• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 10:50 AM
VYAMA VYA KISWAHILI: CHAKILA: Jukwaa bora la makuzi ya Kiswahili Shuleni Laverna, Kaunti ya Machakos

VYAMA VYA KISWAHILI: CHAKILA: Jukwaa bora la makuzi ya Kiswahili Shuleni Laverna, Kaunti ya Machakos

Na CHRIS ADUNGO

SHULE ya Msingi ya Laverna katika Kaunti ya Machakos ni miongoni mwa shule nyingi kutoka humu nchini ambazo kwa sasa zinatambua umuhimu wa Mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huu, NMG inatumia gazeti lake la Taifa Leo kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili nchini.

Bw Stephen Muli ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Laverna, anasema kwamba majaribio ya mitihani katika gazeti hili la Taifa Leo ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika Kiswahili huku wakihimizwa kuthamini masomo mengine kwa kiwango sawa.

Bw Muli anazisihi shule nyinginezo za humu nchini kuiga mfano wao ili kuimarisha viwango vya utayarifu wa wanafunzi wakati wanapojiandaa kuikabili mitahini ya KCPE mwaka huu wa 2020.

“Majaribio hayo ya mitihani huwaondolea hofu wanafunzi wengi wanaotazamia kutahiniwa kwa kuwa huwaweka katika hali ya kujiamini. Hili huwatia motisha ya kujituma maradufu kila wanapotumia maswali na majibu ya mitihani katika gazeti ili kujitia kwenye mizani na kujikosoa wakati mwingine bila ya hata msaada wa mwalimu wao,” anasema Bw Muli.

Kwa mujibu wa mwalimu huyu aliyejiunga na Shule ya Msingi ya Laverna mnamo 2010, jamvi la Chama cha Kiswahili shuleni humo (CHAKILA) linatarajiwa kukunjuliwa rasmi na wapenzi wa Kiswahili mwaka huu wakiwa na lengo la kubadilisha mtazamo hasi kwa somo la lugha hiyo miongoni mwa wanafunzi na hata kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa walimu wenzake.

Ikiongozwa na Bw Muli, Bw Robert Wambua, Bw Joseph Kitavi na Bw Bernard Musyala; kamati ya walimu wa Kiswahili shuleni humo itateua jopo la wanafunzi ambao watatwikwa jukumu la kuwa vinara wa chama baada ya kubaini utashi wao katika kukichapukia Kiswahili kwa ufasaha mkubwa.

Kupitia CHAKILA, wanafunzi watafunguliwa milango ya kuwawezesha kukithamini Kiswahili na kuwa mtazamo chanya kuhusu masomo ya lugha, sarufi na kujieleza vizuri kupitia usomaji, uandishi wa insha bora na mijadala ya kina kuhusu masuala ibuka nchini.

Wanaolengwa kunufaika pakubwa kutokana na mipango hii ni wanafunzi wote shuleni kila watakapotumia CHAKILA kuwa chombo cha kuzizamia mada ambazo zinawatatiza darasani na kuandaa hafla za Kiswahili zitakazoshirikisha shule nyinginezo ndani na nje ya Kaunti ya Machakos.

Mbali na kutekeleza jukumu kubwa la kutambua na kukuza vipaji mbalimbali vya wanafunzi katika uandishi wa kazi za kibunifu na kughani mashairi kwa mahadhi mbalimbali, chama pia kitatoa jukwaa mafaka kwa wanafunzi kujifundisha jinsi ya kuwa mahatibu mahiri na kujadili matumizi fasaha ya misamiati mbalimbali kupitia midahalo na warsha za kila mara.

Katika kulifikia hili, chama kitaanzisha mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa madhumuni ya kuwakutanisha wanafunzi na baadhi ya walimu, wanahabari na waandishi maarufu ya Kiswahili ambao kwa wengi, ni vielelezo.

You can share this post!

MAPITIO YA TUNGO: Ndoto ya Amerika; Novela ya kitashtiti...

SEKTA YA ELIMU: Uhamisho wa walimu utavuruga masomo...

adminleo