• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
BURIANI MOI: Maana kamili ya ‘Nyayo’

BURIANI MOI: Maana kamili ya ‘Nyayo’

Na CHARLES WASONGA

Daniel Moi alianzisha miradi mbalimbali ambayo inaakisi kumbukumbu ya utawala wake wa miaka 24.

Mojawapo ya miradi hiyo ni mfumo wa elimu wa 8-4-4 ulioanzishwa mnamo 1985.

Mfumo huu, ambao serikali inapanga kuufutilia mbali, ulichukua mahala pa mfumo wa zamani wa 7-4-2-3.

Kimsingi, mfumo wa 8-4-4 ulianzisha masomo ya kiufundi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne lengo likiwa ni kumpa mwanafunzi ujuzi ya kumwezesha kujitegemea maishani.

Lakini baada ya miaka kadhaa mfumo huo ulianza kuonyesha dalili za kushindwa kufikia malengo yake asilia na sasa serikali imeleta ule wa CBC wa 2-6-3-3-3.

Mabasi Ya Nyayo

MABASI ya Uchukuzi ya Nyayo (NBS) yalianzishwa na Rais mstaafu Daniel Moi mnamo 1986 kwa lengo la kutoa huduma za uchukuzi jijini Nairobi.

Serikali ilidai mabasi ya kampuni ya Kenya Bus Services (KBS) yalilemewa na ongezeko la idadi ya watu jijini nyakati hizo.

Lakini wakosoaji wa mpango huo walidai kuwa serikali ilianzisha mabasi ya Nyayo kwa sababu ilitaka kumaliza kampuni ya KBS baada ya kampuni hiyo ya Uingereza kukataa kuiuzia hisa.

Mabasi hayo yalikuwa yakitoza nauli nafuu kuliko mabasi ya KBS na wahudumu wake walitoka Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS).

Lakini kuanzia mwaka wa 1994, kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi miongoni mwa wafanyakazi na wasimamizi wa mabasi hayo, kampuni hiyo ilianzia kufifia.

Hatimaye mnamo 1997 kampuni hiyo ilisitisha shughuli na mamia ya Wakenya kutoka NYS na vyuo vikuu wakaachwa bila ajira.

Wadi za Nyayo

Wadi za Nyayo zilikuwa nguzo kuu ya mpango wa afya chini ya utawala wa Rais Moi ambazo zilichangia kupanuliwa kwa hospitali za umma.

Wadi hizo zilijengwa katika hospitali za wilaya licha ya serikali kukabiliwa na changamoto katika ufadhili wa miradi ya afya haswa miaka ya 1990s baada ya mashirika ya kifedha ya kimataifa kukatiza misaada kwa Kenya.

Ili kukabiliana na shida hiyo, Mzee Moi aliandaa harambee katika wilaya kadha nchini kuchanga fedha za kufadhili ujenzi wa wadi hizo.

Ni katika utawala wa Moi ambapo Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) ilifanyiwa mageuzi ili iweze kuwahudumia wafanyakazi katika sekta ya umma.

Vile vile, ni wakati wa enzi ya Moi ambapo ugonjwa wa Ukimwi ulitangazwa kuwa janga la kitaifa mnamo Novemba 1999. Hatua hiyo ilipelekea kuuanzishwa kwa Baraza la Kitaifa la Kupambana na Ukimwi (NACC) na likapewa wajibu wa kushirikisha mipango ya kuzuia kuenea katika sekta zote.

Shirika la Nyayo Tea Zones

Shirika hili lilibuniwa mnamo 1986 kwa lengo la kuhifadhi misitu kupitia upanzi wa majanichai katika maeneo yanayopakana na misitu ya serikali. Lengo lilikuwa ni kuzuia watu kuingia na kuharibu misitu katika maeneo 19 kote nchini

Shirika hilo linamiki kiwanda cha Majanichai cha Kipchabo kilichoko katika kaunti ya Nandi. Na wakati huu shirika hilo linajenga kiwanda cha pili cha majani cha Gatitu katika kaunti ya Kirinyaga.

Mzee Moi pia atakumbwa kama kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kuongoza mipango ya uhifadhi wa udongo kwa ajili ya kufanikisha miradi ya kilimo.

You can share this post!

BURIANI MOI: Alipuuzwa kuwa wingu linalopita lakini...

BURIANI MOI: Alivyodumisha amani nchini huku akiwatesa...

adminleo