Serikali imeonyesha iko tayari kutunusuru kutokana na deni hilo kubwa. Tumekuwa tukitatizika kugharamia timu zetu za taifa ikiwemo ile ya wanawake ya Harambee Starlets kwa hivyo tuliona itakuwa busara kuomba Wizara ya Michezo itusaidie kutatua utata wa kumlipa Amrouche,” alisema Otieno katika makao makuu ya FKF mtaani Kasarani.
Katika kipindi chake kama kocha mkuu wa Kenya kati ya Machi 23, 2013 na Agosti 30, 2014, Amrouche aliongoza Harambee Stars katika mechi tisa.
Stars ilichapa Namibia na Comoros 1-0, ikatoka 1-1 dhidi ya Super Eagles ya Nigeria na kupiga sare nyingine kama hiyo dhidi ya Comoros pamoja na kukabwa 2-2 dhidi ya Malawi na 0-0 dhidi ya Lesotho na kupoteza dhidi ya Nigeria, Lesotho na Misri kwa bao 1-0.
Isipokuwa mechi ya Misri iliokuwa ya kirafiki, mechi hizo zingine zilikuwa za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON). Kenya haikufuzu.
Kutoka Kenya, Amrouche, ambaye ana uraia wa Algeria na Ubelgiji, alitua Libya na kuongoza timu ya taifa katika mechi moja pekee na kisha kujiunga na klabu ya MC Algiers nchini Algeria kabla ya kunyakuliwa na Botswana mwezi Agosti mwaka 2019.
Hajapata ushindi Botswana baada ya kuiongoza ikiumiza nyasi bure dhidi ya Malawi na Zimbabwe na kupoteza dhidi ya Malawi, Misri na Algeria. Amrouche alishtaki Kenya kwa kumpiga kalamu kabla ya kandarasi yake kumalizika na kushinda kesi hiyo.
FKF ina madeni mengi na makocha wa zamani. Mbali na Amrouche, Kenya pia inahitaji kulipa Bobby Williamson Sh55 milioni kwa kukatiza kandarasi ya kocha huyo kutoka Scotland mwaka 2016.
Vilevile, kocha Mfaransa Sebastien Migne anadai Kenya mamilioni ya fedha za Kenya baada ya FKF kumtimua mwezi Agosti mwaka 2019.