• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Serikali yatoa ratiba ya safari ya kumuaga Moi

Serikali yatoa ratiba ya safari ya kumuaga Moi

NA MARY WANGARI

RAIS wa pili nchini Kenya Daniel Toroitich Arap Moi, atapumzishwa katika mazishi ya kitaifa Jumatano, wiki ijayo nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Wakati huo huo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ametangaza Jumanne kuwa sikukuu ili taifa liweze kumuomboleza rais huyo mstaafu.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua alieleza kwamba Wakenya pia watapata fursa ya kuutazama mwili wa Mzee Moi katika Majengo ya Bunge wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Aliyekuwa Kiongozi wa Taifa atapatiwa heshima kamili ya hafla ya kijeshi inayojumuisha kusafirishwa kwa mwili wa rais huyo wa zamani katika gari maalum lisilopenya risasi , muziki wa heshima kutoka kwa jeshi na saluti 19 za bunduki,” ilisema taarifa hiyo.

Ibada ya Mazishi ya Kitaifa itakayojumuisha madhehebu mbalimbali pia itaandaliwa katika Uwanja wa Nyayo mnamo Jumanne ikiongozwa na Kanisa la African Inland Church (AIC), kabla ya rais huyo aliyetawala Kenya kwa miaka 24, kulazwa nyumbani kwake Kabarak, mnamo Jumatano, Februari 12, 2020.

Kulingana na ratiba iliyosomwa na Bw Kinyua, mwili wa Mzee Moi utatolewa katika Mochari ya Lee Funeral Home Jumamosi saa mbili na dakika tano asubuhi na kusafirishwa katika Majengo ya Bunge ukiwa umefunikwa kwa Bendera ya Taifa.

“Msafara unatarajiwa kutumia mikondo hii: Valley Road, Kenyatta Avenue na kisha Parliament Way. Gwaride la Heshima la Kijeshi litaandaliwa katika Parliament Road msafara huo utakapokuwa ukiingia Bungeni,” ilisema taarifa.

Wakenya watapata fursa ya kutazama mwili wa Mzee Moi utakaolazwa katika majengo ya bunge kwa muda wa siku tatu kuanzia Jumamosi, Februari 8 hadi Jumatatu Februari 10 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, katika shughuli itakayoongozwa na jeshi.

“Kiongozi wa Taifa atawasili katika Majengo ya Bunge Jumamosi, saa nne na robo asubuhi ambapo maafisa wa umma watahitajika kuwa wamewasili kufikia saa nne kasoro robo asubuhi hiyo.

“Umma utaruhusiwa kuingia Majengo ya Umma kutazama mwili kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni. Jeshi litaongoza shughuli hiyo ili kutoa mwelekeo na kuimarisha usalama,” alieleza Bw Kinyua.

Aidha, kulingana na taarifa hiyo, Jumanne itakuwa Sikukuu ili kuwapa Wakenya fursa ya kutafakari kuhusu nyakati zake Mzee Moi huku wananchi wakihimizwa kupanda miti au kushiriki vitendo vya ukarimu kwa heshima ya mwendazake.

Hafla hizo za kitaifa zitakazohusisha matawi yote ya serikali na maafisa wote wa umma, zitapeperushwa kwenye runinga na idhaa zote za kitaifa za redio nchini huku wakazi wa kaunti ya Nakuru na Baringo wakipata nafasi maalum.

“Kutokana na jinsi Mzee Moi alivyoenzi wakazi wa kaunti ya Nakuru na Baringo ambao alikuwa amewakilisha moja kwa moja katika baraza la kisheria na baadaye bungeni kwa miongo mitano: vituo vya upeperushaji habari vitawekwa katika maeneo maalum mjini Nakuru, Sacho, Ravine na Kabarnet ili kuwapa wakazi fursa ya kufuatilia Ibada ya Kitaifa na Shughuli ya Mazishi ya Kitaifa,” taarifa hiyo iliongeza.

You can share this post!

Moi alichukia ulevi, asema mjukuu wake

Rais aagizwa na mahakama aapishe majaji walioteliwa

adminleo