• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Thawabu anazopata Muumin anapomtembelea mgonjwa

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Thawabu anazopata Muumin anapomtembelea mgonjwa

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambaye ukubwa na uwezo wake hauna tamthili, Mlezi wa walimwengu wote, na Mfalme wa siku ya malipo.

Rehema na amani zimshukiye Mtukufu wa daraja, kielelezo chetu na kipenzi cha Allah, asiyezungumza kwa utashi wa nafsi yake, Mtume Muhammad swallallahu alayhi wasallam na Swahaba zake kiram na Waislamu kwa jumla.

Leo hii insha Allah tutapambanua japo kwa akali faida na umuhimu wa kumzuru mgonjwa hospitalini au nyumbani au popote anapougulia. Alhamdulillah, dini ya Kiislamu haijasaza chochote katika mafundisho yake mazuri yenye kukuza mahusiano na imani ya mtu. Ni mfumo mzima wa maisha, ziara kwa wagonjwa ni mojawapo ya mwenendo mzuri wa Kiislamu.

Kila siku tunapomwomba Mola wetu dua, huwa tunamtaka atupe afya njema duniani na akhera. Ama kupata maradhi ni mtihani kutoka Kwake na inamhitaji mja kuwa na subira ya hali ya juu kwani hata hivyo anavyougua, anapunguziwa madhambi. Sisi tulio hai na wenye afya hatuna budi Kuwatembelea wagonjwa, wawe Waislamu au si Waislamu.

Mtume Muhammad swallallahu alayhi wasallam asema kuwa Mwislamu ana haki tano juu ya mwingine. Mojawapo wa haki hizo ni kumtembelea akiwa mgonjwa.

Ziara hiyo humfanya mtembelewa kuhisi kuwa angali na matumaini ya kuishi na vilevile huimarisha siha yake. Mwenye kutembelea mgonjwa anafaa kumwombea shifaa na kutochukua muda mrefu sana kwenye eneo alilo mgonjwa.

Baadhi ya dua za kumwombea mgonjwa ni kama vile As-alu Llaha l-adhiym, rabbal a’arshi l-adhiym an yashfiyak. Unafaa kupagusa anapougua mgonjwa kisha usome dua hiyo mara tatu na Inshallah Mwenyezi Mungu atampa shifaa.

Ndugu mu’umin, Mtume swallallahu alayhi wasallam aliwahi kumtembelea adui yake aliyezoea kumfanyia maudhi kwenye njia aliyokuwa akipita Rasul Swallallahu Alayhi wasallam.

Hii ni ishara tosha kuwa tunafaa kuwatembelea hata wale tunaokisia kuwa ni maadui zetu. Hii hatimaye itajenga mwamana na mlahaka mzuri na huenda joto la uhasama kati yenu wawili likayeyuka.

Utagundua kuwa kumtembelea mgonjwa ni darsa kubwa kwani moyo wa mu’umin hutaka kurejea kwa Mola wake na kufanya istighfaar kabla ya kupatikana na hali kama hiyo. Na mwenye kufanya ibada hiyo, hupata fadhila kubwa mno, ikwemo kuombewa na malaika 70,000 tangu anapoanza ziara hiyo hadi anapoimaliza.

Kwa bahati mbaya, leo hii waislamu wengi hawana muda wa kuwatembelea wagonjwa, wamejitia shughuli zisizoisha, pasina kujua kwamba leo mgonjwa ni yule na kesho ni yeye.

Utamsikia tu akisema kuwa atampigia simu au akizidi kuahirisha matembezi hayo. Hilo halifai abadan.

Si hayo tu, wanasema kuwa rafiki mwema ni dawa kwa mgonjwa. Mwenye kumtembelea mgonjwa aliye sahibu wako aweza kupona kutokana na kukuona. Hivyo ni muhimu sana kufanya juhudi ya kuhusisha ziara kwa wagonjwa katika shajara yako. Fadhila ni kubwa!

Muislamu kwa Muislamu mwenzake ana haki 7, haki hizo kama hakuitekeleza moja , mtu huyo ametoka kwenye himaya na ulinzi wa Mungu. Miongoni mwa haki hizo ni kumsalimia mgonjwa na kushiriki katika mazishi yake au ya ndugu yake.

Mtume anasema: “Muislamu yeyote anayetoka kwenda kumtembelea mgonjwa, Allah humwambia hongera kwa kitendo chako cha kwenda kumtembelea mgonjwa na chagua mahali peponi nikuweke. Hakuna muumini ambae anamtembelea ndugu yake mgonjwa.

Adabu za kumtembelea mgonjwa

1. Kubeba zawadi

2. Kukaa muda mfupi

3. Muulizie hali yake kwa lugha nzuri, usiache kumpa mkono na kumgusa.

4. Kumpa moyo na lugha nzuri, muoneshe huruma na matarajio.

5. Kutokula chakula mbele yake.

You can share this post!

Abidal amulika Auba’ baada ya kuponea kisu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Suala la dini halifai kupuuzwa katika...

adminleo