Michezo

HISTORIA ILE! Pires asema Liverpool yaweza kutwaa ubingwa bila kushindwa

February 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, Uingereza

ALIYEKUWA mshambuliaji matata wa Arsenal, Robert Pires amesema klabu ya Liverpool inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) bila kushindwa, kama ilivyofanya Arsenal msimu wa 2003-2004.

Pires amesema huu ndio msimu bora zaidi katika historia ya klabu hiyo ya Anfield, ambayo imejikita kileleni mwa ligi kwa tofauti ya pointi 22 – ikiwa timu ya pekee kutoshindwa katika mechi 24 kufikia sasa.

Kutokana na tofauti hiyo kubwa, Pires anaamini hakuna atakayewazuia vijana wa kocha Jurgen Klopp kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 tangu 1990.

Ushindi wao majuzi wa 4-0 dhidi ya Southampton nyumbani Anfield uliwezesha Reds kufikisha pointi 73, huku nambari mbili Manchester City wakiwa na alama 51.

Iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi, basi itakuwa kwa mara ya 20.

Aidha, watakuwa na mataji sawa na wapinzani wao wakuu, Manchester United ambao walishinda ligi mara ya mwisho msimu wa 2012-2013, chini ya kocha mkongwe Sir Alex Ferguson. Ferguson alitangaza kustaafu baada ya msimu huo.

Katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Southampton, Liverpool walikabwa kipindi cha kwanza kabla ya kunyeshea wapinzani mabao baada ya mapumziko.

Southampton walikuwa sako kwa bako na Liverpool kwa kipindi cha saa nzima cha mchezo, huku Danny Ings akikaribia kutundika goli kipindi cha kwanza naye Shane Long akinyimwa goli na kipa Alisson Becker.

Reds walikaa ngangari kulinda ngome yao na hatimaye kupata mpenyo kupitia kwa kiungo Alex Oxlade-Chamberlain, aliyepiga kombora la chini nje kijisanduku cha penalti na kufungua ukurasa wa mabao.

Bao la pili lilitiwa kimiani na nahodha Jordan Henderson baada ya kuandaliwa pasi safi na Robert Firmino, aliyecheza kwa kiwango cha juu siku hiyo.

Kipa Alisson alipiga mpira mrefu kwa nahodha huyo, ambaye kisha alimtolea pasi Mohamed Salah aliyedondosha bao la tatu dakika ya 71.

Salah alisukuma ndani bao la nne na la mwisho dakika ya 90 hata baada ya kuzungukwa na mabeki wa Southampton.

Mmisri huyo alivuruga ngome ya wapinzani mara kwa mara akitumia vyema pasi za Firmino, ambaye pia alimchanganya kipa Alex McCarthy kwa makombora makali japo hakuna lililotumbukia wavuni.

Wakati Liverpool wakiandikisha ushindi huo mkubwa, Mtanzania Mbwana Samatta alifunga bao na kusaidia klabu yake ya Aston Villa kuibuka na ushindi wa 2-1.

Nahodha huyo wa Taifa Stars ya Tanzania, alifunga bao la kichwa dakika ya 70 akimalizia mpira wake Keinan Davis.

Ilikuwa mechi ya pili kwa Samatta, 27, baada ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Leicester City katika nusu-fainali ya Carabao Cup, ambapo Villa walishinda na kufuzu kwa fainali ya kombe hilo.