BURIANI MOI: Alitengana na mkewe 1974 wakiwa na wana 8
NA MWANDISHI WETU
MZEE Daniel Toroitich Moi alitengana na mkewe Lena Moi mwaka wa 1974 wakiwa wamejaliwa watoto wanane, wavulana watano na wasichana watatu.
Kifungua mimba wao (mvulana) ni Jonathan Toroitich Moi ambaye alitambuliwa nchini kwa kushiriki mbio za magari za Safari Rally.
Jonathan aliaga dunia mwaka jana baada ya kuugua saratani. Mwanawe wa pili ni Philip Moi ambaye ni mwanajeshi mstaafu.
Philip alijulikana nchini wakati wa kesi ya talaka kati yake na mkewe Rosanna Pluda. Raymond Moi ni mwanasiasa na mbunge wa sasa wa eneobunge la Rongai, Kaunti ya Nakuru ambaye hapendi kujitokeza sana katika vyombo vya habari.
John Mark Moi ni pacha na Doris Moi. Ni mwanajiolojia katika wizara ya madini ya Kenya na hajulikani na watu wengi
Jennifer Jemutai Kositany ndiye kifungua mimba wa Mzee Moi na Lena Moi ambaye alikuwa ameolewa na mfanyabiashara raia wa Uingereza. Walimiliki biashara kubwa kubwa hasa mashamba ya majani chai.
June Moi ndiye kitinda mimba wa Mzee Moi. Alijulikana kwa kuhusika pakubwa na kampeni za baba yake kwenye uchaguzi wa 1992 na 1997.
Doris Moi ni pacha na John Mark ambaye alikaidi baba yake na kuolewa na mwana wa aliyekuwa mwanasiasa Ibrahim Choge, Simon.
Simon ambaye alikuwa dereva msaidizi wa Jonathan Moi kwenye safari Rally alikufa kwenye ajali katika hali ya kutatanisha.
Gideon Moi ambaye ni seneta wa sasa wa Baringo alikuwa kipenzi cha baba yake. Alijiunga na siasa na kuchaguliwa mbunge wa Baringo ya Kati.
Ndiye mwenyekiti wa chama cha KANU ambacho baba yake alitumia kutawala Kenya kwa miaka 24 na ana azima ya kugombea urais.