Habari MsetoSiasa

BURIANI MOI: Alipuuzwa kuwa wingu linalopita lakini akasalia Ikulu miaka 24

February 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

DANIEL Toroitich Arap Moi alipochukua hatamu ya uongozi kutoka kwa mzee Jomo Kenyatta 1978, baadhi ya wanasiasa kutoka Kiambu akiwemo Charles Njonjo, walimfananisha na wingu linalopita.

Moi aliendeleza hulka yake ya unyenyekevu hadi aliposhinda uchaguzi na kutwaa mamlaka kama rais kikamilifu 1979.

Waliokuwa wamepofushwa na mamlaka chini ya utawala wa Mzee Kenyatta hawakuamini angeweza kuongoza.

Hata hivyo, wingu lililobashiriwa kuwa linapita liliganda na kubaki usukani kwa miaka 24. Moi akawa rais aliyehudumu kwa miaka mingi katika historia ya Kenya.

Akihojiwa na runinga ya NTV kabla ya kifo chake, John Keen, mmoja wa waliokuwa wanasiasa wakakamavu alisema waliodhani Moi alikuwa kiongozi dhaifu ambaye wangemuondoa kwa urahisi walikuwa wamekosea.

“Watu kutoka eneo la Kati walikuwa wakimfananisha na wingu linalopita lakini walikuwa wamekosea,” Bw Keen alisema kwenye mahojiano na NTV mnamo 2013.

Aliyekuwa mkuu wa kitengo cha habari cha Rais Moi Lee Njiru aliambia kituo hicho kwamba waliomfananisha Moi na wingu linalopita waliamini kuwa ni eneo lao linalofaa kuamua atakayeongoza Kenya.

“Licha ya dua zao, Moi aliongoza kwa miaka 24, miezi minne na siku nane,” alisema Bw Njiru mmoja wa watu ambao waliaminiwa sana na Rais Moi.

Wadadisi wanasema kile ambacho waliokuwa wakimpiga vita Moi walisahau ni kuwa alikuwa amejenga mtandao wa marafiki kote nchini na nje ya nchi alikokuwa akimwakilisha mkubwa wake Mzee Kenyatta ambaye hakupenda kutembea sana kwa sababu ya umri na kuugua.