Miereka ya Uhuru na Ruto yamwinua Raila kisiasa
Na PETER NGARE
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amechukua fursa ya miereka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kujijenga kisiasa.
Huku Rais Kenyatta na Dkt Ruto wakipigana na kubomoa chama chao cha Jubilee, Bw Odinga amekuwa akijenga ODM na kutumia mchakato wa BBI kujiuza kwa Wakenya.
Malumbano baina ya wakuu hao wawili wa taifa yamewafanya kushindwa kuwa na msimamo mmoja kuhusu masuala ya nchi ikiwemo BBI na pia miradi ya maendeleo.
Rais na naibu wake pia wamefanikiwa kugawanya wafuasi wao katika mirengo ya ‘Kieleweke’ wake Rais Kenyatta na ‘Tangatanga’ wa Dkt Ruto.
Bw Odinga ametumia fursa hiyo kupenyeza Ikulu ambapo sasa anashirikiana na Rais Kenyatta katika masuala mbalimbali ya utawala wakati Dkt Ruto akitengwa.
Hatua hii inaweka ODM katika nafasi bora ya kujiimarisha kufikia uchaguzi mkuu wa 2022 huku Jubilee ikisambaratika kutokana na mizozo kati ya kinara na naibu wake.
Bw Odinga, ambaye aliacha siasa za upinzani mnamo 2018 na kujiunga na mrengo wa Rais Kenyatta katika Serikali Kuu, amefanikiwa kuonyesha kuwa ndiye mwenye usukani wa BBI, ambayo alianzisha pamoja na Rais Kenyatta baada ya handisheki mnamo 2018.
Lakini tangu ripoti ya BBI ilipozinduliwa Novemba mwaka jana, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wametekwa na mivutano baina yao na kumwachia Bw Odinga usukani wa kusukuma mchakato huo.
Katika mikutano ya kupigia debe BBI iliyoanza mwezi uliopita, Bw Odinga amekuwa ndiye nyota, hatua ambayo imeinua hadhi yake kisiasa.
Kufikia sasa Bw Odinga ameongoza mikutano ya kupigia debe BBI katika ngome zake za Nyanza, Magharibi, Pwani na Ukambani.
Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawakuhudhuria mikutano hiyo licha ya kusema kuwa wanaunga mkono BBI, jambo ambalo limempa Kiongozi wa ODM fursa ya kung’aa.
Juhudi za mrengo wa Dkt Ruto serikalini kuingia kwenye ‘basi’ la mchakato huo katika juhudi za kuzima nyota ya Bw Odinga zimegonga mwamba.
Washirika wake kama Moses Kuria (Mbunge wa Gatundu Kusini) na Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet wamejipata matatani katika mikutano miwili waliyohudhuria Mombasa na Kitui.
Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wangali wanavutana kuhusu BBI huku Naibu Rais akieleza kutoridhishwa na baadhi ya masuala yaliyo ndani ya ripoti hiyo.
Wanasiasa wa mrengo wa Rais Kenyatta ambao wamekuwa wakihudhuria mikutano ya BBI nao wameharibu mambo zaidi kwa kutumia fursa hiyo kumshambulia Dkt Ruto.
Hatua hiyo imeongeza uhasama kati ya Tangatanga na Kieleweke wakati ODM ikiendelea kujenga umoja wake.
Rais na naibu wake wamekuwa wakitumia kila fursa wanayopata kupimana nguvu huku siasa kati yao zikiingia hatua hatari kiasi cha wandani wao kudai kuwa kila mmoja anakula njama ya kumng’oa mwingine madarakani.
Rais Kenyatta amekuwa akimlaumu Dkt Ruto akidai anahujumu maendeleo kwa siasa za kila mara za 2022 na hivyo kutatiza utimizaji wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.
Katika ngome zao za kisiasa hasa ya Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya, wakazi wamegawanyika kuhusu BBI huku walio upande wa Rais wakiunga mkono na wale wa mrengo wa Dkt Ruto wakiipinga.