• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
BURIANI MOI: Alipata upinzani mkali kuliko Ruto lakini bado akawa Rais

BURIANI MOI: Alipata upinzani mkali kuliko Ruto lakini bado akawa Rais

Na BENSON MATHEKA

DANIEL Moi aliingia mamlakani 1978 baada ya kifo cha Mzee Jomo Kenyatta licha ya upinzani mkali, kuliko anaopata Naibu Rais Dkt William Ruto kwa sasa, kutoka kwa wandani wa mtangulizi wake.

Hata hivyo, halikuwa jambo geni kwake kwani tangu mwanzo alifahamu kulikuwa na maadui ambao wangepanga kumtimua mamlakani.

Mnamo Agosti 1, 1982 hofu yake ilitimia wakati baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha wanahewa wakishirikiana na wanasiasa walifanya jaribio la kupindua serikali yake.

Ilikuwa moja ya siku za giza kuu katika historia ya Kenya ambapo baadhi ya wakazi wa jiji la Nairobi walipoteza maisha, mali kuharibiwa na kuporwa kabla ya wanajeshi wa nchi kavu kuzima jaribio hilo.

Wanajeshi hao waasi walivamia kituo cha utangazaji cha serikali wakati huo kikijulikana kama Voice of Kenya (VoK) na kutangaza kuwa serikali ilikuwa chini ya wanajeshi.

Ilichukua ujasiri wa aliyekuwa mkuu wa majeshi wakati huo Jenerali Jackson Kimeu Mulinge baadaye kumhakikishia Moi atoke mafichoni baada ya jaribio hilo kuzimwa ndipo akajitokeza na kutangaza kuwa alikuwa angali uongozini.

Kufuatia jaribio hilo lililoongozwa na Senior Private Hezekiah Ochuka na Pancras Okumu, Moi alibadilika pakubwa kwa hofu kuwa kila mara kulikuwa na njama ya kuangusha serikali yake.

Wanahistoria wanasema kuwa ni jaribio hilo la mapinduzi ambalo lilimbadilisha Moi ndiposa akaanza utawala wa kidikteta na kutowavumilia waliokosoa utawala wake kwani aliwaona kuwa wenye nia ya kumwondoa.

Aliimarisha idara ya ujasusi na kuhakikisha kuwa waliokuwa serikalini ni wale tu waaminifu kwake chini ya chama cha Kanu.

Tukio hilo la 1982 linaaminika kuchangia maamuzi aliyofanya baada ya hapo. Katika juhudi za kulinda serikali yake isipinduliwe, alipalilia ukabila kwa kuteua katika nyadhifa kuu watu alioamini kutoka eneo la Rift Valley na kutenga jamii alizoshuku kuwa hatari kwa serikali yake hasa katika eneo la Mlima Kenya na Nyanza.

Mzee Moi alikuwa mwenye uwoga wa yeyote ambaye angethubutu kukosoa utawala wake na miongoni mwa waliomtia hofu ni wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Katika kuhakikisha wanafunzi hao wamethibitiwa, mnamo 1984 alianzisha mafunzo ya lazima kwa wanafunzi waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu. Mpango huo ulinuiwa kufanya wanafunzi hao kuwa na nidhamu na waaminifu kwa serikali wakiwa chuoni.

Hata hivyo, badala ya kuwafanya kuwa waaminifu ilivyokusudiwa, mafunzo hayo yaliwafanya wanafunzi hao kuwa sugu dhidi ya Moi na serikali yake.

Ni wanafunzi waliopata mafunzo hayo ambao waliongoza upinzani dhidi ya serikali ya Moi miaka ya themanini na tisini. Fujo za wanafunzi zilishamiri badala ya kupungua kama alivyotaka wanafunzi wakipinga sera zake.

Mnamo 1990, serikali ya Moi ililaumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Dkt Robert Ouko.

You can share this post!

BURIANI MOI: Kutoka mchungaji mifugo, mwalimu hadi Ikulu

BURIANI MOI: Aliwakabili vikali watu waliokosoa utawala wake

adminleo