• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Serikali yatakiwa kuzima mauaji ya kiholela Pwani

Serikali yatakiwa kuzima mauaji ya kiholela Pwani

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

BARAZA la maimamu na wahubiri nchini (CIPK) limemtaka waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi, kuunda jopo litakalochunguza kwa haraka mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu Pwani.

Baraza hilo lilisema hayo baada ya miili ya wanaume wanne waliodaiwa kupotea katika hali ya kutatanisha kaunti ya Kwale kupatikana katika msitu wa Tsavo ikiwa na majeraha mabaya ishara kuwa waliteswa kabla ya kuuawa.

Mkurugenzi wa baraza hilo Sheikh Khalifa Mohammad, alisema ni aibu kwa vitengo vya usalama, kutotambua anaendeleza mauaji ya watu katika eneo la Pwani licha matukio kuripotiwa.

Alisema mauaji hayo yatalemaza vita dhidi ya ugaidi.

Kulingana na shirika la Haki Africa na Human Development Agenda (HUDA) wanaume hao walitoweka kati ya mwezi wa Novemba na Disemba mwaka jana baada ya kuchukuliwa na watu wanaodaiwa kuwa mafisa wa usalama.

Haki Africa iliwataja wanne hao ni, Juma Said Sarai, Khalfan Linuku (Disemba 22), Abdalla Nassir Gatana (Disemba 22) na Usama Nassir (Novemba 30).

Miili hiyo iliokotwa kati ya tarehe 19 na 20 Januari.

Sheikh Khalifa alisema mauaji ya kiholela yanaweza kuleta chuki baina ya watu na kuwafanya wakose imani na serikali.

“Tunataka Dkt Matiang’i kufanya uchunguzi na kutoa ripoti juu ya mauaji haya, anayetekeleza mauaji haya pia ni gaidi anayepaswa kupigwa vita,” akasema Sheikh Khalifa.

Alieleza vita dhidi ya ugaidi vinapaswa kutekelezwa na Wakenya wote bila kubagua dini, kabila na maeneo.

Alisema ugaidi ni janga linaloleta uharibifu nchini. Hata hivyo alitaka vita hivyo vifanyike katika msingi ya sheria za nchi.

“Mtu akishukiwa kuwa gaidi, yafaa apelekwe kortini. Akipatikana na hatia ahukumiwe. Kuua ama kudhalilisha vijana si sahihi,” akasema.

Aliomba uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ufanywe haraka na wanaoyatekeleza waadhibiwe.

Ripoti zilizotolewa na shirika la Haki Africa zaonyesha zaidi ya watu 50 wameuawa Pwani huku wengine wakitoweka mikononi mwa polisi.

Kwingineko, msichana wa miaka 17 aliyekuwa amekamatwa na polisi yadaiwa alijitoa uhai katika hali tatanishi kwenye seli ya polisi.

Shukran Masha aliyekuwa na ujauzito wa miezi saba, alimsihi mamake waende kuomba ruhusa katika kituo cha polisi cha Bamba, ili aende kuishi na mwanamume aliyempachika mimba.

“Alikuwa anaogopa kuwa wazazi wake wangeshikwa kwenye msako wa kuhakikisha wanafunzi wote waliomaliza darasa la nane wanaingia kidato cha kwanza. Kwa hivyo walipitia kituo cha polisi cha Bamba ili wapate idhini ya kwenda kuishi na mwanamume aliyempachika mimba,” alisema Bi Philister Sauti.

Wazazi wake walikuwa wamemnunua sare za shule na vitabu ili ajiunge shule ya upili ya Kajembe huko Mikindani.

Jumanne, mamake alimpeleka kituo hicho cha polisi na msichana huyo akakamatwa na kuzuiliwa katika seli.

Babake msichana huyo Masha Kazungu alisema walikuwa walikuwa wamempangia amalize masomo yake licha ya ujauzito.

Walimsihi asiende kuolewa sababu ya masomo na umri wake bado mchanga.

“Lakini usiku wa manane nilipigiwa simu kwamba kitinda mimba change ameaga dunia baada ya kujinyonga kwa kutimia hijabu. Nilishtuka sana, hata sina la kusema. Ni pigo kubwa sana kwangu,” alisema.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Kazungu alisema anasubiri upasuaji ili kubainisha kiini cha kifo chake katika kituo cha polisi.

Hata hivyo alisema ana wasiwasi huenda mwanaye alidhulimiwa kingono baada ya damu kuonekana akivuja damu katika sehemu ayke ya siri.

Mwili wake ulipatikana ukininginia kwenye dirisha ya seli hiyo.

You can share this post!

Uhusiano wangu na Moi ulikuwa kama wa baba na mwana –...

Kioja polo akidai kufufua maiti

adminleo