• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
SHINA LA AFYA: Madhara ya vinywaji vya kuongeza nguvu

SHINA LA AFYA: Madhara ya vinywaji vya kuongeza nguvu

Na BENSON MATHEKA

KATIKA kona ya kilabu kimoja mjini Athi River, Jane, mwanadada mwenye umri wa miaka 26 na marafiki zake wanafurahia vinywaji.

Hawatumii pombe ila meza yao imejaa mikebe ya vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini au ukipenda vinywaji nishati, maarufu kama ‘Energy Drinks’.

Kwa muda wa saa tatu nilipokuwa katika kilabu hicho, nilihesabu Jane akiteremsha mikebe mitano ya kinywaji hicho na kwa kweli alionekana mchangamfu na mwenye nguvu.

“Mimi nachukia pombe lakini ninatumia ‘Redbull’ kwa sababu inanichangamsha,” Jane aliniambia. Wenzake walikuwa wakitumia vinywaji kama ‘Shark’, ‘Speedo’, ‘Bravo’ na ‘NRG’.

Kile ambacho Jane na marafiki zake hawakufahamu ni hatari ambayo vinywaji hivi vinaweza kusababishia mtu akivitumia kwa wingi na kwa muda mrefu.

Vinywaji hivi vimekuwa maarufu mno na vinachuuzwa mitaani japo wataalamu wanasema matumizi yake ni hatari kwa afya.

Vingi vimeidhinishwa kuuzwa nchini na idara husika huku wataalamu wakisema umma unahitaji kuhamasishwa zaidi kuhusu athari zake.

Kulingana Shirika la Afya Duniani-WHO, vinywaji hivi ambavyo vinaendelea kuongezeka na kupata umaarufu ulimwenguni, vinasababishia watu matatizo mengi ya kiafya ikiwa ni pamoja na kifo.

WHO inasema kwamba vinywaji hivyo huwa na kiwango cha juu cha kafeini na kunywa kiwango kikubwa kwa wakati mmoja na kwa muda mrefu kunasababisha madhara ya kiafya na hata kifo.

“Kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini kwa wingi kunaweza kusababishia umma matatizo ya kiafya hasa walio na umri mdogo,” wanaonya wataalamu wa WHO kwenye ilani katika tovuti yake.

Ingawa havileweshi, wataalamu wa afya wanasema kwamba vinatengenezwa kwa kutumia kafeini, dawa ambayo ikitumiwa kwa wingi inasababisha matatizo ya kiafya na hata kufanya mtu kuwa mraibu.

Darius Kimiza, mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Machakos anasema kwamba hakujua alikuwa mtumwa wa vinywaji hivi hadi alipoanza kuugua.

“Nilikuwa ninatumia mkebe mmoja wa kinywaji cha nishati kila asubuhi, saa saba na saa kumi. Singeweza kufanya kazi bila kutumia kinywaji hicho hadi nilipougua na daktari akanishauri niache kukitumia kabisa,” asema Bw Kimiza.

Miongoni mwa matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo ni moyo kupiga kwa kasi na kushindwa kupata usingizi.

Kulingana na mtaalamu wa matatizo ya moyo, Dkt Sebastian Kairu, vinywaji vya kuongeza nguvu vinaweza kusababisha matatizo ya moyo na hata kuufanya ushindwe kufanya kazi kwa sababu ya kiwango vya juu cha kafeini na hata kifo.

“Vinywaji hivi havifai kutumiwa kwa wingi hasa na watoto. Katika baadhi ya mataifa vimeorodeshwa kama dawa na huuzwa katika maduka ya kuuzia dawa pekee,” asema Kairu.

Kulingana na WHO, vinywaji hivi havifai kuuziwa watoto walio na chini ya umri wa miaka 18.

Dkt Kairu anaonya watu walio na matatizo ya moyo kutotumia vinywaji hivi kwa wingi.

“Kabla ya kutumia kinywaji nishati au hata kafeini, ni muhimu kuhakikisha moyo wako hauna tatizo,” asema.

Utafiti wa hivi punde katika jarida la Journal of Amino Acids unaonyesha kuwa vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini vinachangia ongezeko la maradhi ya moyo ulimwenguni.

Katika utafiti huo, watu 4,854 waliofuatiliwa waliripoti kuathiriwa na matumizi ya vinywaji hivi huku asilimia 51 wakiwa ni watoto. Wataalamu waliofanya utafiti huo wanapendekeza watoto kutotumia zaidi ya mililita 250 za kinywaji hiki kwa siku.

Aidha, wanaonya kuwa ni hatari kutumia vinywaji hivi wakati wa michezo au mazoezi ya viungo vya mwili.

Kulingana na utafiti mwingine uliofanywa 2016 na wataalamu wa moyo nchini Canada na kuidhinishwa na WHO, watu walio na umri wa kati ya miaka 18 na 40 wanaotumia vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini, walipata matatizo ya mpigo wa moyo.

