Habari MsetoSiasa

Kifo cha Moi chaibua makovu ya mauaji ya halaiki Wagalla

February 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BRUHAN MAKONG

MAKOVU ya mauaji ya Wagalla mnamo 1984 yameibuka upya kufuatia kuaga dunia kwa aliyekuwa rais wa Kenya wakati huo, Daniel Moi mnamo Jumanne wiki hii.

Kifo cha Mzee Moi kilitokea siku chache kabla ya maadhimisho ya miaka 36 tangu mauaji hayo kufanyika katika Kaunti ya Wajir ambapo rais wapatao 3,000 waliuawa.

Mauaji hayo yalifanyika Februari 1984, wakati vikosi vya usalama vilipowakusanya wanaume kutoka ukoo wa Degodia kwenye harakati za kutafuta silaha haramu.

Watu hao walizuiliwa katika uwanja mdogo wa ndege wa Wagalla kwa siku kadhaa bila chakula wala maji kabla ya wengi wao kupigwa risasi walipojaribu kutoroka.

Mzee Moi alikuwa miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakielekezewa lawama kutokana mauaji hayo.

Viongozi wengine waliolaumiwa kwa mauaji hayo ni Bethuel Kiplagat na G.G. Kariuki, wanaodaiwa kuhudhuria mkutano ulioidhinisha mauaji hayo kutekelezwa. Wawili hao walifariki 2017.

Kufuatia kifo cha Mzee Moi, waathiriwa wanasema kwamba matumaini yao ya kupata haki yanazidi kudidimia.

Bw Bishar Abdille ni mmoja wa waathiriwa na wakati huo alikuwa mwalimu mkuu katika Shule ya Msingi ya Wagalla. Anasema kuwa vikosi hivyo vilimtoa darasani alipokuwa akifunza.

“Nilikuwa darasani nikiendelea na shughuli zangu kama kawaida wakati maafisa hao waliivamia shule nilikokuwa nikifunza. Walinipiga na kunirusha kwenye lori pamoja na wanaume wengine waliokuwa wakipelekwa katika uwanja mdogo wa ndege wa Wagalla. Tulizuiliwa kwa siku sita kabla ya mauaji kufanyika,” akasema.

Bw Abdille aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba licha ya kutokuwa na hatia yoyote, walifanyiwa mateso ambayo anayakumbuka hadi leo.

Alisema waliagizwa kuvua nguo zote na kulala katika uwanja huo kwa siku kadhaa.

Kulingana naye, muda mfupi baada ya kisa hicho, helikopta ilionekana ikipaa katika eneo hilo, hali iliyozua wasiwasi mkubwa miongoni mwa waathiriwa. Alieleza kuwa hilo lilionyesha kwamba kulikuwa na mawasiliano kati ya waliokuwa ndegeni na wanajeshi waliotekeleza mauaji hayo.

Hata hivyo, alisema kwamba hakuna anayefahamu kile wanajeshi hao waliambiwa, kwani baadaye aliwaona wakiwapiga risasi watu waliokimbilia kwenye ua wa uwanja huo. Alisema wale waliojaribu kutoroka walifanya hivyo kutokana na njaa.

Bw Ali Abdille, ambaye pia ni mwathiriwa, alisema kuwa serikali iliwaahidi kwamba itatekeleza ripoti ya Tume ya Haki, Ukweli na Maridhiano (TJRC) ili kuwawezesha kupata haki, lakini hilo halijawahi kutimizwa.