Jinsi Moi alivyoenziwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyimbo
Na CHARLES WASONGA
NYIMBO nyingi zilitungwa kumsifu Hayati Rais (mstaafu) Daniel Moi na utawala wake uliodumu kwa kipindi cha miaka 24.
Wadadisi wanasema watunzi wa nyimbo hiyo walishawishiwa kuzitunga kama sehemu ya mpango mzima wa kukita falsafa ya Moi miongoni mwa Wakenya.
Hii ndio maana makundi ya kwaya, wanamuziki wa kibinafsi waling’ang’ania nafasi ya kumtumbuiza Moi wakati wa hafla za kitaifa na katika ziara zake kote nchini.
Nyimbo kama vile, “Tuashangilie Kenya” na “Tawala Kenya Tawala”, zilizotungwa msanii Thomas Wesonga ziliondokea kuwa maarufu zaidi wakati wa sherehe za kitaifa na hafla za chama tawala nyakati hizo-Kanu.
Ingawa ilidaiwa kuwa nyimbo kama hizo zilikuwa za kizalendo, ukweli ni kwamba zililenga kuvumisha na kuendeleza utawala wa Moi pamoja na chama cha KANU.
Njia nyingine ambayo Moi alitumia kukita utawala wake mawazoni mwa Wakenya ni kupitia vyombo vya habari.
Alihakikisha kuwa kila siku asilimia 80 ya taarifa za habari katika iliyokuwa Sauti ya Kenya (VOK), sasa Shirika la Habari Nchini (KBC) zilihusu shughuli alizoshiriki. Shughuli hizo ni kama vile michango ya harambee, ziara zake za ng’ambo, uzinduzi wa miradi ya serikali yake, ibada za Jumapili, miongoni mwa nyingine.
“Kwa njia hii Wakenya walielekezwa kuamini kuwa Moi ndiye alikuwa kiongozi pekee ambaye aliongoza katika kila kitu. Alichukulia kama mkulima nambari moja, mwalimu nambari moja na mwanasiasa nambari moja,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Edward Kisiang’ani.
Kwa upande mwingine, taasisi za nyingi za umma zilipewa jina la Moi katika mpango huo huo wa kuendeleza falsafa ya uongozi wake. Shule za msingi na zile za upili, vyuo vya kiufundi, vyuo vikuu, hospitali za umma, viwanja vya michezo na asasi nyinginezo zilizoanzishwa wakati wa utawala wake, zilitajwa kwa jina lake.
Taasisi hizi zilipatikana katika tarafa, wilaya na mikoa mbalimbali nchini.
“Kwa namna hii, Mzee Moi alihakikisha kuwa amekolea katika fikra za Wakenya kila siku. Lengo hapa lilikuwa ni kuhakikisha Wakenya hawangewaza kuhusu kiongozi mwingine – hasa mwanasiasa – isipokuwa Moi,” anaeleza Profesa Kisiang’ani ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Hii ndio maana, anasema, ndio maana wanasiasa kama vile marehemu JJ Kamotho, Oloo Aringo, Wilson Letich miongoni mwa wengi walimuezi Moi kiasi cha kumuabudu.
Katika mkutano wa kisiasa eneo la Rift Valley mnamo 1999, marehemu Kamotho alipiga magoti mbele ya Moi jukwaa ili amnong’onezee jambo. Naye Bw Aringo alipenda kumsifu kama Mfalme wa Amani huku Leitich akitisha kukata kidole cha mtu yeyote ambaye angethubutu kumtusi Moi na chama cha Kanu.
Wanasiasa hawa walifanya haya yote kuonyesha uaminifu kwa Moi ili waendelea kudumu siasani.