WHO inasema kwa vile vinywaji hivyo huwa na viwango vya juu vya sukari, vinasababisha mishipa kudhoofika.

Utafiti uliochapishwa mwaka jana katika jarida la American Journal of Heart Association ulibaini kuwa lita ikitumiwa katika muda wa dakika 60, inabadilisha mpigo wa moyo na kusababisha msukumo wa damu.

Wataalamu 20 waliofanya utafiti huo walihusisha hali hii na kafeini.

Madhara yake

• Maumivu ya kichwa

Wataalamu wanasema hata kwa barobaro wasio na matatizo ya kiafya, matumizi ya vinywaji hivi huwafanya waumwe na kichwa, kukosa usingizi na kuwa na mfadhaiko wa hali ya juu.

• Type 2 Diabetes

Dkt Kairu anaeleza kuwa, kwa sababu ya kiwango cha juu cha sukari kinachotumiwa kutengeneza vinywaji hivi, wanaovitumia kwa wingi na kwa muda mrefu wanaweza kupata Kisukari aina ya Type 2.

“Kiwango cha juu cha sukari kwenye vinywaji hivi kinaweza kuua seli zinazotoa homoni ya Insulin katika kongosho (pancreas) na mtu kupata kisukari aina ya type 2,” aeleza.

Anasema baadhi ya vinywaji nishati vinaweza kufanya dawa kushindwa kufanya kazi mwilini.

• Kutetemeka na wasiwasi

Vikitumiwa kwa muda mrefu, vinywaji hivi vinaweza kufanya mtu kuanza kutetemeka na kuwa na wasiwasi hali ambayo wataalamu wanahusisha pia na kafeini.

“Hali hii inaweza kufanya mtu kushindwa kutekeleza majukumu yake. Inaweza pia kufanya mtu kushindwa kudhibiti hisia zake,” asema

• Kutapika

Watalaamu wanasema vikitumiwa kwa wingi, vinaweza kufanya mtu kutapika na kupunguza kiwango cha maji mwilini. Kwa sababu huwa vina asidi, vinaweza kuharibu meno na koo la mtu.

• Mzio (Allergy)

Kulingana na Dkt Resla Odhiambo wa hospitali ya Penda, jijini Nairobi, vinaweza kusababisha mzio ikiwa ni pamoja na kuwasha kwa ngozi na koo.

• Kiharusi

Wataalamu wanaonya watu walio na msukumo wa damu dhidi ya kuvitumia wakisema vinaweza kusababisha kiharusi (stroke).

Kulingana na utafiti uliofanywa na Mayo Clinic na kuchapishwa katika tovuti ya shirika hilo, mkebe mmoja wa vinywaji hivi unaongeza presha ya damu kwa asilimia 6.4.

• Kuhara

Matatizo mengine ambayo yanahusishwa na matumizi ya vinywaji hivi kwa wingi ni kuhara, maumivu ya viungo, kuhisi kizunguzungu na mfadhaiko.

“Sana ikizidi sana huwa ni hatari na ndivyo ilivyo kwa wanaotumia vinywaji vya kuongeza nguvu. Watu wanashauriwa kuvitumia kwa mpango. Kafeini na viungo vingine katika vinywaji hivi ni dawa na vinapaswa kutumiwa kwa kiwango kilichopendekezwa kwa siku,” asema Dkt Kairu.

Mbali na kafeini na sukari, WHO inasema viungo vinavyotumiwa kutengeneza vinywaji hivyo kama vile ‘guarana’, ‘taurine’ na vitamin B vinapaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi kubaini vinavyoweza kutumika pamoja na kafeini.

Wataalamu wanaonya watu dhidi ya kuchanganya vinywaji hivi na pombe wakisema imethibitishwa kufanya hivi kunasababisha kifo.

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Usalama wa Chakula barani Ulaya (European Medicines Evaluation Agency-EMEA), ulifichua kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu walio na umri wa kati ya miaka 18 na 29 huchanganya vinywaji hivi na pombe.

Kulingana na Dkt Odhiambo wanawake wakiwa na mimba hawafai kuvitumia hata kama wanahisi udhaifu.

“Ni hatari kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kutumia vinywaji hivi kwa sababu ya kafeini. Ingawa vinaweza kukosa kumdhuru mama akitumia kwa kiwango kidogo, kafeini inaweza kuathiri mtoto anayenyonya,” asema.

Vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyopendekezwa kwa akina mama wajawazito na wagonjwa ni Lucozade, Ribena na Boost kwa wanamichezo ambavyo vina viwango vya chini vya kafeini.

Kulingana na Dkt Odhiambo, kiwango cha kafeini kinachohitajika kuwa katika vinywaji ni chini ya miligramu 40. Baadhi ya vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyouzwa nchini vina zaidi miligramu 80.

You can share this post!

Huzuni Kakamega wanafunzi 13 wakifariki shuleni

Tanzia: Rais Mstaafu Daniel Arap Moi amefariki

adminleo