Mzee Moi kuwa rais wa pili kuandaliwa mazishi ya kitaifa
NA MARY WANGARI
RAIS mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi ndiye atakayekuwa rais wa pili kuagwa kwaheri kupitia mazishi yenye heshima kamili ya kijeshi na kiongozi wa sita kufanyiwa mazishi ya kitaifa tangu Kenya ilipoanza kujitawala 1963, kufuatia amri iliyotolewa na rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumanne.
Kulingana na maagizo ya Kiongozi wa Taifa, Mzee Moi atazikwa kwa heshima kamili ya kiraia na kijeshi baada ya kipindi cha maombolezi nchini kilichoanza huku bendera zote nchini zikipeperushwa nusu mlingoto kuashiria maombolezi ya kiongozi huyo.
Bw Moi aliyefariki nyumbani mwake mnamo Jumanne, Februari 4, ataandaliwa mazishi ya kitaifa yanayoambatana na hadhi kamili ya kijeshi katika hafla inayofuata utaratibu na kanuni kali kwa heshima ya viongozi wa mataifa na watu wengine wenye hadhi ya kitaifa.
“Kama ishara ya huzuni nchini bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoti katika Ikulu, majengo ya kitaifa, majengo ya umma na nyanja, ngome za kijeshi, vituo na vyombo vya majini hadi jioni ya siku ya mazishi,” alisema rais Uhuru.
Kulingana na kanuni ni rais pekee anayeweza kutangaza kuhusu kifo cha mtu maarufu anayepatiwa mazishi ya kitaifa.
Bendera kupeperushwa nusu mlingoti, saluti ya ufyatuaji wa risasi kwa heshima ya anayepokea mazishi ya kitaifa baada ya mwili wake kulazwa kaburini ni miongoni mwa mambo mengine yanayohusiana na mazishi ya kitaifa.
Mazishi ya kitaifa aghalabu huvutia vyombo vya habari nchini na kimataifa huku yakihudhuriwa na wajumbe kutoka kote ulimwenguni.
Rais wa kwanza nchini Mzee Jomo Kenyatta ndiye aliyekuwa kiongozi wa kwanza Kenya kupatiwa mazishi ya kitaifa yaliyoambatana na heshima kamili ya kijeshi alipozikwa mnamo 1978 ambapo Mzee Moi atakuwa rais wa pili Kenya kuzikwa kwa utaratibu huo.
Katika mazishi ya kitaifa ya Mzee Kenyatta, mwili wake ulisalia ikulu kwa siku 10 huku kipindi cha maombolezi kikichukua muda wa mwezi mmoja.
Siku ya mazishi, mwili wake ulisafirishwa kutoka Ikulu na kupitishwa katika mitaa ya Nairobi hadi katika Majengo ya Bunge kwa kutumia gari la bunduki lililotumiwa katika mazishi ya Waziri Mkuu Uingereza Sir Winston Churchill mnamo 1965.
Wajumbe 82 wa kimataifa wakiwemo marais 11 ni miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo yaliyoripotiwa kuwa miongoni mwa hafla za kufana zaidi ulimwenguni.
Wakenya wengine maarufu nchini waliopatiwa mazishi ya kitaifa lakini bila utaratibu wa kijeshi ni pamoja na Wangari Maathai ambaye alikuwa mtu wa tatu kupatiwa mazishi ya kitaifa tangu Kenya ilipanza kujitawala.
Mwanaharakati huyo aliyefariki kutokana na saratani mnamo Septemba 25 katika Nairobi Hospital na aliyetajwa na vyombo vya habari kimataifa kama “mwanamke wa mwanzo” alikuwa mwanamke wa kwanza Afrika kushinda tuzo ya Nobeli.
Bi Maathai aliyekuwa mwanamke wa kwanza kupata shahada ya Uzamifu Barani Afrika Mashariki na Kati baada ya kushinda uhisani kwenda kusomea Amerika, alikuwa vilevile profesa wa kwanza mwanamke katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alifunza taaluma ya kutibu wanyama.
Mke wa aliyekuwa rais Mwai Kibaki, Lyucy Kibaki pia alipatiwa mazishi ya kitaifa kufuatia kifo chake katika Hospitali ya Bupa Cromwell Uingereza mnamo Aprili, 2016.
Naibu Rais wa nane Kenya Kijana Wamalwa pia alipatiwa mazishi ya kitaifa alipofariki kutokana na maradhi ya figo mnamo Agosti 2003 katika hospitali ya Royal Free, Uingereza ambapo kifo chake kilitangazwa na aliyekuwa rais Mwaki Kibaki.